Mahojiano kati mwandishi na Paul Kagame | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mahojiano kati mwandishi na Paul Kagame

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Joss, Sep 2, 2010.

 1. Joss

  Joss JF-Expert Member

  #1
  Sep 2, 2010
  Joined: May 28, 2009
  Messages: 729
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 33
  source:raiamwema
  Kagame: Wa nje hawataki kuamini maendeleo ya Rwanda


  Mwandishi Wetu
  Septemba 1, 2010

  Rais Paul Kagame wa Rwanda hivi karibuni alipata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo unaofanyika kila baada ya miaka saba. Yafuatayo ni mahojiano ambayo Jenerali Ulimwengu wa gazeti hili alimfanyia Rais huyo mjini Kigali, Rwanda.

  Swali: Mheshimiwa Rais, Unapimaje mafanikio ya Serikali yako na malalamiko dhidi yake na kwa chama cha RPF?

  Jibu: Hali ya Rwanda imekuwa kidogo si rahisi kuelezeka. Kusema kweli tumekuwa tukishughulikia hali ambazo ni ngumu, nyingine ambazo zimetupatia hata mafunzo kwetu. Siku zote tunajifunza tunavyosonga mbele. Katika kushughulikia baadhi ya matatizo yetu unakuta kwamba hakuna kigezo cha kurejea, hakuna kitabu cha kiada ambacho unaweza kukitumia kwa urahisi na kusema kwamba sehemu nyingine mambo yalikuwa hivi na yalishughulikiwa hivi…

  Wakati mwingine tunalazimika kufanya vitu hata kwa njia ya majaribio, ni uzoefu wa kujifunza… lakini utakuta kwamba tumekuwa tukishughulikia hali, kujaribu kushughulikia matatizo yetu, yanayoanzia kwenye historia yetu, utamaduni wetu na hata tamaduni ambazo siku zote zinaingiliana na mambo mengine.

  Kuna pia mambo mengine ya nje ya eneo ya kiafrika na mbali zaidi ambayo yanakuja ndani (na kufanya mambo yaparaganyike zaidi). Kuna mambo mengi ya kuchambua, kukitafuta kitu hiki kidogo, kama vile unatafuta kipunje cha ngano kwenye nyasi ndefu...

  Nina maana gani kwa kusema hivi? Uhalisi wa watu, mnajua hili siku zote litakuwa linawapita pembeni kwa wengi wenu kutoliandika mnapokuja kuandika (kuhusu Rwanda) kwa sababu mbalimbali. Sababu kubwa moja ambalo nimeliona mara nyingi ni kama kuna masimulizi mbalimbali unayoweza kuyapata lakini kuna simulizi moja linayojitokeza zaidi na hili linasababishwa zaidi na sababu za nje kuliko za ndani… waandishi wa habari hawa, waangalizi hawa, huwa hawaoni kwa sababu fulani fulani sielewi, na kama wakiona hawataki kuamini.

  Wanaona kwamba labda kuna kitu kinachotokea hapa Rwanda na kwamba angalau kwa Wanyarwanda ina maana kubwa, bado kama Rwanda inafanyiwa tathmini, hili halijitokezi. Wataandika kwamba nchini Rwanda Wahutu, Watutsi, watadumisha yale masimulizi ya mgawanyiko kama ilivyokuwa zamani, ndicho kipimo. Lakini pamoja na hayo unapouona umma, watu walivyo, huwezi kuuona Ututsi peke yake au Uhutu ambao wamelazimishwa kuja hapo.

  Ni Wanyarwanda waliokuja kwa sababu wanajifananisha na kitu fulani. Lakini hilo halijitokezi hata kwa watu wanaoliona hilo mara nyingi. Ni kama vile Kagame, chama cha RPF ndivyo vinavyojifanya Rwanda, Rwanda ambayo katika mioyo yao imegawanyika kati ya Wahutu na Watustsi, basi...

  Huwa hata wanaongea kuhusu RPF au Kagame kuwapo juu bila kuwahusisha watu. Masimulizi hayo ndiyo yanayotoka na ndiyo yanayoimbwa kila siku bila kujali kuwapo kwa ushahidi wowote unaoweza kuipatia dunia na kusema hapa, hiyo siyo kweli…

  Inaunganishwa na madai ya mara kwa mara ya kushutumu kwamba hakuna nafasi ya watu kufanya siasa, Kagame kuwa mbabe au hata mkandamizaji, chama cha RPF….

  Ni kama hapa Rwanda watu hawana sauti ya aina yoyote, wanashurutishwa kufanya mambo ambayo hayako kwenye matakwa yao. Kwamba moyoni wana mambo yao lakini sisi tunawasukuma tu kufanya wasiyoyataka bila ya ridhaa yao wakikubali kwamba kuna kitu kinachofanyika. Kusema kweli ni kama pia kwamba kwa maendeleo ambayo yanasifiwa, wengi wameweza kusifia kwa sababu ya kulazimishwa tu.

  Siku zote kutakuwa na hali kama hii, kwamba, ndiyo kuna maendeleo, lakini kwa gharama ya nani? Kilicholengwa kuonyesha ni kama, maendeleo ndiyo… na kwamba wanasema pia ndiyo hata kama unaichukia Rwanda na ni kipofu huwezi kushindwa kuona endapo kuna maendeleo au hapana (kicheko)… Kwa hiyo mjadala unaendelea, ndiyo kuna maendeleo lakini kwa gharama gani?

  Swali: Je, inawezekana kwamba uhusiano mbaya na umma ndiyo unaofanya watu wasikubali maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya Rwanda? Baadhi ya watu wanakana mafanikio hayo wakisema yamesaidiwa na udogo wa nchi na udikteta wa Kagame.

  Jibu: Ngoja nikubali kuhusu uhusiano na umma, Kwangu mimi siyo kitu cha hivi karibuni. Uhusiano wetu wa umma unaweza kuwa mbaya na hiyo haisaidii kufanya vitu kuwa sawa katika suala letu, lakini bado nadhani ni tatizo dogo.

  Tatizo kubwa zaidi ni… hata katika eneo letu wakati mtu anaposema kwamba wanafanya wanachofanya kwa sababu ya udogo wa nchi… ndiyo, kuwa na nchi ndogo hiyo ni sababu, sina ugomvi na hilo. Lakini majibu kama hayo yanahusishwa na maendeleo, kitu ambacho kinaleta matatizo yake yenyewe. Mafanikio tuliyoyapata yameleta pia matatizo yake.

  Si kila mtu ni mkweli wa kutosha kukubali.. ni katika hali ya kibinadamu si watu wote watapongeza panapostahili kwa sababu moja au nyingine. Kusema kweli si jambo la kawaida kwamba kuna ushahidi mmoja mdogo kwamba hata katika mikutano ambayo imefanyika katika miaka kumi au zaidi ambayo watu kutoka sehemu mbali mbali duniani wamekuwa wakizungumzia kuhusu mambo yaliyofanyika Rwanda katika maendeleo.

  Nimewaambia watu wangu: Kitu cha kwanza mnaposikia mambo hayo ya kusifiwa msilewe kwa sababu kuna hatari ya kuangukia kwenye ugonjwa wa kuridhika mno kutokana na ulevi huo kwa sababu watu wanasema mumepiga hatua kubwa ya maendeleo hivyo mnaacha kufanya mambo ya maendeleo au hata mnaanza kurudi chini kimaendeleo.

  Jambo la pili, pia nilisema mujitayarishe kuwapo kwa vijembe vya namna yake, vijembe vya kweli au visivyokuwa vya kweli na vingi visivyokuwa vya kweli kwa sababu watu watasema, kwa nini Rwanda?

  Kwa mfano kuna mwandishi mmoja wa Uganda ambaye aliletwa hapa na rafiki yake mmoja. Mwandishi huyu alipokuwa Uganda alikuwa akiandika (mambo chanya) kuhusu Rwanda hivyo aliletwa na huyo rafiki yake hapa Rwanda. Na uliweza kumwona kwamba si kwamba aliyekuwa hana macho ya kuona, kwa sababu ilifika mahali alikuwa anakubali kwamba ndiyo kuna maendeleo na baadaye anakubali zaidi kwamba kuna maendeleo makubwa zaidi. Lakini ghafla anarudi kwao na kusema hapana, yote ni ujinga. Ni kwa sababu (maendeleo yaliyofikiwa) ya kitu kingine.

  Lakini nilikuwa nataka kusema kwamba katika mikutano ambayo imefanyika kwa miaka mingi, inatokea mtu kwenye Umoja wa Mataifa anaposema jambo kuhusu Rwanda na anajitokeza kusema nchini Rwanda tumeliona hilo, au lile kuhusu ukimwi na katika elimu au katika usalama na kusema wanafurahi kuwa marafiki na Rwanda. Tunapowekeza pesa zetu tunaona matunda yake kwa matokeo na mambo mengine.

  Wengine wanakuwa na roho ya chuki kuhusu mpango mzima wa kuizungumzia Rwanda na wanashindwa kusema ukweli kwamba Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Wote (UPE) umefanikiwa kwa asilimia 92 na ni ukweli kwamba kuna ushahidi na watu wanasifia inapotokea Rwanda au kwingineko kokote watu lazima wasifie. Lakini unapolisifu hilo kwa Rwanda, kuna hali ya kutokubalika.

  Sasa jambo la tatu: Dunia tunayoishi haitabiriki. Tumekuwa na vita vinavyoendelea karibu kila siku na hawa wanaoitwa marafiki zetu. Wakati mwingine tunafanya vitu hata kama wanakubaliana na yale tunayoyafanya watasema kwa nini hamkutuambia? Tunasikia mnafanya hili kwanini hamkutuambia? Na sisi tunasema lakini tunawaambia.

  Na inaonekana kama kuna urafiki wa kweli, wa zamani na unaoeleweka kama ni wa Wanyarwanda, wa Waafrika na pengine wa utu mdogo na hatuwezi kujua tunachokitaka au tunachostahili au tunachopaswa kukipata hivyo mtu atueleze.

  Ni hadithi ya muda mrefu, iwe ya kutoka utumwani kwenda kwenye ukoloni au ile ya baada ya uhuru. Ni kama tunahitaji ruhusa. Nitakupa mfano: Miaka mwili au mitatu nyuma tulifanya uamuzi kuhusu nini cha kufanya kuleta mageuzi ya kilimo chetu.

  Tulikuwa na mambo kama mpango wa kukazania aina fulani ya mazao ili kupiga vita njaa na kupanua masoko. Mpango ambao ungetuwezesha kukazania aina fulani ya mazao yanayostawi vyema katika maeneo fulani na mpango huu wa ng’ombe mmoja kama umewahi kuusikia na mtoto mmoja wa kiume.

  Siyo kwamba mpango huo ulikuwa mpya kabisa, kusema kweli nchi nyingi zimefanya mambo kama hayo. Hiyo sisi tukaanza kufanya kwa mikoa, tukaigawa nchi yetu kwa mfano wapi ambako chai inastawi vizuri? Wapi ambako mahindi yatastawi vizuri? Hatukuwa tumezoea kulima mahindi nchini Rwanda na tuliposema tutafanya hivyo na kupanga sera yetu, tukapigwa vijembe na wahisani.

  Kitu cha kwanza walichokipinga ilikuwa ni mpango wa kuwa na ng’ombe mmoja. Vijembe vilitoka kwenye Benki ya Dunia na vilitoka pia Umoja wa Mataifa: “Hivyo sivyo. Sasa wanawashurutisha watu, wanataka kubadilisha maisha ya watu…”

  Wakati mmoja nilipambana na ofisa wa Benki ya Dunia na kumwuliza ni kwa nini mnapinga mpango wetu wa kukazania aina fulani ya mazao. Walijaribu kuleta hoja zao za kupinga lakini mwishowe wakasema hawa watu (mataifa makubwa ya Ulaya) wanatuhemea sana sisi, wanatuambia tuwaambie kwamba muache mpango huu. Wanasema mnawalazimisha watu kulima mahindi, mnawafanya wakate migomba yao. Wamekuwa wakiandika barua kulalamikia huu mpango wenu.

  Kuna wakati nilikasirika na kuwaambia mlikuwa hapa kwa miaka mingi na watu wetu bado ni masikini. Hivi mlifanya kitu gani kuwasaidia watu wetu kuhusu kilimo kiasi cha sasa kuwa na ubavu wa kuwaambia watu wetu nini cha kufanya na nini cha kutokufanya?
   
Loading...