Picha hii inajulikana kwa jina la Defeated Soldier yaani, "Mwanajeshi Aliyeshindwa" Ni ukumbusho wenye nguvu kwamba vita haviishii kwa askari kuacha silaha tu, bali athari zake huendelea kuishi katika magofu, familia zilizotengana na maisha yaliyovunjika.
Mnamo tarehe 4 Machi 1947, mpiga picha wa Marekani Tony Vaccaro alipiga picha yenye huzuni kubwa ya mwanajeshi wa zamani wa Ujerumani aliyerudi nyumbani baada ya kuwa mfungwa wa vita nchini Marekani.
Alipofika kwao Frankfurt, Ujerumani, alikuta nyumba ya familia yake imegeuka kuwa magofu kutokana na mashambulizi ya mabomu ya Vita vya Pili vya Dunia, hivyo hakumkuta mkewe wala mtoto wake.
Mwanajeshi huyo alitarajia kurudi kwa familia yake baada ya miaka ya vita na kifungo, lakini badala yake alikutana na uharibifu na maumivu makubwa.
Tony Vaccaro baadaye alieleza kuwa mwanajeshi huyo alikuwa akilia, huku akisema vita ilikuwa imeharibu nyumba yake na maisha aliyokuwa akiyafahamu hapo kabla.
Wakati mwingine, mtu anaweza kuishi vitani na kushinda kifo, lakini akirudi nyumbani akakuta maisha aliyokuwa akipigania hayapo tena.