Maisha ya Watendaji wa Serikali za Mtaa baada ya Baada ya Oktoba 29, bado ni yaleyale, hakuna uwajibikaji stahiki

Maisha ya Watendaji wa Serikali za Mtaa baada ya Baada ya Oktoba 29, bado ni yaleyale, hakuna uwajibikaji stahiki

Joined
Dec 1, 2025
Posts
7
Reaction score
3
Maisha ya Watendaji wa Serikali za Mtaa baada ya Baada ya Oktoba 29, bado ni yaleyale, hakuna uwajibikaji stahiki

“Effects” au matokeo ya kilichotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 kinaonesha kuwa kimekusa utendaji wa Serikali za Mtaa kwa asilimia kubwa.

Hapa kwetu Dodoma hali imebadilika kuhusu Watendaji kadhaa wakiwemo Watendaji wa mitaa, wenyeviti wa mitaa na Mabalozi wa Nyumba Kumi, wamekuwa sio watu wa kujiachia kwa maana ya kujisifu au kujivunia nafasi walizonazo.

Hiyo ni kwa kuwa wakati wa Uchaguzi kulitokea vurugu na maandamano na baadhi ya walengwa walioshambuliwa ni Viongozi au Watendaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuwa Watendaji wengi nao inajulikana ni wa chama hicho, hivyo walikuwa katika nyakati ngumu kutokana na Waandamanaji kuwavamia wao au kulenga kuwahadhuru wao.

UTENDAJI UMEBADILIKA
Maeneo mengi ya Dodoma, baadhi ya Watendaji walionekana ni “wabaya” kwa waandamanaji kwa kuwa walionekana ni Watu wanaozingatia zaidi taratibu za kimaandishi, vikao, ripoti na maelekezo ya ngazi za juu ili wapate sifa au hela na sio kutatua matatizo ya wananchi.

Ilionekana kuwa wamekuwa katika hali hiyo ili wasionekana wapinzani inapotokea wanaenda kinyume na vile Serikali inataka au inaelekeza.

Inajulikana kuwa uwajibikaji wa kweli huanza pale ambapo watendaji wa ngazi ya chini wanawajibika moja kwa moja kwa wananchi, si kwa vyeo au miundo ya kisiasa pekee. Hilo ndilo ambalo Waandamanaji walikuwa wanalitaka, UWAJIBIKAJI.

JE, WATENDAJI WAMEBADILIKA
Maoni kadhaa ya Wananchi niliozungumza nao katika Mitaa ya Chakonichako, Majengo na Makole wanaeleza mitazamo yao kama kuna mabadiliko yoyote ya kiutendaji kwa Watendaji wa Chini baada ya kilichotokea kwenye Uchaguzi wa 2025:

“Hakuna Kilichobadilika, ni Watu Walewale” hiyo ni moja ya kauli ambayo imezungumzwa katika maeneo mbalimbali ya masoko, vituo vya daladala na vijiweni.

Zuwena Ally katika Soko la Majengo anasema: “Baada ya uchaguzi tulitegemea uwajibikaji uongezeke, lakini ni viongozi walewale, mtindo ni uleule.”

Maoni mengine ni kuwa Wanawake na wazee wanasema baadhi ya watendaji hawapatikani kirahisi, hawatoi taarifa, na bado wanachagua nani wa kumsikiliza.

Kuna dhana kuwa wananchi wengi wanaamini maandamano ya Gen Z yalifungua macho yao, lakini hayajabadilisha mwenendo wa utendaji wa viongozi wa chini.

Kimya na Majibu ya Kijumla
Viongozi wa Serikali za Mitaa walipoulizwa kuhusu hali hiyo, walitoa majibu ya jumla yasiyoakisi moja kwa moja malalamiko ya wananchi.

“Hali ni shwari, ofisi zinaendelea kufanya kazi na changamoto zinashughulikiwa,” alisema kiongozi mmoja wa serikali ya mtaa bila kufafanua hatua mahsusi.

Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kuwa baadhi ya ofisi zilizoharibiwa wakati wa maandamano bado hazijarekebishwa kikamilifu, hali inayozorotesha utoaji wa huduma na kuongeza taswira ya uzembe kwa wananchi.

Wadau wa Utawala na Haki za Kiraia:

Mfumo Bado Una Kasoro: Wadau wa masuala ya utawala na haki za kiraia wanasema kilichobadilika zaidi ni hofu, si uwajibikaji.

“Baada ya uchaguzi, tunachokiona ni watendaji wanaojilinda badala ya kuwahudumia wananchi kwa ujasiri,Mfumo bado unawaunganisha na siasa za chama, jambo linalodhoofisha uwajibikaji,” alisema Sayuni Moses mtaalamu wa haki za kiraia jijini Dodoma.

Amesema bila marekebisho ya wazi ya mifumo ya utendaji na elimu ya uraia, ngazi ya chini itaendelea kuwa dhaifu na isiyoaminika.

Uchunguzi huu unaonyesha kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, hali ya utendaji wa ngazi ya chini Jijini Dodoma haijapitia mabadiliko ya maana.

Uwajibikaji bado ni wa mashaka, hofu imetawala, na imani ya wananchi kwa viongozi wao inaendelea kuporomoka.

Badala ya kuwa chachu ya mabadiliko, uchaguzi unaonekana kuacha mfumo uleule, watu walewale, na changamoto zilezile hali inayozidi kuibua swali: je, utawala wa ngazi ya chini upo kwa ajili ya wananchi au kwa ajili ya kulinda mfumo uliopo.


Watendaji wa Mitaa na Kata:

Watendaji wa ngazi za chini Dodoma, ikiwemo wenyeviti wa mitaa na wakuu wa vijiji, baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 wamesalia na changamoto zinazofanana na zile zilizokuwepo kabla ya uchaguzi.

Mmoja wa viongozi hao kutoka Kijiji cha Idilo Mpwapwa(hakutaka jina lake litajwe)ameleza ingawa baadhi yao wanaonyesha jitihada za kuimarisha uwajibikaji kwa wananchi, hasa katika masuala ya ukusanyaji wa michango, ufuatiliaji wa miradi midogo ya maendeleo na kuendesha mikutano ya hadhara, uwajibikaji wao unakwamishwa na matamko ya juu.

Anasema Watendaji wengi wanakabiliwa na mifumo mizito ya kiutawala na kisiasa, jambo linalosababisha malalamiko ya wananchi kupuuzwa au kushughulikiwa kwa muda mrefu bila suluhu.

Amesema upendeleo katika upangaji wa maeneo ya biashara, urasimu wa vibali, na ucheleweshaji wa maamuzi yameendelea kuwa kikwazo kwa uwajibikaji wa kweli.

"Kuna wakati sisi kama viongizi tunatamani kuona Wananchi wetu wanapata maendeleo kakini u pendeleo wa baadhi yetu unafanya baadhi ya wachache kunufaika, mara nyingi viongozi wanawajibika zaidi kwa chama au mamlaka ya juu kuliko kwa wananchi waliowachagua, jambo linalodhoofisha uhusiano kati yetu na jamii, "amesisitiza.

Naye Harold Mchemwa, Mwenyekiti wa Kijiji mstaafu wa Kijiji cha Mazase wilayani Chamwino anasema baadhi ya viongozi wa ngazi ya chini hujaribu kuanzisha mabadiliko madogo, kama vile kuzingatia maoni ya wananchi na kutoa majibu kwa baadhi ya kero.

Hata hivyo anasema maboresho haya hayajaenea kwa kiwango kinachogusa maisha ya wengi, na hivyo kuacha hisia kwamba mambo ni yale yale.

"Kwa hiyo, licha ya uchaguzi kuhitimisha kipindi kipya, uwajibikaji wa watendaji wa ngazi ya chini bado unaonekana kuwa hafifu, huku mifumo mizito na ukimya wa wananchi ukibaki kikwazo cha kweli cha mabadiliko, " amesema.

Mchemwa anasema watendaji wa ngazi za chini Dodoma baada ya 2025 wanashughulikia majukumu yao kwa sehemu, lakini uwajibikaji wa kina na unaoonekana kwa vitendo bado haujafikiwa.

Hali hii inaashiria kwamba mabadiliko makubwa yanahitaji mageuzi ya mifumo ya utawala na uwazi zaidi ili kuunganisha uwajibikaji wa kisheria na wa kijamii.

“Tunaendelea na majukumu, lakini kwa tahadhari kubwa”
Watendaji wa Mitaa na Kata walisema kuwa kwa vitendo, hakuna mabadiliko makubwa yaliyotokea baada ya uchaguzi. “Kazi zinaendelea, lakini si kwa uhuru. Kila uamuzi unaangaliwa kisiasa, na hilo linatufanya tufanye kazi kwa tahadhari kubwa,” alisema Mtendaji wa Mtaa mmoja wa Mtaa wa Chinangali aliyeomba jina lake lisitajwe.

Baadhi yao wamesema wanahofia kukosolewa au kushambuliwa na wananchi, huku wakilaumiwa kwa mambo yaliyo nje ya mamlaka yao.

Wengine wanakiri kuwa bado kuna maelekezo yasiyo rasmi yanayowafanya waonekane kama mawakala wa chama tawala badala ya watumishi wa umma.

Kwa upande wa wajumbe nyumba 10 wamesema hadhi yao katika jamii imeporomoka.

“Wananchi wengi hawatuoni kama viongozi tena,hatuna thamani wanatuona kama sehemu ya mfumo uliowakwaza,” anasema Balozi mmoja wa Kata ya Nzuguni.

Anasema wanaogopa kutembelea kaya au kuitisha mikutano kwa hofu ya kukataliwa au kuzomewa, hasa na vijana wa Gen Z.

Wengine walisema wanashutumiwa kuhusishwa moja kwa moja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), hali inayozidi kudhoofisha uhalali wao katika jamii.

Sauti za wananchi.

Mmoja wa wanawake katika eneo la Majengo anasema“Ukihitaji mtendaji, anakuambia ana kikao,ukirudi kesho, yuko nje ya ofisi. Tunabaki na matatizo yetu, hatujui tumpelekee nani.”

Anasema Kwao, tatizo si vurugu za uchaguzi, bali mwendelezo wa utamaduni wa viongozi kutowajibika moja kwa moja kwa wananchi wanaowahudumia.

Kwa upande wa vijana, hasa Gen Z, sauti zao zinaonyesha kukata tamaa kuliko hasira. Kijana mmoja katika Kituo cha Daladala cha Sabasaba anasema, “Maandamano yalituamsha macho, lakini viongozi hawajabadilika, Wanajilinda wao kwanza, si wananchi. tunawaona, lakini hawatusikii.” Kauli hii inaashiria pengo kubwa kati ya matarajio ya wananchi baada ya uchaguzi na uhalisia wa utendaji wa Serikali za Mitaa, hali inayozidi kudhoofisha imani ya umma kwa mfumo wa utawala wa ngazi ya chini.
 
Kiongozi ambaye hatokani na ridhaa ya wananchi hawezi kuwajibika ipasavyo kwa hao wananchi.
 
Back
Top Bottom