Mafia ni utata mtupu:
Katibu wa CCM Wilaya ya Mafia mkoani Pwani, Salehe Kikweo, amelazimisha kurudiwa kwa kura katika ofisi za chama wilayani chini ya usimamizi wake mwenyewe.
Taarifa kutoka Mafia zinaeleza kwamba marudio ya uchaguzi huo yaligubikwa na mizengwe ya kila namna, ikiwapo Katibu kutangaza kurudiwa kwa uchaguzi usiku wa manane katika ofisi za wilaya kinyume cha taratibu za uchaguzi.
Ilidaiwa kuwa Kikweo alimpigia simu Katibu wa tawi la Kilindoni, Emmanuel Luvanda, Agosti 10, majira ya saa 5:00 usiku na kumtaarifu kwamba uchaguzi katika tawi hilo ungerudiwa kesho yake yaani Agosti 11, saa 4:00 asubuhi.
Taarifa zaidi zinaeleza kwamba Luvanda alijaribu kumsihi Katibu huyo kurekebisha tarehe ya uchaguzi huo mdogo ili kutoa taarifa kwa wanachama, jambo ambalo hata hivyo lilipingwa na Kikweo.
"Ndipo Luvanda akanipigia mimi kama mmoja wa wajumbe na kunitaarifu juu ya taarifa hizo...asubuhi ya jana (juzi) tukaamka kuwaambia wanachama kwamba kuna uchaguzi, walioweza kujitokeza walikuja tawini kwa ajili ya kupiga kura," alisema mjumbe wa siasa wa tawi la Kilindoni, Ahmad Kubenea.
Kubenea alifafanua kuwa Kikweo alitaka uchaguzi huo usimamiwe na kamati ya siasa ambayo ilikataa jukumu hilo ndipo aliamua kuusimamia kwa kuanza kuita majina ya wanachama ambao walianza kupigakura.
"Zoezi limekwenda lakini baada ya muda mfupi vijana wakabaini kwamba kuna watu wanaweka kura mbilimbili wakatoa taarifa kwa Katibu (Kikweo) ambaye aliamua kuchukua ndoo ya kura na kuichoma moto...akatangaza tena kwamba uchaguzi utafanyika wilayani saa 8:30 mchana, huko kura zilipigwa hadi saa 5:00 usiku," alisema.
Hata hivyo, alisema baadhi ya wanachama walizuiwa kushiriki zoezi hilo kwa madai kwamba majina yao hayapo kwenye orodha ya daftari la wapigakura.
Taarifa zaidi kutoka Mafia, zinaeleza kwamba mbunge aliyemaliza muda wake, Abdulkarim Shah, juzi hiyo hiyo alikata rufaa kulalamikia mchezo huo na kupeleka nakala yake kwa viongozi wakuu wa chama hicho.
Katibu wa CCM tawi la Kilindoni, Luvanda, alithibitisha kuwepo kwa tafrani hiyo na kueleza kwamba majira ya saa 4:30 usiku wanachama walizuiwa kupigakura.
Source: IPP Media.