Katika uhusiano baina ya mume na mke hutokea mambo mbalimbali yanayoimarisha uhusiano baina yao au kuuharibu. Baadhi ya nyakati mwanaume hufanya baadhi ya mambo yanayomshusha thamani mbele ya mwanamke. Hivyo, wanaume wote wenye khofu ya heshima na thamani yao kuanguka, ninawaletea mambo muhimu ambayo yanashusha thamani ya mwanaume mbele ye mwanamke:
1. HADAA NA UNYONYAJI:
Baadhi ya wanaume ni wazuri sana katika kumnyonya mwanamke kwa kutumia kisingizio cha mapenzi. Wanazitumia mali zake na kuzinyonya kwa kutumia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na maneno matamu ya mapenzi au kutengeneza simulizi za uongo kuhusu matatizo ya kipesa na kiuchumi. Mwanamke akigundua kuwa analaghaiwa, basi atamshusha thamani haraka mwanaume huyo na kuamua kujitenga naye. Na iwapo ataendelea kuwa naye, basi hasara na majuto yatakuwa juu ya mwanamke huyo.
2. WANAWAKE WENGI:
Mwanamke anapenda ahisi kuwa yeye ndiye mtu pekee katika maisha ya mwanaume. Kuwa na uhusiano na wanawake wengi wasiokuwa na ukomo, husababisha katika kushusha heshima yake mbele ya mkewe. Tambua kuwa hiyo sio sifa nzuri ya kujivunia.
3. UONGO:
Urongo ni miongoni mwa mambo ambayo mwanamke huchukia sana kuyaona kwa mwanaume. Kuna wanaume hodari katika kutunga na kusema uongo. Lakini mwanamke akigundua kuwa unamuongopea, basi heshima na thamani yako itakuwa imeshuka kabisa machoni mwake hata kama ataamua kuendelea kuishi nawe.
4. UKOSEFU WA HESHIMA:
Utovu wa heshima ni miongoni mwa mambo yanayoharibu uhusiano maridhawa baina ya wanandoa hata kama kutakuwa na mambo yanayowaunganisha. Hivyo, ewe mwanaume mwenzangu, usiishushe haiba ya mkeo kwa lugha chafu au kumdhalilisha. Usishushe thamani ya vitu anavyovifanya kwa ajili yake hata kama vitakuwa vidogo. Daima jitahidi kuwaheshimu ndugu zake kwa sababu ukifanya kinyume na hivyo, thamani yako mbele yake itashuka, hata kama hatakwambia.
5. KUTOMUAMINI:
Kuaminiana ni miongoni mwa mambo mazuri ambayo yakipatikana katika mapenzi ya wawili, huwasaidia kukabiliana na vikwazo na changamoto mbalimbali. Ikiwa mume ni mtu anayetilia shaka maneno na matendo ya mke kila siku, thamani yake machoni mwa mkewe itashuka. Kuaminiana kuna mafungamano makubwa sana na upendo na kujiamini. Iwapo kutakuwa na ulegevu katika jambo hilo, mahabba yao hayatakuwa maridhawa.
Ndoa Maridhawa