Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Geita inaendelea kuchunguza safari ya China aliyokwenda aliyekuwa Mkurugenzi wa Mji wa Geita, Zahara Michuzi ambaye Desemba mwaka jana alihamishiwa Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
Uchunguzi huo ulioanza mwanzoni mwa Novemba 2023 ulitokana na agizo la Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe aliyelitoa mwishoni mwa Oktoba, 2023 la kuitaka taasisi hiyo kuchunguza safari ya Mkurugenzi aliyekwenda nchini China kama ilikuwa kwa masilahi ya halmashauri au binafsi.
Pia aliitaka taasisi hiyo kubaini kama matumizi ya safari hiyo yalitokana na fedha za halmashauri au binafsi na endapo watabaini alitumia fedha za Halmashauri zirejeshwe na zielekezwe kutekeleza miradi ya maendeleo.
Akizungumza jana Januari 30, 2024 Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, Azza Mtaita amesema uchunguzi huo umechukua muda mrefu kwa kuwa ni wa mtu mkubwa kwenye taasisi, lakini pia fedha zilizochukuliwa ni nyingi.
Kuhusu uhamisho wake kama unaathiri uchunguzi Mtaita amesema kuhamishwa kwake ni faida kwa timu ya uchunguzi kwa kuwa imewapa uhuru watumishi wanaopaswa kutoa ushahidi, na kuifanya Takukuru kufanya kazi kwa kina zaidi.
“Ni kweli uchunguzi umechukua muda mrefu kwa kuwa naye ni mkubwa na fedha alizochukua ni nyingi na kuna mambo ambayo tunatakiwa tuyahakikishe, ni bora kuchukua muda mrefu kupata matokeo chanya.
“Hata chakula kilichopikwa muda mrefu ladha yake ni tofauti na ile ya haraka unapoandaa kitu muda mrefu kinakuwa na matokeo mazuri,” amesema Mtaita.
Hata hivyo, amesema uchunguzi utakapokamilika utatolewa kama wanavyotoa taarifa nyingine walizozifanyia kazi.