Mabadiliko Ya Katiba Visiwani Zanzibar | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mabadiliko Ya Katiba Visiwani Zanzibar

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by X-PASTER, Aug 10, 2010.

 1. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #1
  Aug 10, 2010
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Mabadiliko Ya Katiba Visiwani Zanzibar

  Na Salma Said,

  WAJUMBE wa baraza la wawakilishi jana wamekutana na kujadili rasimu ya sheria ya mabadiliko ya katiba itakayowezeshwa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu wa octoba 31 mwaka huu.

  Wajumbe hao walikutana katika jengo jipya la baraza la wawakilishi, mtaa wa chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar walieleza umuhimu wa kuzika tofauti zao za kisiasa zilizokuwepo tokea kuaznishwa kwa mfumo wa vyama vingi 1992 ili kujenga mustakabali mpya wa Zanzibar .

  Baadhi ya wajumbe hao wakiwa na hamasa ya kuzingumzia serikali ya umoja wa kitaifa ambayo majimbo 10 walipiga kura ya kuikataa walimwagia sifa nyingi rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume na katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad wakipendekeza wapewe tunzo maalumu ya kimataifa kuwashukuru.

  “Mheshimiwa Spika, Karume na Maalim Seif wameifanyia mengi na mazuri Zanzibar kwa hivyo wanastahili kutunzwa kama wanavyotunzwa viongozi wengine duniani. Tunzo ya Nobel na Mo Ibrahim zinawafaa” alisema Said Ali Mbarouk Mwakilishi wa jimbo la Gando (CUF).

  Haroun Ali Suleiman jimbo la Makunduchi (CCM) ambaye jimbo lake ni miongoni mwa majimbo yalioongoza kwa kupiga kukataa alisikitika kwa matokeo hayo na kushauri kuwa rais wa Zanzibar na Maalim Seif wapewe chati maalumu cha shukurani (certificate of appreciation) iliyotiwa saini na wajumbe wote wa baraza wa wawakilishi.

  Kufanyika mabadiliko hayo ya katiba yanafuatia matokeo ya kura ya maoni iliyopigwa julai 31 ambapo asilimia 66.4 waliunga mkono kuwepo kwa mfumo mpya wa serikali ya umoja wa kitaifa na asilimia 33.6 kukataa mfumo huo.

  Wajumbe wengi pamoja na wale ambao katika majimbo yao wananchi walipiga kura ya hapana leo waliungana pamoja kuunga mkono sheria hiyo wakisema kwamba wakati umefika kwa wazanzibari kufanya kazi pamoja na kuweka kando itikadi za kisiasa kama anavyoeleza mwakilishi wa CUF wa jimbo la Tumbe, Ali Mohammed Bakari.

  Wawakilishi hao wamesema ni hatua muafaka kwa Zanzibar kuwa serikali ya umoja wa kitaifa kwa sababu ndio njia pekee ya kumaliza mpasuko wa kisiasa uliodumu tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.

  Rasimu ya sheria ambayo imewasilishwa na waziri wa katiba na utawala bora, Ramadhani Abdallah Shaaban inaainisha serikali ijayo itakavyokuwa ikiwa ni pamoja na kuwa na rais na makamu wawili wa rais na mawaziri ambao watachaguliwa kutokana na uwiano wa kura.

  Rais pamoja na makamu wa pili wa rais watatoka katika chama kitakachoshinda katika uchaguzi wakati makamu wa kwanza wa rais atatoka katika chama kitachoshika nafasi ya pili na baraza la mawaziri litaundwa ndani ya siku 14 baada ya rais kuapishwa.

  Wajumbe wengi wa baraza la wawakilishi walijadili kwa hisia za kuunga mkono huku wakiwa na matarajio makubwa kwa kuijenga Zanzibar mpya. Mwakilishi wa jimbo la Mkanyageni (CUF), Haji Faki Shaali alisema wananchi wa Zanzibar wamechoshwa na migogoro inayotokea kila baada ya uchaguzi na ndio maana wameamua kuunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa.

  “Wananchi wana matumaini makubwa na mfumo huu mpya wa serikali hivyo ni wajibu wetu kupitisha marekebisho haya ya 10 ya katiba ili mfumo huu mpya uweze kufanya kazi, baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba”, alisema Mwakilishi Shaali.

  Kiongozi wa upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Abubakar Khamis Bakari alisema ni jambo la faraja kuona marekebisho ya katiba Zanzibar hayana tafauti na hoja binafsi aliyoiwasilisha barazani hapo na kupitishwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

  Mwakilishi wa kuteuliwa na Rais Asha Bakari Makame alisema kitendo cha kufikiwa maelewano katika ya vyama vya CCM na CUF kinastahili kupongezwa na wananchi wote wa Zanzibar.

  Mwakilishi huyo alisema kwamba viongozi wa kisiasa Zanzibar walijisahau katika suala zima la kutetea maslahi ya wananchi na nchi, kabla ya Mwenyezi Mungu kuwazindua na kuleta maelewano ambayo yamesaidia kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar.

  “Hakuna kitu kizuri kama uzalendo katika nchini, sisi ndio wenyewe nchi hii bahati mbaya viongozi tulijisahau katika kutetea maslahi ya wananchi na nchi”, alisema Mwakilishi huyo.

  Mwakilishi wa kuteuliwa na Rais Juma Duni Haji, alisema serikali ya umoja wa kitaifa itasaidia kukuza maelewano kwa wananchi wa Zanzibar na kuendeleza misingi ya Mapinduzi ya mwaka 1964, kwa kujenga umoja wa kitaifa.

  Aidha, alisema Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha anastahili kupongezwa kwa kuandika historia kubwa Zanzibar yeye na Kiongozi wa Upinzani barazani, Abubakar Khamis Bakar kwa jinsi walivyofanikisha hoja binafsi ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa.

  Alisema mwanzo hoja binafsi iliyotaka kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa ilionekana kama Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na Rais Karume, lakini baadaye iliridhiwa na wajumbe wa Baraza baada ya kuonekana ina maslahi kwa wananchi wote wa Zanzibar.

  Akichangia katika baraza hilo, Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yussuf Himid aliwaeleza wajumbe wa baraza hilo, ili maridhiano yaliyofikiwa yabakie kuwa salama zaidi ni vizuri mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohammed Shein akachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar.

  Alisema kwamba mafanikio yaliyopatikana yalitokana na moyo wa ujasiri wa Rais Karume ingawa baadhi ya wakati alikuwa katika mazingira magumu, lakini hakurudi nyuma hadi alipohakikisha anafikiwa kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar.

  Waziri Mansour alisema kamati ya watu sita ya kusimamia utekelezaji kura ya maoni inapaswa kupewa jina maalum kama zilivyopewa kamati zilizoongozwa na Jaji Kisanga, Shelukindo na Nyalali.

  Alisema itakuwa muafaka kamati hiyo ikapewa jina la Ali, kwa vile iliongozwa na Mwenyekitiwa Baraza la Wawakilishi, Ali Mzee.

  Mwakiishi wa jimbo la Mji Mkongwe, Bi Fatma Abdulhabib Fereji alisema marekebisho hayo ya katiba yana umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Zanzibar na wananchi walioshiriki kura ya maoni na kutia hapana, huko mbele wataunga mkono baada ya kuona faida ya serikali ya umoja wa kitaifa ikishakuanza kufanya kazi zake.

  Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala Bora, Haji Omar Kheri alisema kura ya maoni ni ushahidi kuwa wananchi walio wengi wana hamu ya kuona mabadiliko katika nchi yao na kufungua ukurasa mpya wa maendeleo pamoja na kusahau tafauti zao za muda mrefu.

  Aliishauri Tume ya Uchaguzi Zanzibar kuendeleza mafanikio iliyoyapata katika kusimamia kura ya maoni, ili uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba uweze kwenda kwa amani, huru na uwazi.

  Wajumbe hao walijadili na kuunga mkono kipengele kinachoitambua Zanzibar kuwa ni nchi na kusema kuwa marekebisho hayo yataondosha utata uliokuwepo tangu mwaka juzi kuwa Zanzibar sio nchi.

  Kwa mujibu wa kifungu cha katiba 1 na 2 vinarekebishwa na kuwa “Zanzibar ni nchi ambayo eneo lake la mipaka ni eneo lote la visiwa vya unguja na pemba ambayo kabla ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa jamhuri ya watu wa Zanzibar ….Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda jamhuri ya muungano wa Tanzania.”

  Kipengele hicho 1 na 2 kabla ya mabadiliko haya kinaitambua Zanzibar kuwa ni sehemu tu ya jamhuri ya muungano bila ya kutoa ufafanuzi jambo ambalo lilizusha mjadala mkali baina ya wajumbe wa baraza la wawakilishi na viongozi wa jamhuri ya muungano akiwemo waziri mkuu mizengo panda.

  Chini ya marekebisho mapya ya Katiba wakuu wa mikoa wanafutwa kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, ambapo pia muundo wa serikali utakuwa na Rais, Makamo wa kwanza wa Rais na makamo wa pili wa Rais.
  Nafasi ya Waziri Kiongozi pia inafutwa na shughuli alizokuwa akifanya waziri kiongozi chini ya marekebisho hayo zitasimamiwa na Makamo wa pili wa Rais ambaye atatoka chama kilichoshinda uchaguzi huku Baraza la Mawaziri litaundwa kwa kuzingatia uwiano wa viti ndani ya Baraza la Wawakilishi.

  Serikali ya umoja wa kitaifa inatarajia kuundwa baada ya miaka mingi ya malumbano na chuki za kisiasa ambazo hapo awali ilishindikana kumalizwa katika miafaka mitatu ilisimamiwa chini ya jumuiya ya madola na viongozi wa ndani ya Tanzania kutaka kusuluhisha.
   
Loading...