Magamba yawatega Msekwa, Malecela

nngu007

JF-Expert Member
Joined
Aug 2, 2010
Messages
15,871
Points
1,225

nngu007

JF-Expert Member
Joined Aug 2, 2010
15,871 1,225
Na Waandishi Wetu (Raia Mwema)
Dodoma
24 Aug 2011
Toleo na 200
KUGUSWA kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Pius Msekwa, katika kashfa alizoziita za uongo zilizoelekezwa kwake na Mbunge wa Ngorongoro, Saning'o ole Telele, sasa kunahusishwa na majukumu yake ya kuongoza mchakato wa kuwahoji vigogo wa chama hicho, wanaopaswa kujivua nyadhifa walizonazo ndani ya chama hicho kikongwe nchini, Raia Mwema, imeelezwa.

Msekwa mwenyewe alisema tuhuma dhidi yake ni za uongo na zinakiuka kiapo cha wana-CCM kisemacho "nitasema kweli daima fitina kwangu mwiko."

Mbali na Msekwa, kigogo mwingine aliyeshambuliwa katika mkakati huo ni waziri mkuu wa zamani, John Malecela. Malecela ambaye ni mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu, naye anatajwa kuwa na msimamo mkali kwamba watuhumiwa wa ufisadi ndani ya CCM wafukuzwe haraka.


Malecela alitajwa wiki iliyopita bungeni kuwa anamiliki eneo kubwa la ardhi mkoani Morogoro lakini ikabainika baadaye kuwa eneo hilo aligawiwa kwa utashi wa viongozi fulani serikalini bila yeye kuwahi kulitembelea wala kuwa na umiliki wake na kwamba, hakuliendeleza na kwa mujibu wa sheria si lake na wala halijui.


Katika kukanusha, Malecela alisema halijui shamba hilo na wala hajawahi kuwa na umiliki wake lakini pia alisema kama lilikuwapo lilipaswa kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria kwa sababu hakuliendeleza na halikuwa na mwenyewe kwa muda mrefu.


Hata hivyo, pamoja na kutoa ufafanuzi huo Malecela katika kile kinachoelezwa kuwa ni kutambua mkakati unaotekelezwa dhidi ya hatua za kujivua gamba ndani ya CCM, aliweka bayana kuwa mafisadi wanapaswa kuondolewa haraka ndani ya chama hicho.


Kwa upande mwingine, inaelezwa kuwa kuna mkakati wa siri unaoratibiwa kwa njia mahsusi kwa kuwatumia baadhi ya wanasiasa kwa wao wenyewe kujua au kutokujua, kuchafua baadhi ya vigogo wa CCM walio mstari wa mbele kukisafisha chama hicho dhidi ya tuhuma za ufisadi wa baadhi ya vigogo wake waandamizi.


Wanasiasa hao wanaotumika, baadhi kwa kujua na wengine kutokujua wamejikuta wanashabikia baadhi ya hoja kwa ‘kivuli' cha kutetea maslahi ya nchi ni pamoja na baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, eneo ambalo limeelezwa kuwa linatumika kama sehemu mahususi ya mkakati wa kujihami kisiasa.


Taarifa zaidi zinabainisha kuwa mkutano wa sasa wa Bunge la Bajeti unaohitimishwa mwishoni mwa wiki hii, unatajwa kutumika kutekeleza azma hiyo, kupitia uchangiaji hoja katika baadhi ya wizara.


Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa hizo baadhi ya viongozi wanaotajwa kwenye kashfa zilizoibuka bungeni wanahusika moja kwa moja, lakini wengine wameunganishwa kwenye kashfa hizo ili tu kuvuruga mchakato wa CCM kujivua gamba, ambao baadhi ya viongozi waandamizi wamekuwa wakikazia utekelezaji wake, akiwamo Mzee Malecela na Msekwa ambaye ndiye mratibu mkuu wa mchakato huo.


Kwa mujibu wa watoa taarifa wetu, Msekwa ndiye anayetarajiwa kuwasilisha ripoti maalumu katika kikao kijacho cha NEC na taarifa hiyo ndiyo inatarajiwa kuhitimisha kuwavua madaraka baadhi ya viongozi ambao wamekwishahojiwa kwa lengo la kujiengua.


"Kwa sababu wanaopaswa kujiuzulu nyadhifa zao wanashinikizwa kufanya hivyo kutokana na kuhusika katika kashfa za ufisadi, nao wanatekeleza mkakati maalumu wa kutumia kashfa zitakazoaminika katika jamii na kuwahusisha nazo baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM ambao kwa sasa ni nguzo ya Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete kusimamia uamuzi wa kujivua gamba.


"Kwa hiyo ni piga nikupige, ili hatimaye idhihirike kuwa sababu zinazowang'oa katika madaraka zinapaswa kuwarudia pia wasimamizi wa mkakati huo. Na hapa kuna baadhi ya wanasiasa hata wa kambi ya Upinzani na CCM wanatumika wengine kwa kujua na wengine kwa kutokujua," anaeleza mtoa habari wetu na kusisitiza kuwa wapo wanaonufaika kimaslahi na mkakati huo.


Wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Msekwa ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadho ya Ngorongoro (NCCA) alituhumiwa na baadhi ya wabunge, akiwamo Mbunge wa Ngorongoro, Saning'o ole Telele, kuwa amekuwa akiingilia utendaji wa Mamlaka hiyo na amewahi kuhusika kugawa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa hoteli, ikiwamo eneo ambalo ni njia ya wanyama aina ya faru.


Katika tuhuma hizo Msekwa pia alidaiwa kutumia jina la Rais Kikwete kugawa viwanja kwenye eneo ambalo ni njia ya faru na kwamba hatua hiyo ya kugawa viwanja si jukumu lake bali na kwa hiyo amejigeuza Mwenyekiti Mtendaji na ikasisitizwa kuwa kazi yake kama Mwenyekiti wa Bodi ni kuendesha vikao vya Bodi tu.


Tayari Msekwa amekanusha tuhuma hizo na nyingine akisema hakuwahi kutumia jina la Rais kama inavyodaiwa bali Desemba 28, mwaka 2006, Rais alifanya kikao naye pamoja na aliyekuwa Kaimu Mhifadhi wa Ngorongoro, Bernard Murunya, na kuelekeza kuongezwa kwa idadi ya vitanda (hoteli) eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kutokana na eneo hilo kuwa na mahitaji hayo makubwa yanayotokana na idadi ya watalii.


Msekwa anaeleza kuwa aliandika waraka maalumu kuhusu maelekezo hayo ya Rais kuongezwa kwa vitanda katika Hifadhi hiyo kubwa ambayo ilikuwa na hoteli nne tu zisizokidhi haja na kuusambaza kwa wajumbe wote wa Bodi ya NCCA.


Katika maelekezo ya Rais ni pamoja na kuongeza hoteli katika maeneo maalumu kwa kuzingatia taratibu za hifadhi, na kwamba baadaye Rais alijibiwa kuwa upo mpango maalumu wa Mamlaka kuongeza maeneo matano kwa ajili ya hoteli na kambi za mahema.


Hata hivyo, anaeleza kuwa baada ya maelekezo hayo ya Rais ilibidi kuharakisha utekelezaji wa mpango huo na kwa hiyo anajitetea kuwa kila jambo lilifanywa kwa mujibu wa taratibu na si kweli kwamba yeye binafsi alijitwalia mamlaka ya kugawa maeneo.


Kuhusu kashfa nyingine ya kugawa viwanja kwenye hifadhi hiyo, Msekwa anaeleza maombi ya viwanja yalikuwapo mwaka 2005 wakati Kikwete anaingia madarakani naye hakuwa amekwishakuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi.


"Ingawa bodi iliyokuwapo wakati huo ilikuwa imekubali ombi hilo, tathmini ya mazingira (EIA) ilikataa ombi la kampuni ya Kempiski iliyoomba kujenga hoteli kwenye njia ya faru eneo la crater rim kujenga hoteli hiyo. Uamuzi wa kukataa ulitolewa na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), sisi tunaendelea na tutaendelea kusimamia uamuzi wa NEMC).


"Tunaendelea kutekeleza uamuzi wa NEMC kwa kutoruhusu hoteli yoyote kujengwa katika crater rim ndiyo sababu katika orodha ya viwanja vilivyogawiwa na Bodi katika mkutano wake wa 87 wa Oktoba 2007, hakuna kiwanja chochote kilichopo kwenyecrater rim kama Mhe. Telele (mbunge) anavyodai. Yeye anajua hivyo kwa sababu alishiriki kikamilifu katika zoezi hilo," alisema Msekwa katika kukanusha shutuma dhidi yake ambazo pia zinahusishwa na jukumu lake zito ndani ya CCM kwa sasa, kusimamia mchakato wa kujivua gamba.


Tayari baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM wameelezea wasiwasi wao kuhusu ucheleweshwaji wa maamuzi ya kujitoa kwa wana CCM wanaoelezwa wanakipunguzia haiba chama hicho kwa maelezo kwamba kunatoa nafasi kwa watuhumiwa na wafuasi wao kufanya hujuma na kuvuruga hata ufanisi katika utekelezaji wa ahadi na Ilani ya CCM ya mwaka 2010.
 

Forum statistics

Threads 1,355,557
Members 518,682
Posts 33,112,125
Top