Mafao EAC:Wastaafu sasa watishia kutumia makomandoo

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,009
Imetolewa mara ya mwisho: 22.10.2008 0005 EAT

• Mafao EAC:Wastaafu sasa watishia kutumia makomandoo

*Waonya wataadamana hadi Ikulu zote
*Wataka Rais atumie uadilifu, uaminifu

Na Gladness Mboma
Majira

WASTAAFU wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (T) na wastaafu wengine, wamecharuka na kusema kama Serikali itaendelea kukaa bila kuwalipa mafao yao wataagiza makomandoo na kuandamana nchi nzima katika Ikulu zote.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufuatiliaji, Bw. Benjamin Mutembeyi, alitaka busara na uadilifu na uaminifu wa kimataifa, utumike katika kutatua mgogoro wa mafao ya wastaafu.

"Tunasema kuwa Rais Jakaya Kikwete atumie uadilifu na uaminifu wa kimataifa atulipe mafao yetu kila mmoja kikamilifu kwa haki anayostahili, aachane na ushauri potofu wanaojipendekeza nao kwake mawaziri na maofisa waandamizi wa Wizara za Fedha na Sheria.

"Tunasema hivi kwa sababu tuna hakika ya mia kwa mia tukipeleka kesi hii majuu tutashinda, tunaionea huruma Serikali yetu na wananchi itakapoagizwa kulipa madai na usumbufu maradufu hivyo kuwakamua wananchi kodi zisizo za lazima kulipia mafao haya," alisema.

Alisema Oktoba 16 na 17 mwaka huu, Serikali kupitia Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Omari Mzee, ilitoa kile alichokiita tangazo maalumu kwa vyombo vya habari kudai ni barua za mapunjo za wastaafu 16 tu wa Jumuiya ya zamani ya Afrika Mashariki (T) ndizo zinaonesha kuwa wanastahili kulipwa mafao.

Bw. Mutembeyi alisema tangazo hilo lilidai kuwa hata hivyo, hawatalipwa hadi kwanza Serikali ipate ufafanuzi na uthibitisho wa ajira zao kutoka kwa waliokuwa waajiri wao.

"Hakusema mahesabu ya barua hizo yamefanywa kwa fomula ipi, hadi akadai kwamba wastaafu wengine wote waliowasilisha nyaraka zao za mapunjo wakati huo wakifikia 4,268 eti hawastahili kulipwa chochote na kudai wametumia au wanatumia fomula zao binafsi.

"Huo ni mwendelezo wa uongo na ubabaishaji alioanzisha Waziri wa zamani wa wizara hiyo, Bw. Basil Mramba, uongo huo ulianza kutolewa rasmi na aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Serikali Mama Nyoni kwa niaba ya Katibu Mkuu S. S. Mgonja, alipodai katika tangazo alilolibariki kuwa tangazo maalumu Namba 14/2007.

"Akidai eti Serikali ilikuwa imeishawalipa wana Jumuiya wote, bali eti walikuwa wanaleta madai mapya, huo ni uongo wa Wizara kumdanganya Rais," alisema.

Alisema Jumuiya hiyo iliundwa na Serikali wanachama kama ilivyo Jumuiya ya sasa na ilikuwa na Bunge la kutunga sheria na ikaendeshwa kwa sheria kama Serikali na mafao ya wafanyakazi yalikuwa yanalindwa na bado yanalindwa na kifungu namba 82 cha uliokuwa Mkataba wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya mwaka 1967.

Bw. Mutembeyi alisema sheria namba 11 ya pensheni na sheria namba 13 ya Provident Fund ambazo zilikuwa na kanuni za utekelezaji zikiwamo fomula na fomu mbalimbali, hizo ndizo ambazo wana Jumuiya walijaza au kuziandika kama barua za madai kuitikia agizo la Naibu Waziri alilolitoa bungeni na kurudia Septemba.

Alisema hakuna aliyejitungia fomula yake na kwamba huo ni uongo na ndoto za mchana za Alinacha, za kutaka kuupotosha umma kwa malengo yao ya kuwakata wana Jumuiya asilimia 90 ya mafao yao.

Bw. Mutembeyi alisema Jumuiya ilipovunjika iliutikisa Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) zikazishauri nchi wanachama, kuteua Bneki ya Dunia kushughulikia mgawanyo wa mali na madeni yake, yakiwamo mafao ya waliokuwa wafanyakazi wake wote.

Alisema Benki ya Dunia kupitia wataalamu wake wakiongozwa na Hayati Dkt. Victor Umbricht, ilifanikisha mkataba wa East African Community Mediation Agreement 1984.

Bw. Mutembeyi alisema katika eneo la kulipia madeni na mafao, benki hiyo ilizingatia mambo kadhaa ya kuwalinda wafanyakazi wasiathirike, kubwa likiwa ni kuporomoka kwa thamani za sarafu za Uganda, Tanzania na Kenya kwa kiasi kidogo.

"Kutokana na hali hiyo, iliweka katika article 1 "n" ya mkataba huo kile kinachoitwa weighted average ya sh. 8.31542 za nchi wanachama kuwa sawa sawa na dola moja ya Marekani kuwa ndio msingi wa kulipia madeni na mafao.

"Kwa kulinda thamani hiyo nayo isije ikaangushwa na farigisi (mfumuko wa) ya bei wataalamu wa Serikali ya Uingereza wa uthamanishaji wa fedha za pensheni na Provident Fund Actuarists, waliweka asilimia saba ya riba limbikizi la dola hizo kwa kila mwaka, ambao deni au mafao hayo yatakuwa yamecheleweshwa kulipwa kikamilifu," alisema.

Alisema kwa maana nyingine, benki ya Dunia iliweka bayana kwamba kama bei ya mfuko mmoja wa saruji ilikuwa sh. saba mwaka wa 1977 Jumuiya ilipovunjika ambapo wafanyakazi wote walipaswa kulipwa mafao yao na sasa bei ya mfuko huo ni sh. 20,000, wana Jumuiya wanapaswa kulipwa mafao yao kwa bei ya sasa na Serikali inajua suala hilo.

Aliongeza kuwa lakini inapokuja kwenye utekelezaji, Serikali 'inaota mbawa' na kuwaruka ambapo alitolea mfano hai wa Tume ya pamoja ya mwaka 1998 iliyoeleza Serikali kinagaubaga kwamba njia pekee ya kuumaliza mgogoro wa mafao ya wana Jumuiya ni kuwalipa mafao yao kwa kuwapigia mahesabu yao kwa thamani ya dola ya mwaka 1977 kama Mkataba wa E.A. Mediation Agreement 1984 unavyosema.

"Lakini ripoti hiyo ikabadilishwa ilipopelekwa katika Baraza la Mawaziri, Serikali ikakaidi kutumia thamani ya dola kupigia mahesabu hayo na badala yake ikaamua kutumia thamani ya sarafu ya Tanzania kama ilivyo, licha ya kujua fika kuwa sarafu yake ilikuwa imeporomoka kwa asilimia 10,000 mwaka huo.

"Matokeo yake wanajumuiya wakaishia kulipwa vijisenti vya sh.10 hadi sh. 130. Baada ya vilio vingi na kupelekana mahakamani, Serikali iliunda Tume ya Muafaka ya mwaka 2004/5," alisema

Alisema tume hiyo ilikwenda mbali zaidi ikayapiga mahesabu yakafikia sh. bilioni 450.426 ambazo bila shaka ndizo Rais mstaafu Benjamin Mkapa alizopewa na aliyekuwa Waziri wa Fedha Bw. Mramba akatangaza bayana katika hotuba ya Mei Mosi 2005 mjini Songea kukiri Serikali kuwa na deni hilo kubwa na kuahidi kulilipa kwa awamu.

Bw. Mutembeyi alisema cha kushangaza Waziri Mramba huyo huyo alipeleka bungeni bajeti kiduchu ya kulipa mafao hayo eti ya sh. bilioni 50 tu na kudai akishazitoa hizo kusingeongezwa chochote.

Hivi karibuni Wizara ya fedha na uchumi ilitoa tangazo katika vyombo vya habari ikidai kuwa wastaafu hao walilalamika kuwa fomula iliyotumika kuandaa mafao yao mwaka 2005 haikuwa sahihi.

Wizara ilisema kuwa ombi hilo la wastaafu kukokotoa mafao kwa fomula wanayoitaka lilikataliwa na walielezwa kuwa wao wawasilishe nyaraka za malalamiko ya madai yao ambayo yatachambuliwa na watumishi wa Wizara ya Fedha na Uchumi, ili kuona uhalali wa madai hayo.

Naibu Waziri Bw. Mzee katika tangazo lake hilo alisema malalamiko ya madai yatakayopokewa ni ya mtu binafsi na si makundi.

Pamoja na wastaafu hao 4,269 kuwasilisha nyaraka za malalamiko ya madai yao, Wizara ilisema hawakustahili kulipwa chochote na ni 16 tu, ndio wanaostahili kulipwa.

Wengine walitakiwa wapeleke ufafanuzi na uthibitisho wa uhalali wa ajira na makato kutoka kwa waliokuwa waajiri wao na kwamba huo ndio utakaowafanya wastahili au wasistahili.
 
Back
Top Bottom