Mohamed Omary, mkazi wa Kimamba A wilayani Kilosa amefikishwa mahakamani katika mahakama ya Hakimu mkazi Mkoa wa Morogoro na kusomewa mshtaka manne likiwemo mauaji na ubakaji.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi Renatus Barabara, mwendesha mashtaka wa Serikali, Elizabeth Malya, amesema kesi namba 8108/2024 inahusu mtuhumiwa kumuua mpenzi wake, Beatrice Ngongolwa.
Katika kesi namba 8101/2024 mshatakiwa kwa nyakati tofauti anadaiwa kumfanyia vitendo vya ukatili mtoto wa marehemu mwenye miaka 9 kuanzia Aprili 2023 hadi Machi 2024, ambapo alimjeruhi kwa kumng’oa meno mawili, kumchoma kwa kutumia kifaa chenye moto mapajani, kumchoma kwa misumari pamoja na kumpiga rungu kichwani.
Kesi ya mauaji namba 8108/2024, Elizabeth amesema mshtakiwa anadaiwa kumuua mke wake Beatrice Ngongolwa Januari Mosi mwaka 2024 na kumfukia ndani ya chumba chake.
Kwenye shtaka hilo, mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo kisheria ya kusikiliza kesi ya mauaji.
Shtaka la ubakaji namba 1112/2024 Mstakiwa anadaiwa kumbaka mtoto wa kike wa marehemu mwenye miaka 12 kinyume cha sheria.
Shauri namba 8113/2024 mshtakiwa anadaiwa kumfanyia ukatili mtoto wa kiume wa marehemu mwenye miaka tisa ambapo alimng’oa meno, kumchoma mdomo na makalio na kumtengua kiwiko na kumtoboa kwa misumari sehemu zake za siri.
Mtuhumiwa huyo amekana mashtaka mawili ya ukatili na ubakaji. Amerudishwa rumande mpaka Machi 28, ambapo shtaka la ukatili na ubakaji litakapotajwa tena, huku lile la mauaji likipangwa kutajwa tena Aprili 9 mwaka huu.