Maisha ya wakulima hayana mvuto - Obasanjo

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
Rais wa zamani wa Nigeria, Olesegun Obasanjo amesema maisha ya wakulima hayana mvuto kama ilivyo ya wanasoka au watangazaji maarufu wa televisheni hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya vijana wakimbie kilimo.
Amesema kilimo barani Afrika kinakabiliwa na hali ngumu kwa sababu ya hadhi duni wanayopewa wakulima ama kutokana na maisha waliyonayo ama kutokana na mifumo iliyopo ambayo haimwezeshi mkulima kunufaika na kazi anayoifanya ikilinganishwa na kazi nyingine.
Alitoa maelezo hayo Alhamisi iliyopita katika ukumbi wa AICC jijini Accra, Ghana wakati akichangia mada kuhusu njia bora za kuinua hali ya kilimo katika Mkutano wa siku tatu wenye lengo la kuleta Mapinduzi ya Kilimo Barani Afrika unaomalizika leo.
“Nimeongea na baadhi ya vijana na kuwauliza wanataka wafanye nini wakimaliza shule… utasikia huyu anasema anataka kuwa Rais, Waziri Mkuu au Mbunge.
Hakuna anayetaka kuwa mkulima kwa sababu wanaona maisha ya wanasiasa yana mvuto mkubwa. Tuna changamoto ya kubadili maisha ya mkulima kama kweli tunataka kuinua hadhi ya kilimo,” alisema.
Obasanjo aliwachekesha wajumbe zaidi ya 600 waliokuwa ukumbini humo aliposema yeye mwenyewe ni muathirika (victim) wa taswira mbaya ya mkulima kwani akiwa uwanja wa ndege, alizuiwa kuingia nchini Canada kwa zaidi ya saa tatu kwa vile pasi yake ya kusafiria imeandikwa kazi yake ni mkulima.
“Nikiwa Rais mstaafu, nilienda kumtembelea rafiki yangu… ndege iliwahi sana. Waliniuliza wewe ni mkulima? Unakuja kufanya nini huku? Wakasema kaa hapo pembeni… nilisubiri kwa saa tatu. Alipokuja rafiki yangu kunipokea, akaniuliza mbona umekaa huku pembeni... ulijitambulishaje?
Nilimpojibu mkulima, akasema nilikosea sana, nilipaswa kusema mimi ni Meneja Kilimo na Biashara (Agricultural Business Manager) kwani hapo wangeniruhusu bila shida yoyote kwa vile nchini kwao mkulima hathaminiwi kabisa kama ilivyo Afrika,” alisema huku akishangiliwa na washiriki wa mkutano huo.
Akielezea kuhusu ugumu wa vijana kujiunga na kilimo, alisema hata mtoto wake ambaye amehitimu shahada ya teknolojia ya habari (IT) alikataa kufanya kazi katika shamba lake wakati akimhimiza wafanye wote kazi ya kilimo badala ya kwenda kuajiriwa.
Akichangia katika mjadala huo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema vijana wengi wanakimbilia mijini kwa sababu ya ugumu wa kazi ya kilimo, lakini kama wakiwezeshwa katika vikundi na kupewa zana za kisasa, lazima watapenda kilimo kwa sababu kazi itakuwa rahisi.
“Kilimo cha jembe la mkono kinachosha na ndiyo maana vijana wengi wanaikimbia kazi hiyo… tuanze sasa kubadili taswira hiyo kwa kuwapa zana za kisasa… wakijiunga kwenye makundi na kupatiwa zana za kisasa na utaalamu watabadilika… wako ambao wameanza kutambua kuwa ardhi ni mali,” alisema.
Rais wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuendeleza Kilimo (IFAD), Bw. Kanayo Nwanze alisema ni lazima watu waache tabia ya kudhani kilimo ni kupanda mbegu ardhini tu bali watambue kuwa kuna fursa za biashara kwenye kilimo na kwamba kinaweza kuwa cha manufaa kikiendeshwa kitaalamu.
Alisema ili kuinua hali ya mkulima, kuna haja ya kuendeleza vyama vya wakulima na wazalishaji wengine ili waweze kuwa na uhakika wa masoko kwa bidhaa wanazozalisha. “Hatuna budi kuwaelewesha faida za kuongeza thamani ya mazao yao na jinsi wanachama wanavyoweza kufaidika na mchakato huo,” alisema.
Mada zilizojadiliwa jana ni namna ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. Pia mawaziri kutoka Ghana, Rwanda, Tanzania, Malawi na EAC watapata fursa ya kutoa misimamo ya nchi zao na sera zao za kilimo kabla ya waandaji wa mkutano kutoa maazimio ya mkutano huu.
Mkutano huo umemalizika jana mchana na Waziri Mkuu anatarajiwa kuondoka Accra leo.



CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Ni kweli umesema Mzee Obasanjo Maisha ya Mkulima hayana Mvuto kila siku atakuwa masikini mkulima.
 
Back
Top Bottom