Kumbukumbu la torati
Maagizo kuhusu fungu la kumi
22 Usiache kutoa zaka ya fungu la kumi katika mavuno yote ya mbegu zako, yatokayo shamba mwaka baada ya mwaka. 23 Nawe utakula mbele za BWANA, Mungu wako, mahali atakapochagua apakalishe jina lake, zaka ya nafaka zako, na divai yako, na mafuta yako, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yako ya ng'ombe na ya kondoo; ili upate kujifunza kumcha BWANA, Mungu wako, daima. 24 Na njia ikiwa ndefu mno nawe, usiweze kuzichukua kwa kuwa mahali ni mbali nawe mno atakapochagua BWANA, Mungu wako, apakalishe jina lake, hapo atakapokubarikia BWANA, Mungu wako; 25ndipo uzibadili ziwe fedha, na kufunga zile fedha uende nazo mkononi mwako, hata mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako; 26na zile fedha zitumie kwa chochote itakachotamani roho yako, ng'ombe, au kondoo, au divai, au kileo, au roho yako itakacho kwako chochote; nawe utakula huko mbele za BWANA, Mungu wako; tena furahi, wewe na nyumba yako; 27 na Mlawi aliye ndani ya malango yako usimwache, kwani hana fungu wala urithi pamoja nawe.
28 Kila mwaka wa tatu, mwisho wake, toa fungu la kumi lote la mavuno yako ya mwaka huo, uliweke ndani ya malango yako; 29 na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na kushiba; ili kwamba BWANA, Mungu wako, akubarikie katika kazi yote ya mkono wako uifanyayo.