ZHUKOVSKY, URUSI – Ndege ya kihistoria ya usafiri wa abiria ya mwendo kasi wa juu zaidi ya sauti (Supersonic Transport) Tupolev Tu-144D yenye namba ya usajili CCCP-77115, inafanyiwa ukarabati na kurejeshwa katika hali nzuri kupitia mradi unaoendeshwa na watu wa kujitolea katika Uwanja wa Ndege wa Zhukovsky, karibu na Moscow nchini Urusi.
Mradi huo unalenga kuhifadhi ndege hiyo maarufu iliyokuwa sehemu muhimu ya historia ya maendeleo ya teknolojia ya usafiri wa anga wa kasi ya juu duniani.
Kazi za ukarabati zinajumuisha kufungwa kwa kifaa cha kuzalisha umeme wa ziada (Auxiliary Power Unit – APU) aina ya TA-6A, marekebisho ya mifumo ya nyaya za umeme, vifaa vya ndani ya chumba cha marubani, taa pamoja na mifumo ya tahadhari.
Aidha, mafundi na wajitolea wanafanya kazi ya kurejesha mfumo wa pua ya ndege inayoweza kuinama kuelekea chini (droop nose), ambao ulikuwa moja ya ubunifu muhimu uliowezesha marubani kupata mwonekano mzuri wakati wa kuruka na kutua.
Ukaguzi wa betri na matairi pia unafanyika kama sehemu ya maandalizi ya kuhifadhi na kuonesha ndege hiyo kwa umma.
Kwa mujibu wa taarifa za mradi huo, kuna matarajio kwamba Tu-144D CCCP-77115 inaweza kuoneshwa katika hali tuli (static display) wakati wa maonesho ya anga ya MAKS 2027.
Tupolev Tu-144 ilikuwa ndege ya kwanza ya abiria yenye uwezo wa kuruka kwa kasi inayozidi kasi ya sauti kuanza safari za kibiashara, ikiwa imeitangulia Concorde katika historia ya usafiri wa anga wa aina hiyo.
Hata hivyo, kurejeshwa kwa ndege hiyo kwa ajili ya maonesho hakumaanishi kwamba itarejeshwa katika hali ya kuruka. Kwa sasa, lengo kuu ni kuhifadhi urithi wake wa kihistoria na kiteknolojia kwa ajili ya vizazi vijavyo.