Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Samia Suluhu amesema kamwe Serikali haitagawa chakula kwa wananchi wavivu ambao hawataki kufanya kazi na kusubiri chakula kutoka serikalini.
Samia ametoa kauli hiyo wakati akihutubia mamia ya wananchi wa Manispaa ya Musoma katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mukendo mjini Musoma.
Amesisitiza kuwa Serikali itapeleka chakula kwa wananchi ambao mazao yao yaliharibiwa kwa mvua au yalikauka kwa ukame au kwa maafa mengine na sio kwa wananchi wanaokaa vijiweni mchana kutwa bila kufanya kazi wakisubiri neema ya chakula kutoka kwa serikalini.
Amewahimiza wananchi kote nchini kuendelea kufanya kwa bidii ikiwemo shughuli za kilimo na pindi wanapovuka wajiwekee akiba na waache tabia ya kuuza mazao yote wanayovuna ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa chakula kwenye familia zao.
Makamu wa Rais pia amewataka viongozi wa Mkoa wa Mara washirikiane na wananchi katika kuwaelemisha mbinu bora za kilimo ili waweze kupata mazao mengi ikilinganishwa na hali ilivyo kwa sasa.
Chanzo: Mwananchi