Maige anakumbuka shuka asubuhi kweupe!

KAMBOTA

Senior Member
Mar 21, 2011
176
103
Na Nova Kambota
novakambota@gmail.com
www.novakambota.com

Nakubaliana kwa asilimia mia moja na falsafa isemayo wenye upeo mdogo
hujadili watu, wenye upeo wa kati hujadili matukio na wale wa upeo wa
juu kabisa hujadili hoja tu. Hakika huu ni ukweli usio na chembe ya
uongo ndiyo maana leo katika makala haya badala ya kumjadili yule
waziri wa maliasili na utalii aliyepigwa chini Ezekiel Maige,
nitajadili hoja zake anazozitoa kila uchao.

Tangu ang’olewe kwenye nafasi ya uwaziri Maige amekuwa haishi
kubwabwaja ovyo kiasi cha kunitia majaribuni kuanza kumfananisha na
kilio cha mlevi aliyemwagiwa gongo yake, kwa jinsi anavyopiga mayowe
ya “nikumbuke kikwete” sasa hata wachache waliokuwa wanamwona ameonewa
wameshajiridhisha kuwa hakuonewa hata kidogo badala yake alistahili
“kufilisiwa kabisa” na kufukuzwa uanachama wa CCM.

Mimi si mshauri wa Chama Cha Mapinduzi lakini sitasita kukishauri
chama hiko kumwajibisha mtu anayetoa kauli zinazoleta picha kuwa
uwaziri nchi hii ni “ulaji” ndiyo maana mtu aking’olewa haachi kulia
machozi ya mamba aliyekosa kitoweo. Mbunge huyo wa jimbo la Msalala
huko Kahama ametabiri kuwa jimbo hilo litachukuliwa na CHADEMA mwaka
2015.

Ingekuwa busara endapo Maige angetwambia kama hayati Shehe Yahaya
Hussen alimwachia mikoba ya utabiri ama la? Kwa maana haiingii akilini
kwa Maige kuendelea kubaki ndani ya CCM anayoamini itakufa, au anataka
tuamini uwezo wake wa kufikiri unamtuma kupanda basi analojua litapata
ajali na yeye kufariki? Kama Maige amefikia hapa hafai kuwa hata
“mpiga debe” wa daladala za kariakoo sembuse ubunge!

Kwanza na hakika CHADEMA haihitaji mtabiri Maige kuitabiria itazoa
majimbo mengi 2015, hili liko wazi CCM watake au wasitake kwa maana
wananchi wameshachoshwa na wanasiasa “mufilisi” wa aina ya Maige na
chama chao. Hata Maige angeimba mashairi mazuri kama Shaaaban Robert
bado si Kikwete wala CCM yake wanaweza kumsikia kwa maana anachodhani
kuwa CCM ingali hai ni mawazo yaliyopitwa na wakati , kilichobaki ni
mazishi tu ya CCM.

CCM haitakufa kwasababu Maige katabiri, bali imekufa kwasababu ya
kupuuza walalahoi, kupeana vyeo kindugu, kuminya uhuru wa wananchi,
kujenga shule za kata kuzalisha sifuri, ufisadi uliokubuhu,kulinda
muungano kinguvu, kuuza madini yetu na kufukarisha wananchi. Haya
ndiyo yameiua CCM sasa iweje Maige na wenzake wajifanye kushtuka sasa
hivi? Hakika hili ni jaribio dhaifu la kukumbuka shuka asubuhi kweupe!

Tunataka viongozi waseme ukweli hata kama unawagharimu kiasi gani,
lakini ukweli unaosemwa kwa tamaa ya cheo au hasira za kunyimwa mkate
ni unafiki mkubwa! Watu bado wanajiuliza kilichomsukuma Maige
kujitumbukiza kwenye tasnia ya unajimu dhidi ya chama kinachompa
“ulaji” ni kukosa cheo au udhaifu wa CCM?

Kama tatizo ni kukosa uwaziri mbona wengi wameng’olewa lakini
hawajataka kututapisha kwa maneno ya unafiki kutoka vinywani mwao?
Kama anavyofanya Maige? Au Maige ameandikwa kwenye paji la uso kuwa
sharti awe waziri? Au anayoyasema sasa kayajua baada ya kung’olewa
uwaziri? Na iwapo CCM inashindwa kumwajibisha mtu wa namna hii basi
haistahili kuwa hata chama cha upinzani kwenye nchi yetu! Haitakuwa
matusi kama nikisema namfanisha Maige na nyoka aliyepigwa mkiani kisha
anaendelea kujitikisatikisa sasa busara zinanituma ukitaka kuua nyoka
umponde kichwa CCM wanangoja Nyerere afufuke kumshughulikia Maige!


Naomba nimkumbushe Maige juu ya wingu la kashfa zinazomwandama za
kujenga mjumba wa mabilioni ya shilingi? ambazo pasi na shaka
zitamwandama milele, watanzania bado wana kiu ya kumsikia akijibu
tuhuma hizi napengine kuomba msamaha jinsi alivyoacha maliasili zetu
kuporwa na wageni kwa ahadi za “ten percent”.

Watu wa aina ya Maige wanapaswa wafunge midomo sasa hususani kipindi
hiki ambacho watanzania wameamua kuchukua hatua za kujikomboa wenyewe
kupitia kile kinachoitwa “M4C” chini ya mwavuli wa CHADEMA. Maige
anapojigeuza mtabiri kwasasa hana tofauti na mtu anayenunua sanda
nzuri kwaajili ya marehemu ilihali hakumsaidia chochote akiwa mgonjwa.

Alipopewa nafasi ya uwaziri alipaswa kuwaonyesha walalahoi kuwa Rais
Kikwete hakukosea kumteua badala yake akajiingiza kwenye ulaji
mwishowe kamshika “kipofu” mkono . Au alidhani uwaziri ni kuvaa suti?
Au mikogo na tambo za “ubwana mkubwa”? Watanzania watakuwa watu wa
ajabu kuendelea kuchakaza viwambo vya masikio yao kusikiliza kilio cha
“mamba aliyepigwa mkuki”.

Iwapo CCM inadai wanaotoka ndani ya chama hiko ni “oil chafu” kwa
mantiki hiyo wanaobaki ni oil safi halafu wakaacha watu wa aina ya
Maige kuendelea kujitafutia “cheap popularity” kwa staili ya
kuitabiria kifo CCM basi niseme wazi kuwa na shaka sana nahii “oil
safi” ya aina ya Maige! Hofu yangu huko tuendako gari itazima kabisa .

Nani leo hii hafahamu jinsi makampuni ya kigeni yanavyomaliza
wanyamapori wetu? Nani hajui misitu inavyoteketea kwa kasi ya kimondo?
Mtu alipewa dhamana ya kusimamia haya, kashindwa kafukuzwa kazi halafu
anataka tumsikilize ati leo amekuwa na busara ala! Busara kazichota
wapi? kwanini Maige ajigeuze kocha wakati alipokuwa mchezaji kwenye
mechi hiyohiyo kaachia magoli lukuki?

Maige anadai CCM kuna fitina! Na fitina zitaua chama, hivi sasa viroja
yaani leo hii Maige ndiyo kaliona hili ? Kwanini hakuwasikiliza kina
Dk Salim na Sumaye 2005? Au alikuwa kaahidiwa uwaziri? Hivyo akakaa
kimya wakati wenzake wanafitiniwa, akakenua meno kwa furaha. Sasa
msumeno umeanza kurarua na upande B ndiyo anastuka. Hivi Maige hajui
kwamba msumeno hukata kila upande? Kama aliyajua haya kwanini
alalamike muda huu?

Mimi nadhani watanzania tuseme imetosha sasa kwa hawa kina Maige ambao
hawaishi kutukera kwa maneno ya kinafiki na kizandiki. Mara utasikia
CCM ndiyo chama dume , mara hakuna kama CCM lakini pale vitumbua vyao
vinapoingia mchanga utasikia kila aina ya laana dhidi ya CCM hiyohiyo
wanalaani mpaka mapovu yanawatoka. Tuwaambie pasi na shaka kuwa muda
wa kuwasikiliza umeisha miaka hamsini ya kuwasikiliza imeyeyuka, sasa
ni zamu yetu wananchi kutenda wao ni watu wa kungoja matokeo mara
ifikapo oktoba 2015.

Maandishi tayari yameshaandikwa ukutani , si kwa majeshi au propaganda
ni lazima maandiko yatimie. Sasa Maige yaelekea anataka kuanza
propaganda za “kitoto” za kutaka kuwahadaa wana wan chi hii kwa maana
nyingine anataka kuzuia unabii usitimie ala haula! Maige kakosea sana
! yaani anadhani uanbii unaweza kuzuiwa usitimie. Najiapiza hili katu
hawezi.

Badala ya kuendelea kuvumilia uasi ndani ya chama busara iwaongoze
Mukama, Nape na timu yao kuondoa “utando wa buibui” chumbani mwao ili
kivutie wageni vinginevyo sioni kwanini CCM iendelee kulipa posho
watendaji wabovu wanaochekelea chama kuvuliwa nguo hadharani na mtu
anayedhani ana hakimiliki ya uwaziri.



Mimi ni shabiki wa watoto wakweli lakini sitamuunga mkono hata kidogo
mtoto anayekiri ukweli mbele ya wageni kuwa baba yake amejamba au
chupi ya baba yake imetoboka. Lolote liwalo hii ndiyo aina ya ukweli
unaotoka kinywani mwa Ezekiel Maige kwa staili ya “Kikwete mwaga
mboga” mimi namwaga ugali. Sasa ingekuwa busara CCM ikang’ata kuliko
kuendelea kuitwa “jibwa koko” au mbwa kibogoyo asiyeweza kung’ata !
CCM ina mawili kukubali kuubusu mkono ulioasi kwasababu ya hofu ya
kuukata au imwachilie Maige aende kwa maana anachekesha walimwengu kwa
kutaka kusuma gari akiwa ndani.


Nova Kambota ni mwandishi na mchambuzi wa maswala ya kisiasa,
anapatikana kwa anwani ya barua pepe novakambota@gmail.com , au waweza
kutembelea tovuti yake www.novakambota.com
 
Maige ana haki ya kutoa maoni yake! Leo hii mnaona amekosea kutoa utabiri mzuri na waukweli?

Mbona cdm ilivyo mkemea shibuda mlimtetea kuwa ana haki?

Minaona maige yuko right kabisa uwaziri wa ccm ni ulaji tu.
Na ni ukweli usiopingika 2015 cdm lazima tuibuke kidedea.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom