Mabadiliko ya kijamii yanavyoathiri malezi

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,569
9,429
Jamii yetu inapitia mabadiliko makubwa yanayotulazimu kutafakari upya wajibu wetu kama wazazi. Mtindo wa malezi umebadilishwa na mageuzi yanayoendelea katika jamii. Wiki iliyopita, tuliangalia mifano kadhaa. Kwanza, ajira na migogoro ya kifamilia inayoongeza umbali kati ya wazazi.

Pili, kumomonyoka kwa ukaribu wa kifamilia kwa sababu mbalimbali na tatu kufunguka kwa fursa zinazowawezesha kinamama kuingia kwenye soko la ajira.
Haya matatu yanawadai wazazi kufikiri namna wanavyoweza kuwalea watoto wao bila kuathiri ufanisi wa shughuli zao.

Makala haya yanaendelea kuangazia mabadiliko mengine manne yanayoibua changamoto tunazohitaji kuzitazama kwa karibu.

Udhibiti hafifu wa taarifa
Watoto wetu wanaishi kwenye zama za maendeleo ya habari na mawasiliano. Taarifa, zikiwamo zile asizozihitaji mtoto, zinapatikana kirahisi. Upatikanaji huu wa taarifa unamwezesha mtoto kujifunza kirahisi kuliko ilivyokuwa zamani.

Hata hivyo, si mara zote taarifa anazozipata mtoto zina tija. Bila udhibiti mzuri wa taarifa, mtoto anaweza kujifunza mambo yanayomtangulia ufahamu wake.

Kwa mfano, michezo ya kiteknolojia inayofahamika kama ‘games,’ pamoja na kusisimsha ufahamu wa watoto, zipo tafiti zilizobaini kuwa michezo hii inaweza kutengeneza mazingira ya kuwashawishi watoto kufanya maamuzi potofu.

Sambamba na hilo, tabia ya kutazama televisheni, mbali na kuwafundisha watoto tabia zisizotarajiwa, huwajengea watoto matarajio yasiyofikika katika hali halisi. Wazazi wasioweza kuyaishi matarajio hayo wanaweza kujikuta katika wakati mgumu.

Televisheni na filamu aghalabu huonyesha matumizi ya nguvu kupita kiasi. Vipande vinavyoonyesha matukio ya ukatili huwasisimua watoto. Vitendo hivi vina uwezekano mkubwa wa kuwafundisha watoto namna mbaya ya kuonyesha hasira na matumizi ya mabavu.

Udhibiti wa taarifa anazozipata mtoto kupitia zana hizi za kiteknolojia, unategemea kwa kiasi kikubwa na ukaribu wa watu wazima katika mazingira aliyomo mtoto.

Bahati mbaya hili linakuwa gumu kwa sababu hao wanaotarajiwa kumuongoza mtoto kutafsiri kile anachokiona, wamebanwa kwenye shughuli nyingine muhimu za maisha.

Pilika nyingi za maisha
Tumebadili tafsiri ya kile tunachokiona kuwa ni mafanikio katika maisha. Siku hizi kufanikiwa kunachukuliwa kama uwezo wa kujilimbikizia mali kadri inavyowezekana.

Ili kufikia malengo hayo, kazi kubwa lazima ifanyike. Kipaumbele cha maisha kimekuwa ni kutafuta fedha ili kukidhi tafsiri mpya ya maendeleo.

Mzazi wa sasa ana mambo mengi ya kufuatilia kuliko ilivyokuwa zamani. Saa zinazotumika kwenye pilika za maisha ni mara dufu ya muda wa kukaa na familia. Kwa mfano, mzazi anayejituma kuchapa kazi anaweza asipate muda wowote wa kujua kile kinachoendelea kwenye maisha ya mtoto. Mambo ni mengi kuanzia Jumatatu mpaka Jumapili. Mama yuko ‘bize’ kama alivyo baba.

Matokeo ya pilika hizi ni kusahaulika kwa familia ambayo ni eneo muhimu la maisha. Watoto wetu wanalipa gharama ya shauku zetu za kupata mafanikio. Wanatuhitaji kihisia lakini hatupatikani. Matokeo yake tunapata vitu tunavyoweza kuwarithisha lakini wakati huohuo wakipotelea kwenye tabia zisizokubalika.

Shinikizo la matarajio
Maendeleo ya ‘kisasa’ yametufanya wazazi tuwe na matarajio makubwa kwa watoto kuliko zamani. Tumewatengenezea watoto shinikizo kubwa la kufanikiwa. Ili kukidhi matarajio hayo, tumeamini mtoto lazima asome na kufaulu.

Tunapima mafanikio ya mtu kwa kigezo cha ufaulu wa mitihani.Hakuna tatizo la kuwa na matarajio makubwa. Kufikiri mambo makubwa ni kichocheo cha kujituma na kujibidiisha. Hata hivyo, matarajio hayo lazima yazingatie hali halisi.

Mhadhiri wa elimu ya awali wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Lyambene Mutahabwa, alibaini kwamba matarajio makubwa tuliyonayo wazazi yanaathiri makuzi ya watoto. Kwa mfano, kwa sababu ya matarajio makubwa, wazazi huwapeleka watoto shule kabla ya wakati. Mtoto mwenye miaka mitatu anaanza kutarajiwa ajue kusoma, kuandika na kuhesabu.

Mtoto huyu anapoandikishwa kwenye darasa la awali, walimu wanakuwa na kazi ya kufikia matarajio ya wazazi. Wanafikiri shughuli muhimu waliyonayo kama walimu bora ni kuhakikisha mtoto mdogo ‘anaivishwa kitaaluma.’

Wazazi hawatarajii mtoto acheze, aimbe, akosee, afeli, ajifunze. Muhimu ni kujua Kiingereza iwe isiwe. Matokeo yake watoto wanatumia muda mwingi kwenye taaluma ambayo wakati mwingine inazidi umri wao.

Tunawasomesha watoto kwenye shinikizo kubwa. Ukubwa wa matarajio haya unatufanya wazazi tusitambue juhudi kubwa zinazofanywa na watoto. Mtoto anapokuja na alama 70 nyumbani hatuoni. Tunakuwa wepesi wa kukemea uzembe. Kwa namna hii, tunawavunja watoto moyo kujibidiisha.

Mwingiliano wa tamaduni
Kabila lilikuwa kigezo kimoja muhimu kilichoamua hatma ya uhusiano wa watu wawili waliotaka kuishi pamoja. Ilikuwa mwiko na kosa kubwa kwa makabila kuoeleana.

Kufanana kwa utamaduni kati ya wazazi kulifanya iwe rahisi kujua kipi mtoto afundishwe na kipi hakifai. Mstari wa ‘mema’ na ‘mabaya’ ulikuwa bayana.

Mfano rahisi ni mgawanyo wa kimajukumu kijinsia. Mtoto wa kike alijua kwa hakika kipi alipaswa kukifanya na wa kiume vivyo hivyo. Hapakuwa na mjadala mzito wa nani afanye nini kuanzia kwa wazazi wenyewe mpaka kwa watoto.

Sasa hivi tumeendelea. Hakuna mipaka ya utamaduni. Hata hivyo, mwingiliano huu wa tamaduni za jamii umetengeneza hali fulani ya kuchanganyikiwa. Hatujui kipi kinapaswa kufanywa na nani.
Kwa sisi tulio wazazi wapya, kwa mfano, imekuwa vigumu kujua majukumu yetu nyumbani. Mama anatarajia baba afanye majukumu ambayo baba naye anatarajia yafanywe na mama.

Katika mazingira haya, watoto wanakosa watu wazima wanaoweza kuwaonyesha mfano wa kile kinachopaswa kufanywa. Mkanganyiko huu haukuwepo zamani.

Tafsiri ya mabadiliko haya
Mabadiliko haya makubwa ya kijamii yameibua changamoto mpya za malezi. Katika kukabiliana nazo, hatuwezi kuendelea kuamini kuwa kuwa malezi ni jambo rahisi lisilohitaji kujifunza.

Sisi kama wazazi tuna kazi ya kwenda sambamba na mabadiliko hayo. Tunahitaji kubadilika na kujifunza namna ya kukabiliana na changamoto hizi ambazo wazee wetu hawakuzishuhudia.
 
Sisi kama wazazi tuna kazi ya kwenda sambamba na mabadiliko hayo. Tunahitaji kubadilika na kujifunza namna ya kukabiliana na changamoto hizi ambazo wazee wetu hawakuzishuhudia...

Nimekupata sana mtoa mada
 
MI NAHISI CHANZO KIKUBWA SANA NI WAZAZI KUWA BIZE NA KUUKABILI UGUMU WA MAISHA.MTU UNATOKA SAA 11 ASUBUH NA UNARUDI SAA 4 USIKU,LABDA NA MKEO NAE ANATOKA UNATEGEMEA NINI?WATOTO WATAANGALIE VIPINDI VIBOVU,KUWA HURU KUTEMBEA POPOTE NA KUFANYA LOLOTE LILE
 
Back
Top Bottom