SoC01 Mabadiliko ya kweli

Stories of Change - 2021 Competition

Truthh

New Member
Sep 20, 2021
2
1
Habari wana jf. Ni matumaini yangu kila mmoja wetu anaendeleza harakati za kutengeneza maisha bora kwake na familia yake na taifa kwa ujumla.


Kwa takwimu zilizopo Tanzania ni moja ya nchi masikini duniani licha ya utajiri mkubwa tulionao wa rasilimali ikiwemo watu, madini, vivutio vya utalii, mlima mrefu zaidi Africa n.k.

Tuliamini kuwa ongezeko la wasomi katika nchi lingesaidia kuongeza tija katika nchi lakini matarajio yetu yamekua sio sahihi kwani mamilioni ya wanafunzi wanahitimu kila mwaka na hakuna mtu wa kuwaajiri. Serikali pamoja na sekta binafsi zote kwa pamoja zimeshindwa kumudu uhitaji wa ajira uliopo katika jamii swala ambalo limepelekea yafuatayo;​
  • Ongezeko kubwa la vijana ambao hawana ajira​
  • Kutokana na uhitaji mkubwa wa ajira, waajiri wametumia nafasi hiyo kushusha kiwango cha mishahara wanacholipwa wafanyakazi hasahasa pale wanapoanza kazi.​
  • Kupoteza thamani kwa mfumo wa elimu katika nchi. Kama kuna kipindi elimu ya Tanzania imepoteza thamani ni katika kipindi cha miaka 15 iliyopita hadi sasa. Kwa sasa Tanzania msomi aliehitimu chuo kikuu hana tofauti sana na kijana alieshia kidato cha nne na akaenda kusomea ufundi seremala veta. Hii ni kwa sababu kutokana na ukosefu wa ajira wasomi wanajikuta wanafanya kazi ambazo hazihitaji taaluma yoyote hivyo jamii inabaki inajiuliza walisoma mpaka chuo kikuu wakitafuta nn. Ni uhalisia usiopingika wote katika pitapita zetu tunakutana na msomi aliehitimu chuo kikuu akifanya kazi zisizohitaji taaluma ilimradi tu aweze kupata japo pesa ya kujikimu kimaisha​
  • Ongezeko la rushwa za ngono. Rushwa ya ngono imeongezeka sana katika kipindi ambacho ajira imekua changamoto kubwa katika nchi. Dada zetu wasomi wanajikuta wakiombwa kutoa rushwa ya ngono ili waweze kupatiwa kazi tena yenye mshahara mdogo katika maeneo mbalimbali katika nchi.​
  • Ubora na hali ya maisha kwa mtanzania wa kawaida vimezidi kushuka kila leo. Tupo katika zama ambazo maisha yamekua magumu sana kupita kiasi. Wazazi walijitoa kusomesha watoto kwa lengo kuwa watoto watawasaidia katika uzee wao kitu ambacho imekua ndivyo sivyo kwani hali ya maisha inapelekea vijana kushindwa kutunza hata familia zao hasa wazazi wawapo katika umri wa uzee​
  • Ongezeko la chuki na ukosefu wa uzalendo. Sijui kuhusu wewe lakini binafsi siwezi kuwa mzalendo kama nchi yangu imeshindwa kuweka mfumo endelevu wa kusaidia mamilioni ya vijana kupata ajira au kuanzisha biashara zao ili wajikimu. Hali ngumu inapelekea hali ya chuki kwa viongozi na ukosefu wa uzalendo katika nchi.​
NINI KIFANYIKE TUWEZE KUPATA MABADILIKO YA KWELI?
Ili kuweza kupata mabadiliko ya kweli napendekeza serikali, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wananchi kuona umuhimu na uhitaji mkubwa wa mabadiliko katika nyanja zifuatazo;
  • MABADILIKO KATIKA MFUMO WA ELIMU. Iko wazi kwa sasa mfumo wa elimu haumpi kijana wa kitanzania maarifa anayohitaji ili kuweza kufanikisha katika maisha. Hii ndio inapelekea mamilioni ya wahitimu kutokujua nini cha kufanya pale wanapokosa ajira. Asilimia kubwa ya mifumo yetu katika nchi za kiafrika ni ile ambayo tulirithi kutoka kwa wakoloni. Miaka 50 mbele bado hatujaweza kuanzisha mifumo yetu binafsi kama nchi. Mfumo wa sasa wa elimu unamtengeneza sana mwanafunzi kukariri anapofundishwa kuliko kuelewa. Hii ndo maana mwanafunzi anaweza kufaulu masomo yake kupitia kukariri paipo kuelewa sana kile kilichofundishwa. Lakini pia tunahitaji mfumo ambao utamuandaa mwanafunzi kwa kumpatia ujuzi utaomsaidia kutotegemea ajira bali kuweza kujiajiri. Hili linawezekana kwa kuanzisha elimu ya fedha mashuleni na kuandaa watoto tokea wanapokua wadogo waweze kujikita katika masomo kadhaa na sio yote. Haileti maana mtu anasoma chemistry au physics wakati ndoto zake ni kuwa mwanasheria. Ni vyema kuwa na wataalamu wa saikolojia mashuleni ambao wataweza kutambua vipaji vya watoto tokea wadogo hivyo wasome masomo yanayoendana na vipaji vyao. Hii itasaidia wanafunzi kusoma vitu wanapenda na kupata ujuzi utaowasaidia hasa pale wanapomaliza vyuo vikuu
  • KATIBA MPYA. Nchi yoyote inaendeshwa kupitia katiba hivyo mabadiliko ya kweli katika nchi yataanza pale ambapo katiba itabadilika pia. Katiba ya sisi haiendani na uhitaji wa sasa wa nchi. Kama tunavojua katiba ndio sheria mama hivyo basi ni vyema tukiweza kupata katiba mpya ambayo italeta tija ya kweli katika jamii. Katiba mpya italeta uwajibikaji kwa viongozi hasahasa wale wanaolewa madaraka na kusahahu dhamana waliopewa na wananchi. Katiba mpya pia italeta ukweli na uwazi katika chaguzi zetu mbalimbali. Hatuwezi sema tuna tume huru ya uchaguzi wakati kiongozi wa hiyo tume anachaguliwa na Rais ambae na yeye pia ni moja ya wagombea. Hakuna uhuru apo. Hatuwezi sema tuna mahakama huru wakati jaji mkuu anachaguliwa na Rais. Hii inapelekea mahakama kushindwa kusimamia sheria kwa uweledi hasahasa pale katiba inapovunjwa na serikali. Mfano sakata la waliokua wabunge wa chadema kuvuliwa uanachama hivyo kupoteza sifa za kuwa wabunge lilionyesha jinsi gani katiba inavunjwa katika nchi hii na mahakama haiwawajibishi wanaofanya hivyo. Spika wa bunge alivunja katiba kwa kuwaruhusu wabunge wale kuendelea kuwa bungeni japo wapoteza sifa lakini serikali kuu pamoja na mahakama wote walikaa kimya. Mabadiliko ya katiba yatatupatia taasisi ambazo zitakua na uhuru wa kweli wa kusimamaia masilahi mapana ya nchi kulingana na katiba inavotaka.
ELIMU YA UONGOZI ITOLEWE NA VIONGOZI WAWE NA SIFA NA VIGEZO VINAVOSTAHILI. Hivi kweli kama nchi tulikaa tukaamua kwamba kigezo cha mtu kuwa mbunge ni kujua kusoma na kuandika tu? kweli mtu mwenye elimu ya darasa la saba tu ana elimu inayohitajika kuwawakilisha wananchi bungeni pamoja na kushiriki ipasavyo katika utungaji wa sera na sheria mbalimbali zinaoiongoza nchi? Kutokua na vigezo vya msingi wakati wa kuchagua viongozi imepelekea uongozi kuwa sehemu ya kutafuta maisha kwa baadhi ya watu.

Kipindi cha uchaguzi tunaona ongezeko kubwa la watu ambao hawana sifa za kuwa viongozi wakigombea kuwa viongozi. Wanatumia umaarufu wao katika jamii ( wasanii wa muziki, wachekeshaji, waigizaji n.k ) kushawishi wananchi wawachague kuwa viongozi. Lakini je hawa ni watu sahihi kusimamia masilahi mapana ya nchi? Napendekeza kuwepo na vigezo vya kweli katika kupata kiongozi. Uongozi sio kitu cha mchezo kwamba mtu yeyote anaweza. Iwepo elimu ya uongozi ambayo mtu yeyote anaehitaji uongozi awe amepitia elimu hiyo na kufaulu. Nachokiona kwa sasa ni kundi kubwa la vijana wanaotaka kutumia uongozi kama njia ya kutafuta maisha. Ndio maana utasikia wengi wao wakipata tu uongozi wanachukua mikopo mikubwa kwenye mabenki kuendesha miradi yao.

UWEKEZAJI MKUBWA UFANYIKE KATIKA SEKTA YA MICHEZO. Ni kweli ajira ni tatizo kubwa katika nchi mbalimbali. Nchi za wenzetu zimewekeza sana katika michezo kama njia mojawapo ya kuongeza ajira. Hii ni wazi sana na ndio maana tunaona michezo aina mbalimbali katika nchi zilizoendelea. Kuwa na aina mbalimbali za michezo kutaongeza ajiira katika jamii pamoja na mapato kwa serikali hivyo basi ni wakati serikali na wawekezaji kuliangalia suala la michezo kwa jicho la kipaumbele

ONGEZEKO LA MIRADI YA KIMKAKATI. Kuna msemo wa kingereza unasema "without plan you are planning to fail". kama nchi inatakiwa tuwe na mipango maalumu ya miradi ya kimkakati, miradi ambayo ikifanyika italeta mabadiliko ya haraka katika uchumi pamoja na kutengeneza ajira. mfano utengenezaji wa bandari ya bagamoyo ambayo itahudumia nchi nzote za ukanda wa afrika mashariki kupitia reli kama ilivoandikwa katika mpango wa viwanda wa 2025 itasaidia katika ongezeko la ajira pamoja na kuleta mabadiliko ya haraka katika uchumi wa nchi.

KUNUNUA HATI MILIKI YA TEKNOLOJIA KUBWA AMBAZO SISI HATUNA. Dr Richard Buckminster Fuller aliwahi kusema "learn to do more with less". Kama nchi bado tupo nyuma katika nyanja za teknolojia lakini hiyo isiwe sababu ya sisi kushindwa kusonga mbele kwa njia za kibunifu. Ununuzi wa hati miliki ( Patent rights ) ni njia mbadala inayoweza kutumika katika kununua haki za kutumia teknolojia fulani ambayop sisi hatuna. Cocacola Tanzania wanatumia teknolojia ya Coca Cola kutengeneza soda tunazotumia hapa nchini. Nchini Rwanda serikali iliweza kununua hati miliki za utengenezaji magari ya kampuni ya volkswagen hivyo kuongeza ajira katika nchi na kuleta mabadiliko chanya katika uchumi. Hivyo tunaweza kujifunza kupitia majirani zetu kwa kutafuta teknolojia ambazo tunaeza zitumia kwa kutumia hati miliki kwa lengo la kuongeza viwanda katika nchi hivyo kuongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi.

NISHATI YA GESI NA UMEME. Bila gesi na umeme ni kama mtu anaetaka kuendesha gari bila kuwa na funguo na mafuta. Hakuna maendeleo ya viwanda na uchumi bila ya kuwa na upatikanaji wa uhakika wa nishati ya gesi na umeme. Tanzania tumebarikiwa kuwa na gesi inayopatikana mtwara. Hii ni baraka kubwa sana. Tukicheza karata zetu vizuri nishati ya gesi inauwezo wa kuleta mabadiliko makubwa sana kiuchumi katika nchi.

Tunavoelekea mbele ni vyema serikali pamoja na wadau kuangalia namna nishati ya gesi itatumika kuzalisha umeme wa uhakika katika nchi. Baadhi ya tafiti zinaonesha umeme wa gesi ni wa uhakika zaidi na bei nafuu kulinganisha na umeme unaozalishwa kwa maji. Matumizi ya gesi pia yatasaidia katika kupambana na uchafuzi wa mazingira kwa kuhamasisha matumizi ya gesi majumbani na sio mkaa. Kwa sasa siku ikipita bila umeme kukatika ndio watu tunashangaa sababu ishakua mazoea kwamba hatuna umeme wa uhakika. Bila umeme wa uhakika hatuwezi piga hatua kama taifa.

UTUNZAJI WA MAZINGIRA UPEWE KIPAUMBELE. Uchafuzi wa mazingira limekua ni tatizo la kidunia sio tu Tanzania. Uchafuzi wa mazingira umepelekea mabadiliko ya tabia ya nchi, ukame, mafuriko, mabadiliko ya hali ya hewa hasahasa ongezeko la joto duniani. Bila jitihada za msingi tutashindwa kuandaa mazingira yanayofaa kwa vizazi vijazo. Jitihada hizi ni vyema zikianzia katika familia zetu. Ni wakati sasa tufanye maamuzi tukiwaza vizazi vijavyo.

Tupunguze matumizi ya mkaa, ukataji miti, utupaji takataka ovyo katika vyanzo vya maji badala yake tujikite zaidi katika matumizi ya gesi pamoja na mkaa mbadala, matumizi sahihi ya vyoo pamoja na taratibu sahihi za utunzaji taka. Kama nchi itungwe sheria kila kaya ipande miti katika eneo lake na ukataji miti au uchafuzi wa mazingira liwe ni kosa lenye adhabu kali. Hii itasaidia utunzaji wa mazingira uzingatiwe katika maeneo mbalimbali ya nchi

KAMA TUMEKUBALI DEMOKRASIA BASI VYAMA VIPEWE UHURU WA KUFANYA SHUGHULI ZAO MBALIMBALI ZA KISIASA BILA WASIWASI WA KUPEWA KESI ZA UHUJUMU UCHUMI NA UGAIDI. Hii kitu imekua ni muendelezo sasa katika nchi yetu. Tunauaminisha ulimwengu kuwa sisi ni nchi yenye amani na demokrasia lakini cha kushangaza demokrasia inasahaulika pale serikali ikikosolewa. Serikali inaongozwa na watu hivyo ni kawaida kuwa na mapungufu sababu binadamu hatujakamilika. Tanzania ukiikosoa serikali wewe unaonekana ni adui.

Viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani nchini wamekua wakifanya siasa katika mazingira magumu sana. Wamepewa kesi za uhujumu uchumi, ugaidi n.k kama njia ya kuwanyamazisha. Marakadhaa tunaona polisi wanavyotishia watu wanaotaka kufanya maandamano kudai haki zao mbalimbali. Katiba ya nchi inatuambia tuna uhuru wa kuzungumza pamoja na kuandamana lakini kwenye macho ya serikali mtu anaeandamana ni adui na ndio maana waandamanaji wanakutana na vipigo vizito na mabomu ya machozi kutoka kwa polisi.

Nashauri kama tumechagua demokrasia basi waache watu waongee yaliyomo moyoni hata kama yatakukera. Na kama sivyo basi tuchague mfumo mpya kikatiba ambao utakua na chama kimoja tu ili serikali itimize malengo yake kuliko kuwaaminisha watu tuna vyama vingi alafu nyuma ya pazia unacheza rafu au ndo ile Alikiba alisema unaniibia "penseli alafu unanisaidia kutafuta?'

AFYA NJEMA NA ULAJI SAHIHI. Tukubaliane kabisa kwamba asilimia kubwa ya magonjwa yanayoitesa dunia kwa sasa ni magonjwa yasioambukizwa kama kisukari, presha, kansa n.k. magonjwa haya yote yanasababishwa kwa asilimia kubwa na ulaji mbovu. Wazungu wanasema " You are what you eat". Ulaji sahihi ni kitu muhimu sana ili kutengeneza afya njema. Ukila vyakula sahihi magonjwa utayasikia redioni lakini ukiendekeza ulaji mbovu, matumizi ya pombe yaliyopitiliza, uvutaji wa sigara uliokithiri basi unatengeneza mazingira ya kushambuliwa na magonjwa sugu huko mbeleni. Jamani tujitajhidi sana kula vizuri. tunywe sana maji kuliko soda na pombe, tule sana matunda na michemsho kuliko wanga na mafuta yani colestro, tule sana mbogamboga kuliko nyama nyekundu.

BILA SEKTA BINAFSI HATUENDI POPOTE. Uchumi unakuzwa na sekta binafsi na sio vinginevyo hivyo basi serikali iweke sera bora za uwekezaji zitazoiwezesha sekta binafsi kukua na kuanzisha miradi mbalimbali itayokuza uchumi wa nchi pamoja na kuongeza ajira.

Ni hayo tu ndugu zangu. Ni matumaini yangu ntakua nimeongeza chochote katika jamii
Usisahau kunipigia kura kama ukiona nilichoandika kina mashiko..

Asanteni​
 
KIKWAZO KIKUBWA KINACHOIKWAMISHA TANZANIA NI KWA SABABU;
Democracy kwa Watanzania inashambuliwa na maadui waitwao;-

1. Ukanda,

2. Ukabila,

3. Serikali za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,

4. Udini

6. Uzao wa waliowahi kuwa viongozi wa nchi.

7. Ujinga wa washiriki katika Democrasia ambao huwafanya wawe wasaliti kati ya walioibuliwa na majukwaa ya vyama vya Upinzani.

CCM ni Carpet tu la kupitia kwa wanaolenga kuya_win hayo maadui 7.
 
Back
Top Bottom