Magufuli noma kwa muda mfupi tu,mafanikio ya ukusanyaji mapato na ubanaji matumizi yameonekana

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
MARA tu baada ya kuingia Ikulu, Rais John Magufuli alitembelea Wizara ya Fedha na Mipango ili kujionea shughuli zinazofanywa na wizara hiyo nyeti katika uchumi wa nchi yetu na huku pia akiwa na neno moyoni.

Wizara ya Fedha ndiyo ambayo inasimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA) na kuyapangia bajeti inayotokana na kilichokusanywa pamoja na misaada au mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo. Ni kwa kutambua hili, na kwa kuzingatia ahadi zake wakati wa kampeni ambazo ili zifanikiwe zinahitaji fedha, ndio maana Rais akiwa na saa chache toka aingie Ikulu akalazimika kuzuru katika wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na viongozi wakuu wa wizara, kipindi hicho akiwa ni katibu mkuu wa wizara na watendaji wenzake.

Alitoa maagizo ya namna ya kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima, akasisitiza pia waongeze ukusanyaji wa mapato ya serikali ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku kuwalipa posho wabunge nje ya malipo wanayolipwa na Bunge. Ziara hiyo ya ghafla ilimwezesha Rais kutoa maagizo kwa watendaji wa Wizara ya Fedha kuhakikisha kuwa wanavunja haraka mtandao wa wakwepa kodi, na kwamba wizara itoe maelekezo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili ikusanye kodi halali za serikali kwa mujibu wa sheria.

Kwa nia ya kudhibiti mianya ya wakwepa kodi, Rais Magufuli alisisitiza kuwa katika serikali anayoiongoza, hakuna mkubwa yeyote atakayeruhusiwa kutoa ‘kimemo’ kwa TRA kwa lengo la kusamehe ulipaji kodi halali za serikali. Hatua hii ilidhihirisha namna Rais Magufuli, siyo tu anavyokerwa na uzembe unaoweza kujitokeza katika ukusanyaji kodi halali za serikali bali pia kuhakikisha kwamba serikali anayoiongoza haitakuwa na mchezo katika suala zima la ukusanyaji mapato na udhibiti wake kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Katika kuhakikisha kwamba alichokuwa anazungumza hatanii, siku chache baadaye, Serikali ya Rais Magufuli ikabaini upotevu wa makontena 329 ambayo yalitoroshwa kwenye bandari za nchi kavu (ICD) bila kulipiwa ushuru na kuikosesha Serikali zaidi ya Sh bilioni 80. Kilichotokea hapo ni Rais kumsimamisha Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade na makamishna wengine wa TRA wakasimamishwa kazi sambamba na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kutumia madaraka vibaya.

Rais Magufuli hakukomea hapo, aliendelea kuwabana wakwepa kodi na baadaye akakutana na Jumuiya ya Wafanyabiashara ambako aliwataka walipe kodi stahiki za Serikali. Akatoa siku saba kwa waliokwepa kodi kupitia utoroshaji wa makontena wawe wamelipa kodi hiyo.

Sehemu kubwa ya kiasi hicho kilichokuwa kimeshapotea kilipatikana. Kutokana na juhudi hizo baadaye Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA Alphayo Kidata, alisema malengo ya ukusanyaji kodi yaliyofikiwa na mamlaka hiyo ikiwa ni baada ya kazi nzuri ya Rais kuwabana walipa kodi ambapo kwa mwezi Desemba ilivuka lengo la ukusanyaji mapato kutokana na kukusanya Sh trilioni1.4.

Ongezeko la makusanyo hayo kwa mujibu wa Kidata ilikuwa ni wastani wa Sh bilioni 490 kwa mwezi ikilinganisha na wastani wa makusanyo kwa mwezi Julai hadi Novemba ambayo yalikuwa ni kati ya Sh bilioni 850 na 900. Makusanyo hayo yamekuwa yakiongezeka kuelekea kwenye Sh trilioni 1.5 kwa mwezi na hakuna ubishi kwamba mafanikio hayo yametokana na mikakati mizuri ambayo Rais wa Awamu ya Tano tangu aingie madarakani ameiweka, ikiwemo kuteketeza mianya ya upotevu wa mapato.

Akizungumzia hali ya uchumi na mapato ya nchi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Dk Servacius Likwelile, anasema Serikali imeweza kutumia fedha za ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo bila ya kutegemea fedha za wahisani kutokana na makusanyo ya mwezi Januari mwaka huu. Dk Likwelile anasema Rais Magufuli alisisitiza suala la kuongeza makusanyo ya mapato ya kodi, kwa kuwataka wale wote wanaostahili kulipa kodi walipe, ili fedha hizo zifanye kazi ya maendeleo ya taifa.

Anasema kwa msisitizo huo, makusanyo ya mapato ni mazuri na kwamba mwelekeo ya makusanyo ya Januari mwaka huu hadi sasa ni zaidi ya Sh trilioni moja na kwamba mategemeo ni kufikia Sh trilioni 1.5 na ana uhakika lengo hilo litafikiwa na kuvuka. Katibu Mkuu huyo anasema kutokana na mfumo mzuri uliowekwa hivi sasa wa kubana matumizi yasiyo na tija na kuweka vipaumbele kwenye mambo muhimu, serikali imeweza kutumia fedha za ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na hivyo utegemezi wa wahisani kuwa mdogo.

Anasema kwa mwezi Januari mwaka huu serikali imetenga Jumla ya Sh bilioni 318.406, fedha za ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi yote ya maendeleo ambayo imepewa vipaumbele. Miradi hiyo ya vipaumbele ni pamoja na elimu, afya, maji, barabara, umeme na kulipa madeni na pensheni za wastaafu. “Suala la kujivunia ni kwamba tunaweza kutoa fedha za ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi yetu ya maendeleo, fedha za wahisani za nje ni kidogo sana.

Mfano kwa mwezi huu Januari, fedha za nje ni Sh bilioni 71.2, wakati fedha za ndani ni bilioni 318.406”, anasema Dk Likwelile. Faida ya ukusanyaji kodi makini na ubanaji matumizi imejitokeza katika maeneo mengi ikiwa ni pamoja na serikali kulipa makandarasi wa ujenzi wa barabara huku ikiahidi kwamba kufikia Juni wote watakuwa wamelipwa na kufufua miradi iliyosimama.

Katika muktadha huo, wiki hii kwa mara ya kwanza Mahakama ya Tanzania ilipokea asilimia 100 ya bajeti ya maendeleo kwa ajili ya kuhakikisha wanafanikisha huduma za utoaji wa haki kwa wananchi. Hii ilikuwa ni baada ya Serikali kutekeleza ahadi ya Rais John Magufuli kwa kuipa Mahakama Sh bilioni 12.3 aliyoahidi Siku ya Sheria, Februari 4, mwaka huu ili kutekeleza miradi yao ya maendeleo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango anasema idadi ya watu wanaolipa kodi kwa sasa hapa nchini bado ndogo, kwa maana ya kwamba wanaopaswa kulipa kodi ni wengi kuliko wanaolipa, hivyo amewaagiza wafanyabiashara wote kujisajili wapatiwe namba ya mlipa kodi (TIN). Pia amewataka waache tabia ya kufanya udanganyifu kwa kuwa na vitabu vingi vya utunzaji wa kumbukumbu za biashara.

Sambamba na hilo amewaagiza wafanyabiashara wote nchini kuhakikisha wanatoa stakabadhi na suala hilo lisiwe hiyari. Amewataka wote watumie mashine za EFDs na serikali inaendelea na mpango wa kununua nyingine ili wagawiwe bure. Anawataka wafanyabiashara kutoa taarifa kwa Kamishna Mkuu wa TRA kama kuna mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) au wa halmashauri ya wilaya ambaye atadai hongo au atawanyanyasa wakati wa kudai kodi.

Katika kutekeleza hilo, waziri huyo amewapatia namba zake pamoja na za kamishna na kuwataka waache tabia ya kutoa rushwa ili wasilipe kodi. Dk Mpango pia anawataka wafanyabiashara waache kufanya biashara za magendo ambazo zimeshamiri katika pwani ya bahari ya Hindi na kwenye Ziwa Victoria, badala yake wafanye biashara halali. “Tumewadhamiria na tutapambana na magendo hayo. Tunajua kuna watumishi kama polisi wanashiriki kusindikiza magendo hayo, ila nasema hatutamwogopa mtu,” anasisitiza Waziri Mpango.

Anasema hatua zinazofanywa na Serikali ya Rais Magufuli ya kukusanya kodi haina malengo ya kumwonea mtu bali inalenga kuifanya nchi iweze kujitegemea na kupunguza utegemezi. Anasema yeye kama Waziri wa Fedha asingependa kuwa ombaomba kwa wahisani kutokana na kuwa na masharti magumu ambayo mengine yanadhalilisha maadili ya Mtanzania kwani wahisani wanaweza kutaka nchi iruhusu ndoa za mashoga kama inataka misaada.

Dk Mpango anasema kama alivyowahi kusema mwasisi wa Taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere, kwamba Serikali yoyote ambayo haikusanyi kodi lazima itajaa rushwa. Anaongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haitamvumilia mfanyabiashara au mtu yeyote ambaye atakwepa kodi. Anasema Watanzania wengi ni masikini na hivyo lazima kodi ikusanywe ili wakombolewe kutoka kwenye lindi la umasikini.
 
Kwa Mimi mwananchi wa kawaida bado sioni afadhali yoyote labda bado mnasema ule usemi wenu, tumpe muda hata mpaka 2019 huko mwishoni
 
Bora uongozi wa kwenye magazeti (UNAOJITANGAZA) kuliko wanaofanyia kazi habari za magazetini
Kumbe wanajitangaza!!! nilikua sijui kwa kweli!! ethiopia wanatumia treni za umeme sisi viongozi wetu wanajitangaza magazetini daaah
 
Nachukia sana watu wanaojipendekeza kama wewe mleta mada,
Ubanaji gani wa matumizi unaouzungumzia? vipi wameacha kutumia ma v8?
 
Tusibaki tunasifu ukusanyaji was mapato waka elimu yetu IPO I.C.U.hari ya maisha kwa mtanzania mbaya .acha akusanye wanjanja we ataijia hukohuko
 
yakowapi matokeo ya hayo makusanyo mazuri ?
au ndio kuzipa idara hela za kulipia tu umeme ?
agh pengine ndio maana wengine wake zao wanasura za kusononeka kwa kuwabania kila kitu,kuwabania hata furaha.
 
Back
Top Bottom