Wafuasi wa mgombea urais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye wamejitokeza katika mitaa ya mji mkuu, Dakar, kusherehekea matokeo ya awali ya uchaguzi uliofanyika jana, Machi 24, 2024, yakionyesha mgombea huyo wa upinzani anaongoza.
Sherehe hizo zilifanyika huku wagombea wasiopungua watano kati ya 19 katika kinyang’anyiro hicho wakitoa taarifa za kumpongeza Faye kwa kile walichokiita ushindi wake.
Hata hivyo, mpinzani wake mkuu kutoka muungano unaotawala, Waziri Mkuu wa zamani, Amadou Ba, amesema sherehe hizo zilikuwa kabla ya wakati wake.
“Kwa upande wetu, na kwa kuzingatia mrejesho wa matokeo kutoka kwenye timu yetu ya wataalamu, tuna uhakika kwamba, katika hali mbaya zaidi, tutaenda kwenye duru ya pili,” timu ya kampeni ya Ba imesema katika taarifa yake.
Hakukuwa na maoni ya moja kwa moja kutoka kwa Faye mwenyewe.
Mamilioni ya wananchi wa Senegal walipiga kura Jumapili kumchagua Rais wa tano wa nchi hiyo.
Hatua hiyo ilifuatia baada ya miaka mitatu ya msukosuko wa kisiasa ambayo haijawahi kushuhudiwa ikiwamo maandamano dhidi ya Serikali na kuungwa mkono kwa upinzani.
Kuna uwezekano wa kumalizika kwa utawala wa Rais anayemaliza muda wake, Macky Sall ambaye anaondoka madarakani baada ya muhula wa pili uliokumbwa na machafuko kutokana na kufunguliwa mashtaka kwa kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko.
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa