Kutoka gazeti la Mtanzania
MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amekibomoa Chama cha Wananchi (CUF) Mjini Mtwara, baada ya kuzoa wafuasi zaidi ya 463 wa chama hicho.
Miongoni mwa walioihama CUF, ni aliyekuwa mgombea ubunge wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, Abdallah Uledi na Kiongozi wa Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Mtwara, Mussa Abdallah.
Kutokana na wingi wa wafuasi hao, Mbatia, ambaye alikuwa na jukumu la kupokea kadi za CUF na kuwagawia wanachama wapya kadi za NCCR- Mageuzi, alizidiwa uwezo na badala yake kukaimisha jukumu hilo kwa wasaidizi wake, wakiwamo Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali na Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar, Mussa Kombo Mussa.
Hata hivyo, zoezi la kugawa kadi hizo halikumalizika kutokana na wingi wa wananchi na pia Mbatia alikuwa akiwahi kwenda kufungua tawi jipya eneo la Majengo, Ilala, mjini Mtwara kabla giza halijaingia.
Tukio hilo, lilitokea jana wakati Mbatia alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Vigaeni, vilivyoko eneo la Chikongola, Mjini Mtwara.
Mbatia, mshauri wake mkuu, Danda Juju, Machali, Kombo, pamoja na viongozi wengine wa ngazi za juu wa chama hicho, wako katika ziara ya kukijenga chama mkoani Mtwara.
Wakati wa kuwapokea wanachama hao, Uledi alionekana kuwa kivutio kikubwa kwa kuwa wakati alipokuwa akieleza sababu za kuhamia NCCR-Mageuzi, mamia ya wananchi waliokuwa katika mkutano huo, walikuwa wakilipuka kwa shangwe na vigelegele wakionyesha kuungana naye. Uledi ndiye aliyekuwa mpinzani mkuu wa Mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnain Murji (CCM), wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
Akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano huo, Mbatia alisema Watanzania, wakiwamo wakazi wa Mtwara, wanaishi maisha magumu kutokana na tabia yao ya kutotaka mageuzi ya kisiasa.
"Mtwara mna utajiri wa kutosha, nyie mna gesi lakini gesi haiwanufaishi, badala yake sasa inapelekwa Dar es Salaam, nyie mnalima korosho na mna utajiri mwingi tu, lakini kwa sababu hamtaki mageuzi ya kisiasa mmekuwa mkiwachagua CCM kila uchaguzi unapofika. "Badilikeni kama kule Kigoma, walikuwa nyuma sana kimaendeleo, Kigoma hawakuwa na barabara na pia Mkoa wa Kigoma ulikuwa ni moja ya mikoa iliyokuwa nyuma kimaendeleo kwani hawakuwa hata na umeme.
"Lakini Kigoma walipokubali mageuzi, walipokubali kuwachagua wapinzani, sasa Kigoma wana barabara nzuri za lami na hivi sasa wanapelekewa umeme wa uhakika tofauti na nyinyi."
Mbatia alizungumzia zao la korosho na kusema anashangaa kuona korosho ya Tanzania inauzwa bei kubwa katika maduka ya kisasa jijini Dar es Salaam, wakati bei ya zao hilo kwa wakulima iko chini.
Kwa mujibu wa Mbatia, bei ya nusu kilo ya korosho katika baadhi ya maduka jijini Dar es Salaam ni Sh 10,500 na kwamba bei ya zao hilo nchini Uholanzi ni Sh 24,000 kwa kilo.
Kutokana na hali hiyo, alisema Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho, Anna Abdallah na Makamu wake, Mudhihiri Mudhihiri, hawawasaidii wakulima wa zao hilo, badala yake wanashika nafasi hizo kwa masilahi yao binafsi.