Makamba akimbila Tanga baada ya Operesheni Sangara

Regia Mtema

R I P
Nov 21, 2009
2,970
864
CCM yatikiswa Tanga
• Makamba, Bendera waenda kuweka mambo sawa

na Asha Bani


amka2.gif
MIKUTANO ya Operesheni Sangara ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyomalizika hivi karibuni mkoani Tanga na ile ya Operesheni Zinduka ya Chama cha Wananchi (CUF), imekitikisa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kubadili kabisa upepo wa kisiasa mkoani humo, ikiwa ni miezi 11 tu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwakani, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Katika uchaguzi mkuu uliopita, CCM ilishinda ubunge katika majimbo yote 11 mkoani Tanga na kujipambanua kama chama chenye nguvu kubwa ya kisiasa mkoani humo, licha ya kuwapo kwa malalamiko ya vyama vya upinzani kwamba kilipata ushindi huo kwa kufanya hujuma na dhuluma.
Hata hivyo, uchunguzi wa hali ya kisiasa ya kabla na baada ya vyama vya upinzani kufanya harakati za kisiasa mkoani humo katika miezi ya hivi karibuni, umeonyesha dhahiri chama hicho kikongwe kupoteza umaarufu wake kiasi cha kuhofia majaliwa yake katika uchaguzi mkuu ujao.
Katika hali inayoashiria CCM kuhofia ushindani mpya wa kisiasa uliowekezwa Tanga hivi karibuni, makada maarufu wa chama kutoka Dar es Salaam, wakiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba, walifunga safari kwenda mkoani humo kwa ziara ya kisiasa, ikiwa ni siku moja tu baada ya viongozi wa CHADEMA kumaliza ziara yao mkoani humo.
Mwingine aliyekuwa katika msafara huo ni Naibu Waziri wa Utamaduni na Michezo, Joel Bendera, ambaye alikwenda moja kwa moja jimboni kwake Korogwe kuweka mambo sawa baada ya CHADEMA kufanya kazi ya siasa jimboni humo na kuendelea kuwatuhumu viongozi wa CCM kwa kukumbatia ufisadi.
Katika ziara yake hiyo, Bendera alitoa zawadi ya vifaa vya michezo kwa baadhi ya wananchi wa jimbo lake, hatua inayotafsiriwa kuwa jitihada za kujibu mapigo ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa, ambaye akihutubia katika Kijiji cha Kilole katika jimbo hilo, alimshutumu mbunge huyo kwa kuwasahau wananchi wake ikiwa ni pamoja na kushindwa hata kuwapatia kiwanja cha michezo licha ya kuwa ni waziri mwenye dhamana na michezo nchini.
Mvuto mpya wa kisiasa umeibuka mkoani humo, hasa baada ya Bendera kuwa miongoni mwa wabunge walioshutumiwa vikali na wapinzani, kwamba wamewasahau wananchi wa majimbo yao.
Hofu ya CCM dhidi ya nguvu ya upinzani mkoani humo ilijionyesha dhahiri hata wakati mikutano ya vyama hivyo vya upinzani ikiendelea mkoani humo kwa nyakati tofauti.
Wakati CHADEMA ikiendelea na mikutano yake hiyo hivi karibuni, baadhi ya wakuu wa wilaya za mkoa huo wanaoaminika kuwa ni makada wa CCM, walituma ujumbe kwa waandishi wa habari wakiwashutumu kwa kuripoti habari za Operesheni Sangara iliyokuwa ikiendelea katika wilaya zao.
Moja ya ujumbe wa simu ya mkononi (sms) kutoka kwa mkuu mmoja wa wilaya kwenda kwa mwandishi wa habari wa kituo kimoja cha umma, ulisomeka hivi; “Hivi ni wewe unayefanya ‘coverage’ ya CHADEMA kupita kazi zetu unazotufanyia ambazo ndizo zinakuhusu?”
Aidha, uongozi wa Mkoa wa Tanga nao ulidaiwa kuiandikia barua Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) wakitaka iondoe kibali cha usafiri wa helikopta ya CHADEMA mkoani humo, kwa madai kuwa ilikuwa inahatarisha usalama, hatua ambayo ilitafsiriwa na wadadisi wa mambo kuwa, walikuwa wakijaribu tu kukibana chama hicho baada ya kutishwa na mwamko wa umma kwa Operesheni Sangara.
Hata hivyo, chama hicho kilifanikiwa kumaliza operesheni yake mkoani humo na kuhamia Same bila kuzuiwa kutumia helikopta.
Katika mikutano hiyo ya CHADEMA, sawa na ilivyokuwa kwa mikutano ya Operesheni Zinduka ya CUF, mamia ya wananchi walihudhuria na kujiunga na vyama hivyo katika vijiji na miji ya mkoa huo, wakiwemo wale wa Tanga mjini.
Kwa upande wake, CUF nayo ilizidi kujiimarisha mkoani humo kupitia mikutano yake iliyoifanya Oktoba mwaka huu, ambapo ilishuhudiwa ikipata mahudhurio makubwa na kuvutia wanachama wapya.
Kwa ujumla, kupitia Operesheni Sangara, CHADEMA ilifanikiwa kujipenyeza kwa kishindo kwa mara ya kwanza katika mkoa huo na kuvuna wanachama wapya, licha ya kuwa ni moja ya ngome za CUF.
Katika mikutano yake, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, aliwaambia wakazi wa mkoa huo kwamba chama chake hakikwenda kuibomoa CUF bali kuimarisha upinzani, hivyo kufanikiwa kuvutia mamia ya wanachama wapya kujiunga na chama hicho.
 
Back
Top Bottom