Akihutubia wananchi watakaopitiwa na mradi huo, Dar es Salaam, jana Mstahiki Meya wa Halmshauri ya Manispaa ya Kinondoni, Benjamini Sitta alisema , fidia hizo zitaanza kutolewa kuanzia leo tarehe 04/09/2017 kwa watu waliokamilisha tararibu zote ikiwemo kuthaminiwa, kuhakikiwa na kufungua akaunti.
Aliwahakikishia wananchi hao kuwa kila mwananchi aliyepitiwa na mradi huo atapata stahiki yake kama eneo lake lilivyo thamaniwa.
Alisema utekelezaji wa DMP ulisimama katika baadhi ya maeneo kutokana na kukosa fedha za kulipia fidia na sasa utaanza kutekelezwa katika maeneo yaliyopata idhini.
“Utekelezaji wa mradi huu wa DMP unafanywa kwa awamu kulingana na mpango wa manunuzi uliokubaliwa na benki ya dunia na serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na halmashauri ambapo katika mwaka wa fedha 20016/17 miradi iliyoanza kutekelezwa ni ujenzi wa barabara tano za awamu ya kwanza ambazo hazikuhitaji fidia kati ya barabara 11 zinazotakiwa kujengwa ambazo ni Makumbusho- Sokoni, MMK, Nzasa na TANESCO, Soko la samaki Msasani na barabara ya viwandani,” alisema Meya Sitta.
Alisema mradi huo ulianza kutekelezwa Kinondoni mwaka 2010 kabla ya kuanziashwa kwa wilaya ya Ubungo, ambapo barabara zinazohusika ni Makumbusho- Sokoni yenye urefu wa Kilomita 1.45, MMK yenye urefu wa Kilomita 0.9, Nzasa Kilomota 1.2, TANESCO – Msasani soko la samaki Kilomita 1.67 Viwandani Kilomita 2.1, Makanya Kilomita 5.10, Simu 2000 Kilomita 0.80, Kilimani Kilomita 1.80,Tandale -Kisiwani Kilomita 1.30, Maji chumvi-Kilungule Kilomita 3.00 na Kilongawima Kilomita 1.80.
“Kati ya barabara hizo barabara tano za Makumbusho – Sokoni , MMK, Nzasa , TANESCO-Soko la Samaki na Viwandani tayari zimejengwa kwa kiwango cha lami,”alisema Sitta.
Alisema uboreshaji miundombinu katika maeneo ambayo hajapangwa unakusudia kuboresha makazi ya wananchi hasa wenye kipato cha chini na utahusisha kata tatu ambazo ni , Tandale, Mwananyamala katika Manispaa ya Kinondoni na Kata ya Mburahati Latina Manispaa ya Ubungo.
“Uboreshaji huu utahusisha miradi ya ujenzi wa madaraja, barabara, njia za waenda kwa miguu, taa za barabarani , vizimba vya taka ngumu na vituo vya mabasi,”alieleza Meya huyo.
“Ninamshukuru Rais Dk. John Magufuli na benki ya dunia kwa kutoa fedha hizi za fidia kwani hatua hiyo itawezesha kuboresha miundombinu na kukabiliana na changamoto kubwa za usafiri na wananchi kuishi maisha bora na kuwa suluhisho la majanga yatokanayo na mvua,”alisema Meya Sitta.
Kwa upande wa Mkuu wa Dar es salaam, Paul Makonda amesema mradi huo utafanya jiji la Dar es Salaam kuendelea kuwa la kisasa na kufikia azma yake ya Dar Mpya.
Amewataka wananchi watakaolipwa fidia kuhakikisha wanazitumia fedha hizo vizuri kwa kufungua miradi itakayowaingizia kipato.
Aidha Makonda amesema kuwa Kata za Tandale, Mburahati na Mwananyamala zitaingizwa kwenye idadi ya Kata 14 zinazopandishwa viwango kwa kuwa Barabara za kisasa maana ya kuwa na Lami,Taa na Mitaro ya Maji.
Makonda amempongeza Meya wa Kinondoni Benjamin Sitta na Manispaa hiyo na kuwataka kuhakikisha kila anaestahili kulipwa fidia analipwa kile anachostahili bila usumbufu.
Bongo5