Mahabusu Songea wagoma, wavua nguo

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
Mahabusu zaidi ya 20 wa kesi za mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha mkoani Ruvuma, wamegoma kuingia kwenye gari la polisi wakidai kesi zao zimekuwa zikichukua muda mrefu na kuahirishwa mara kwa mara bila sababu za msingi kukiwa na dalili za kuombwa na kudaiwa rushwa.
Mahabusu hao waliamua kuvua nguo nje ya jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma walidai kuwa kwa muda mrefu kesi zao zimekuwa zikipigwa danadana huku wakibambikwa kesi nyingine tofauti na zile zinazowakabili.
Mahabusu hao ambao walielekeza shutuma zao kwa mmoja wa maofisa waandamizi wa jeshi la polisi mkoani Ruvuma (jina tunalihifadhi), kuwa ndiye chanzo cha kesi zao kucheleweshwa, wakidai kuwa amekuwa akitaka wampe fedha wakati ni watoto wa wakulima ambao hawana uwezo wa kifedha.
Wamemuomba Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Michael Kamuhanda, afike kusikiliza kilio chao, lakini haikuwezekana badala yake alikwenda Mkuu wa kituo cha polisi, Peter Kubezya, na kujaribu kuzungumza nao kwa zaidi ya saa moja.
Baada ya mazungumzo hayo, mahabusu hao walimtaka Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dk. Christine Ishengoma, aende asikilize kilio, lakini Kubezya aliwasihi mahabusu hao kuingia kwenye gari kwa kuwaambia matatizo yao yatakwenda kusikilizwa wakiwa mahabusu nao walikubali kwa sharti kuwa hawatashuka kwenye gari kuingia mahabusu mpaka viongozi hao wafike ili wasilikilizwe kero zao.
Mahabusu hao baadaye walikubali kisha kupanda kwenye gari la polisi ambalo liliwapeleka kwenye gereza la mahabusu na kuendelea kugoma kushuka kwenye gari hilo wakiwataka Kamuhanda na Dk. Ishengoma waende kuwasikiliza. Baada ya juhudi hizo kushindikana, walishuka huku wakiimba nyimbo za kumtukana ofisa mwandamizi wa polisi wanayedai anawaomba rushwa kwamba ni fisadi.
Akizungumzia sakata hilo, Kamanda Kamuhanda alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa watuhumiwa hao ni wa kesi za mauaji na unyanganyi wa kutumia silaha ambazo ni zote ni za mwaka huu tofauti na wanavyodai wao.
Amesema baadhi yao walihusika na uporaji wa silaha mbili aina ya SMG na risasi 60 za Jeshi la polisi mjini Songea tukio ambalo lilihusisha kuwajeruhi vibaya askari polisi wawili.
Alisema wengine walihusika na mauaji ya kinyama ya mama na mwanaye yaliyotokea katika mtaa wa Lizaboni siku chache baada ya tukio la kuporwa kwa bunduki mbili na mauaji ya mfanyabiashara mmoja katika mtaa wa Bombambili mjini Songea pamoja na na mauaji ya dereva teksi wa mjini hapa.
Hata hivyo, alisema Jeshi la polisi kwa kushirikiana na mwanasheria wa serikali wanafanya jitihada kuhakikisha upelelezi wa kesi hizo unakamilika na wanatendewa haki.
CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom