Swali ulilouliza, jibu nitakupatia,
Tulia nitakujuza, si gumu nakuambia,
Ya mamba unauliza, wa kijiji nachangia,
Mamba asiyeng'ata, si mamba huyo mjusi!
Huyo mamba asong'ata, lazima awe mjusi,
Asiyeweza kunyata, mwenye rangi za tausi,
Mwenye mwendo kama bata, na macho kama mkisi,
Mamba asiyeng'ata, si mamba huyo mjusi!
Macho anavyokodoa, kama kabanwa mlango,
Mjusi kajipodoa, na nyororo yake shingo,
Kelele anazotoa, na mwendo wenye malingo,
Mamba asiyeng'ata, si mamba huyo mjusi!
Beti nne nazifunga, jawabu nimemaliza,
Kama gwiji nimepanga, msije kuniuliza,
Mjusi nimemnanga, nang'ata sijapuliza,
Mamba asiyeng'ata, si mamba huyo mjusi.
Na. M. M. Mwanakijiji (Tarumbeta ya Kijiji).
Uhamishoni USA