Mafisadi wakomba zaidi ya shilingi trilioni moja serikalini | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mafisadi wakomba zaidi ya shilingi trilioni moja serikalini

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, Sep 20, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Sep 20, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,768
  Likes Received: 83,104
  Trophy Points: 280

  Date::9/19/2009Mafisadi wakomba zaidi ya shilingi trilioni moja serikaliniNI FEDHA ZA BAJETI YA WIZARA SITA

  Na Mwandishi Wetu
  Mwananchi


  ZAIDI ya Sh1 trilioni zimechotwa nyakati tofauti kutoka serikalini katika miaka ya hivi karibuni, imefahamika.

  Fedha hizo ni sawa na zile zilizotengwa kwa ajili ya bajeti ya wizara sita kwa mwaka wa fedha 2009/2010, Mwananchi Jumapili imebaini.

  Kiasi cha fedha zilizochotwa kifisadi serikalini na kusababisha baadhi ya wahusika kufikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali, yakiwemo ya uhujumu uchumi, ni S988 bilioni.

  Kwa mujibu wa uchunguzi huo, fedha hizo zinazidi bajeti za wizara kadhaa kwa mwaka huu wa fedha. Katika bajeti ya mwaka 2009/10 Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ilitengewa Sh 21.6 bilioni, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilitengewa Sh478.9 huku Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikitengewa Sh14.0 bilioni.

  Wizara ya Maliasili na Utalii ilitengewa Sh70.8 bilioni, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sh60 bilioni na Wizara ya Mambo ya Ndani Sh bilioni 395.3.

  Baadhi ya watu wanaotuhumiwa kuchota fedha hizo na ambao wana kesi mahakamani ni aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na mwenzake aliyekuwa ofisa utawala kwenye ubalozi huo, Grace Martin ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kuhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh2 bilioni.

  Wengine ni mkurugenzi wa utumishi na utawala wa Benki Kuu (BoT), Amatus Liyumba ambaye anatuhumiwa kuchota Sh221 bilioni, ikiwa ni tofauti ya fedha iliyo katika gharama halisi za ujenzi wa majengo ya ghorofa pacha kwenye makao makuu ya BoT na gharama zilizokuzwa kifisadi.

  Maafisa hao waandamizi wa BoT, wanashtakiwa kwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh221, 197, 299, 200.95 katika mradi wa ujenzi wa minara pacha ya BoT.

  Tuhuma nyingine za uchotaji wa mamilioni ya fedha ni zile zinazodaiwa kufanywa kwenye ununuzi wa rada ambao uliisababishia serikali hasara ya Sh70 bilioni.

  Tayari mchakato wa uchunguzi kuhusu tuhuma hizo umeanza, lakini hadi sasa hakuna aliyekamatwa na kufikishwa mahakamani, ingawa waziri wa zamani wa Miundo Mbinu, Andrew Chenge, ambaye alikuwa mwanasheria mkuu wa serikali wakati wa ununuzi wa rada hiyo, alilazimika kujiuzulu baada ya kutajwa kwenye kashfa hiyo.

  Pia ripoti ya Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), imeonyesha kuwa kuna ufisadi wa Sh2 bilioni zilizotolewa kwa ajili ya kuwekezwa kwenye mgodi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma na Liganga.

  Kwa mujibu wa ripoti hiyo, fedha hizo zilipotea bila kuwekezwa kwenye mgodi huo hivyo kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha.

  Ufisadi mwingine mkubwa ambao baadhi ya wahusika wake tayari wamefikishwa mahakamani ni ule unaodaiwa kufanyika kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na kuisababishia serikali hasara ya Sh133 bilioni.

  Tangu tuhuma za ufisadi huo ulioyahusisha makampuni 22 nchini zitolewe mwaka juzi, hadi sasa watuhumiwa 21 wamefikishwa mahakamani. Watuhumiwa hao, ambao ni mchanganyiko wa wafanyabiashara na wafanyakazi wa BoT, ni wanaume 18 na wanawake watatu.

  Kesi nyingine ambayo inahusu ufisadi ni ya kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond Development Corporation (LLC), ambayo mmiliki wake Naeem Gire, amefikishwa mahakamani. Wizi huo unadaiwa kufanyika mwaka 2006.

  Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited inadaiwa kuchota Sh40 bilioni, huku jumla ya Sh180 bilioni zilichotwa kutoka kwenye Mfuko wa Kuagiza Bidhaa Nje na makampuni mbalimbali.

  Tuhuma nyingine ya ufisadi inahusu kampuni ya kukagua thamani ya uchimbaji madini ya Alex Stewart ambayo mawaziri wawili wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona wameshtakiwa kwa madai ya kutumia vibaya madaraka yao. Mawaziri hao wameunganishwa na aliyekuwa katibu mkuu wa Wizara ya Fedha, Grey Mgonja katika kesi hiyo.

  Mawaziri hao wa zamani, Mramba aliyekuwa Waziri wa Fedha na Yona, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini na Mgonja wanadaiwa kutumia madaraka vibaya na kuitia serikali hasara ya Sh11.7 bilioni.

  Kesi hiyo ambayo imevuta macho na masikio ya wananchi wengi iko mbele ya Hakimu Mkazi John Utamwa.

  Washtakiwa hao watatu wanakabiliwa na mashtaka 12 yakiwemo ya matumizi mabaya ya ofisi na kusababisha hasara hiyo.

  Fedha nyingine zilizochotwa ni zile zilizo kwenye tuhuma za ufisadi zilizoibuliwa na katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa dhidi ya uwekezaji wa Meremeta katika mgodi wa Buhemba, Tangold na Mwananchi kwamba kuna upotevu wa zaidi ya Sh215 bilioni.

  Inadaiwa fedha hizo `zilitafunwa ` katika awamu ya serikali ya Rais Benjamin Mkapa kuanzia 2003 hadi 2006 kupitia wawekezaji wa kampuni ya Tangold inayotuhumiwa `kujimilikisha` mgodi huo kinyemela.

  Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana kutoka BoT, jijini Dar es Salaam, Tangold ilichukua mgodi wa Buhemba ambao kuanzia mwaka 1997 ulikuwa ukiendeshwa kwa ubia na kampuni ya MEREMETA, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Triennex Properietary Limited ya Afrika Kusini.

  Nyaraka nyeti kutoka BoT zilisema kuwa JWTZ na mbia huyo walianza kuchimba dhahabu Oktoba 1997 na baadaye mkataba ulimalizika na Tangold ilijimilikisha mgodi huo kuanzia mwaka 2003 hadi 2006.

  Habari zilidai kuwa Meremeta ilianzisha miradi hiyo kwa kutumia fedha za mikopo kutoka benki ya Nedcor ya Afrika Kusini, ambayo ilichukuliwa na kampuni ya Triennex Properietary kwa niaba ya Serikali ya Tanzania.

  Kwa upande wa Deep Green Finance, Dk Slaa alisema nyaraka mbalimbali hususan rekodi za kibenki zinaonyesha kuwa Sh10,484,005,815.39 ziliingizwa katika akaunti ya Deep Green Finance katika kipindi cha miezi minne tu.

  Katika mwaka wa fedha 2006/07 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), Ludovick Utouh katika ripoti yake alieleza kuwa kiasi cha Sh 3.1 trilioni hupotea kutokana na kutorudishwa kwa risiti za safari na matumizi ya wafanyakazi wa serikalini.

  Utouh alisema katika ripoti hiyo kuwa kiasi hicho cha fedha ni sawa na nusu ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2008/09 ambayo ilikuwa ni kiasi cha Sh7 trilioni.

  Pia wiki iliyopiita vigogo wanne wa BoT walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi ulioisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh104 bilioni katika mkataba wa uchapishaji wa noti.

  Wakurugenzi hao wameshtakiwa kwa makosa tofauti, likiwemo la kupandisha gharama za uchapishaji noti tofauti na gharama za awali zilizo kwenye mkataba mkuu na kusababisha hasara hiyo.

  Waliofikishwa mahakamani ni Simon Jengo, ambaye ni mkurugenzi wa huduma za benki wa BoT, Kisima Thobias Mkango (kaimu mkurugenzi wa fedha), Bosco Kimela (kaimu mkurugenzi wa huduma za sheria) na Ali Farijalah Bakari ambaye pia ametajwa kuwa mkurugenzi wa huduma za benki.

  Kufikishwa mahakamani kwa vigogo hao kumekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza kuwa, kuna kesi tatu zitafikishwa mahakamani wakati wowote dhidi ya vigogo, ikiwa ni mwendelezo wa vita dhidi ya ufisadi.

  Dk Slaa, ambaye pia ni mbunge wa Karatu, akitoa maoni yake kuhusu kiasi cha fedha kilichochotwa na mafisadi, alisema fedha hizo ambazo jumla ya zaidi ya Sh1 trilioni ni mateso kwa serikali.

  Dk Slaa alisema ufisadi utaendelea kuitesa Tanzania kwa kuwa serikali haina uwezo wa kufanya chochote, akitoa mfano wa suala la Deep Green Finance ambalo alisema watuhumiwa wanafahamika na ushahidi upo, lakini serikali haiwakamati.

  ''Ni furaha kwangu kama sasa vyombo vya habari mmeamka kufanya utafiti wenu kwa kuwa nilishasema na siyo trilioni moja tu ni zaidi ya hizo," alisema Dk Slaa.

  Naye Profesa Mwesiga Baregu alisema kiasi hicho ndicho kilichoonekana, lakini kuna uwezekano wa kuwepo kwa fedha nyingi zaidi ambazo zimechotwa.

  Alisema ripoti ya CAG inaweza ikaonyesha fedha nyingine nyingi ambazo zimechotwa kwa kuwa fedha nyingi zinapotea na serikali inakaa kimya. "Serikali imehusika kwa kiasi kikubwa kuhujumu kodi za wananchi hivyo ni vyema wananchi nao wakaiadhibu serikali ili hayo yasitokee tena," alisema Baregu.

   
Loading...