Mafanikio ya Ziara za Mikoani za JK: Lindi Report

M

MegaPyne

Guest
SERIKALI YATENGA TSH BIL 3.4 KUNUNULIA KOROSHO


Serikali imetenga shilingi bilioni 3.4 kwa ajili ya chama cha Ushirika cha Ilulu ili kumaliza tatizo la ununuzi wa korosho.


Rais Jakaya Kikwete amewaeleza wananchi wa Lindi mwishoni mwa ziara yake ya siku sita mkoani Lindi kabla ya kufanya majumuisho ambapo ameongea na viongozi wote.

Serikali ya awamu ya nne ina lengo la kuongeza na kuboresha kipato cha wananchi wake nchini kote.

“Tunataka ushirika wa Ilulu ukopesheke” amewaasa viongozi katika kikao cha majumuisho.“ Muweke ajenda katika vikao vyenu ili muwe mnazungumzia mambo ya ushirika wenu, matatizo myajue mapema na kuyatatua mapema ili mfanikiwe kwani ushirika ukishindwa hakuna matumaini tena kwa mkulima, hivyo ni muhimu kusimamia haki ya mkulima” amesema.

Rais Kikwete pia amewaeleza viongozi kutenga maeneo kwa ajili ya ufugaji, viwanda na mahoteli ili kuweza kuvutia uwekezaji na watalii Hata hivyo amewatahadharisha viongozi kutouza ardhi kiholela mkoani humo na kuwatahadharisha viongozi kutopata vishawishi.

‘Pangeni vizuri na utoaji wa ardhi muusimamie vizuri ili kuepukana na migogoro hapo baadaye” amesema

Baada ya kutatua tatizo kubwa lililokuwepo la ununuzi wa korosho, Rais amehimiza wananchi kukuza na kuendeleza mazao ya ufuta na dengu ili kuongeza mazao mengine ya kibiashara mkoani Lindi kwa nia ya kuongeza kipato kwa wananchi.


Kwa ujumla serikali imepiga hatua kubwa kimaendeleo mkoani Lindi kwa kutimiza ahadi zilizotolewa na Chama Cha Mapinduzi wakati wa kutafuta kura mwaka 2005.


ELIMU

Mafanikio makubwa yameonekana katika Elimu ambapo watoto wote wenye umri wa kuenda shule wameingia darasa la kwanza na waliofaulu wamepata nafasi za kuingia sekondari kwa kiwango cha asilimia mia moja.

Hata hivyo bado kuna tatizo la watoto wengi kutomaliza masomo yao ya msingi na sekondari kwa sababu za utoro na mimba kwa watoto wa kike ambapo zaidi ya nusu ya watoto wanaoanza shule hawamalizi masomo yao.

Rais amewahimiza viongozi kuzingatia pia ujenzi wa maabara na hosteli ili watoto wengi wabakie shuleni na kuepuka na vishawishi wanavyopata wakikwa majumbani kwao.

MIUNDO MBINU.

Mkoa wa Lindi umekuwa na kilio cha barabara kwa muda mrefu sasa lakini kwa jitihada na mipango ya makusudi matengenezo makubwa ya barabara za mkoa, wilaya na za vijijini,yamefanyika na yanaendelea kufanyika ikiwemo ujenzi wa madaraja.

Ili kuongeza katika juhudi za kuleta maendeleo mkoani Lindi Rais Kikwete amesema serikali ina mpango wa kuweka lami katika viwanja vya ndege vya Lindi na Kilwa ili mikoa ya Kusini ambayo ina fukwe na hifadhi kubwa ya misitu iwe kivutio cha utalii na uwekezaji.

MAJI.
Pamoja na kwamba maji bado ni tatizo mkoani Lindi, serikali imetenga bajeti kubwa kwa ajili ya huduma ya maji nchini kote.

Rais amesema tatizo hili ambalo tayari linashughulikiwa na kuwekewa mipango kamili, litakwisha katika miaka michache ijayo na tofauti itaonekana. Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kujenga visima, mabomba chini ya mradi mkubwa wa maji kwa lengo la kuimarisha huduma ya maji katika vijiji mbalimbali mkoani Lindi na pia katika sehemu zingine kote nchini bajeti imeongezwa kwa zaidi ya asilimia sitini ili kusambaza huduma hiyo hadi vijijini nchini kote

UMEME.

Katika ilani ya CCM mikoa ya Lindi na Mtwara iwe imepata umeme ifikapo mwaka 2010, lakini ahadi hiyo inatimia ifikapo mapema mwakani kutokana na gesi asilia ya Msimbati na tayari mipango ya kusambaza umeme huo hadi vijijini umeshakamilika.
Serikaliimeanza kutenga pesa chini ya mfuko wa umeme kwa nia ya kusambaza umeme vijijini.

AFYA.

Rais amewambia wananchi kujiandaa na mpango mwingine wa serikali wenye lengo la kujenga kituo cha afya katika kila kata nchini ili wananchi wake wasitembee zaidi ya kilomita 5 kutafuta huduma ya afya.

Rais pia amesisitiza wananchi kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa ukimwi na kuwaasa viongozi kutokuwa na haya kuzungumza na wananchi juu ya ugonjwa huu na jinsi ya kuchukua tahadhari Rais amekamilisha ziara mkoani humo leo na atarejea Dar-es-salaam tarehe 19.Novemba.

Ziara za Rais Kikwete mikoani zinatarajiwa kukamilika mwakani ambapo anatarajia kutembelea mikoa na wilaya zote nchini, tayari ametembelea mikoa 13 hadi sasa.

Source: Ikulu
 
anazidi weka mahadi tuuu akumbuke ahadi ni deni...na mtu kuja kukudai deni ni haki yake.....
 
Back
Top Bottom