Makahaba: Usiombe kukutana na polisi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Makahaba: Usiombe kukutana na polisi

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by kilimasera, Jan 29, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Jan 29, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  MAPAMBANO dhidi ya Ukimwi yanaendelea kwa kasi nchini, elimu, matangazo ya kuhimiza uaminifu na kujikinga, upimaji wa hiari pamoja na uwepo wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) ni baadhi tu.

  Lakini pamoja na juhudi hizo, kuna kundi katika jamii ambalo halijatiliwa maanani katika mapambano hayo hali inayosababisha liwe chanzo kikuu cha maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
  Makahaba au wafanyabishara ya ngono ni kundi ambalo limekuwa likipewa mtazamo hasi na jamii na hata serikali.

  Licha ya kunyanyapaliwa, huchukuliwa kama wahalifu na hilo huwatia hofu ya kukosa fursa ambazo wananchi wengine huzipata zikiwemo elimu ya Ukimwi, uzazi wa mpango na njia za kujikinga na maambukizi ya VVU.

  Mbali ya hayo, makahaba hupata manyanyaso ya hali ya juu kutoka kwa wateja ambayo huchangia kuenea kwa maambukizi ya VVU. Timu ya watafiti kutoka Afrika Mashariki ikiongozwa na mwanaharakati, Leila Sheikh ilifanya utafiti kuhusu biashara ya ukahaba, lengo lao likiwa ni haki za binadamu na usalama wa watu hao katika muktadha wa VVU.

  Katika utafiti huo, makahaba 109 wa Kenya walihojiwa, 89 wa Uganda na 109 Tanzania. Wengi wa waliohojiwa walisema, polisi, wateja, na sheria za nchi ndiyo sababu kubwa ya manyanyaso wanayoyapata.

  Walisema polisi wanapowakamata huwalazimisha kufanya nao ngono, kuwadai fedha au vyote kwa pamoja. Sheikh anasema, sehemu kubwa ya Afrika Mashariki inaamini kwamba makahaba hulazimishwa kufanya biashara hiyo na kundi jingine la wanaharakati wa jinsia huamini kwamba biashara ya ngono ni unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake.

  Mmoja wa wahusika waliohojiwa kutoka Dar es Salaam, aliyetajwa kwa jina mola la Valeria anasema: “Kwa mdomo huo huo wanaharakati mnasema mnatetea haki za kiuchumi na za kuishi kwa wanawake, kisha mnatumia mdomo huo huo kusema kwamba biashara ya ngono ni unyonyaji. Nani anayenyonywa? Kahaba ambaye anajipatia pesa bila kudanganya yeyote au mteja, mwanamume ambaye anapata huduma kutoka kwetu?

  Mkanganyiko huu umeleta madhara katika hili kwa sababu kuna tofauti kati ya biashara ya ukahaba na utumwa wa ngono lakini vyote hutafisriwa kama uvunjaji wa maadili na hilo husababisha ukatili wa hali ya juu dhidi ya wafanyabiashara wa ngono.
  Wataalamu wa afya wanasema unyanyapaa na ukatili kutoka kwa wateja wanaume, polisi na jamii inalifanya kundi hili la wafanyabiashara ya ngono kuwa sehemu kuu ya maambukizi ya VVU.

  Akizungumzia kiwango cha maambukizi kwa makahaba wanaojiuza Tanzania Sheikh anasema hakuna takwimu sahihi kwa sasa kwani wengi wao huishi maisha ya kujificha wakihofia kukamatwa, unyanyapaa na ukatili.

  “Utafiti wetu ulifanikiwa kugundua kuwa, kwa ujumla makahaba wanakosa elimu ya VVU, wakihofia kukamatwa, kunyanyapaliwa na kuchekwa, kwani watu huamini kuwa kujipatia kipato kwa njia ya ukahaba ni kosa la jinai,” anasema Sheikh.

  Anasema walifanya utafiti Tanzania na kuwahoji makahaba 84 kutoka Dar es Salaam, 43 Tanga na wengine Pwani na Morogoro.
  “Tuliwahoji makahaba wanaume kwa wanawake, wasagaji, mashoga, walioko baa, klabu za usiku, vyumba vya masaji na madanguro,” anasema Sheikh.

  Pia waliwahoji makahaba wahamiaji kutoka Ulaya ya Mashariki, Asia, Afrika na wanafunzi wa elimu ya juu baada ya kugundua kuwa baadhi yao hufanya biashara hiyo. Kisha waliwaendea wateja wao, wamiliki wa baa, nyumba za wageni na madanguro.

  Makahaba walikiri kupata manyanyaso makubwa hasa kutoka kwa wateja wao na kusema baadhi yao huwapiga, huwabaka, hukataa kuvaa mipira, huwaibia au hukataa kuwalipa. Wanasema wateja wao hupenda kufanya hivyo kama njia ya kuwaadhibu au kuwapa fundisho kwa kufanya biashara isiyo halali wakiamini kwamba sheria inawagusa wauzaji na si wanunuaji.

  “Ukikutana na polisi unakumbana na manyanyaso makubwa, kwani kama asipokubaka, hutaka fedha lakini hakuna uchaguzi kwani wakati mwingine hufanya yote kwa pamoja” anasema Valeria.

  Ndiyo maana Sheikh anasema: “Kwa kuwa makahaba bado wapo katika mazingira magumu ya unyanyasaji kutoka kwa wateja wao, jamii na polisi, njia bora ya kuwaokoa ni kuwawezesha kupata huduma za kisheria na kuwalinda dhidi ya wateja wakatili.”

  Mmoja wa makahaba hao aliyejitambulisha kwa jina la D anasema: “Sisi ni binadamu, tunapumua kama binadamu wengine, tuna ndoto na matumaini, tuna hisia, tuna haki ya kuheshimiwa na kuthaminiwa.”

  Sheikh anasema mafunzo ya kujikinga na VVU hayana budi kutolewa kwa makahaba na kuwepo mazingira rafiki ya huduma za afya ambayo hayatakuwa na unyanyapaa kwa wale walioathirika au magonjwa ya zinaa pamoja na mikakati bora zaidi ya mawasiliano.

  “Tuondoe unyanyapaa na ukatili dhidi yao, ili wasihofie kwenda kupata huduma za afya, ili waweze kujilinda na kuwalinda wateja wao. Lakini pia tuanze kujadili hizi sheria ambazo hukandamiza wale walioamua wenyewe kufanya biashara ya ukahaba. Sera mpya ya VVU na Ukimwi ya mwaka 2010 imezungumzia mahitaji ya kundi hili, ingawaje, hakuna mshikamano kati yake na sheria.”

  Anasema vita dhidi ya Ukimwi inahitaji ushirikishwaji wa makundi yote wakiwemo wafanyabiashara ya ngono ambao wametajwa kuwa katika hatari zaidi, hivyo kuendeleza, unyanyapaa, ukatili na ubaguzi dhidi yao yatachukua muda kufanikiwa. Lakini anasema: “Katiba yetu inasema, kila mtu ana haki ya afya na haki hiyo haitakiwi kuwatenga makahaba.”
   
Loading...