Stories of Change - 2023 Competition

Ronda Nico

New Member
Jul 28, 2023
2
0
Mtu yeyote akisimama mbele ya mkusanyiko wowote wa Watanzania akatoa kauli ya kwamba, ili kuwe na maenendeleo makubwa na kumfikia kila mtanzania, kunahitajika mabadiliko makubwa katika utawala na uwajibikaji serikalini; hakika hakutakuwa na mjadala.

Ila mjadala utakuwepo, tena mkali; ikitakiwa kuainisha mabadiliko yanayohitajika yatakavyopatikana. Yamkini walio wengi wakataja kupatikana kwa Katiba mpya. Japokuwa kunawezekana kukawa na wengine wengi wakapinga, nitaliangazia hili la Katiba mpya kwa vile ndilo limekuwa kwenye vinywa vya wengi kwa muda mrefu.

Japokuwa naona haja ya kuandika Katiba mpya ya nchi, sikubaliani na dhana ya kwamba Katiba mpya ndiyo muarobani wa matatizo makubwa yanayosababisha tusipate maendeleo kwa kasi, endelevu, na ya kumfikia Mtanzania wa kawaida. Kabla ya kutoa sababu ya kuwa na maoni tofauti, ni muhimu nitaje na kuelezea mambo ninayoyaona kama matatizo makubwa kwa maendeleo ya nchi yetu.

Kimsingi, mambo yanayokwamisha maendeleo ni mawili: Nayo ni udhaifu katika utawala wa nchi, na udhaifu katika uwajibikaji wa watendaji. Mambo haya mawili nimeyagawa kwa minajili ya uchambuzi, lakini kiuhalisia ni mambo yenye uhusiano mkubwa, kama itakavyodhihirika baadaye kwenye makala hii.

Kwanza, nizungumzie udhaifu katika utawala. Udhaifu katika utawala wa Tanzania una taswira kuu mbili: Moja ni katika kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma kwa ujumla; na ya pili, ni kutozingatia utawala wa sheria. Mfano mzuri wa udhaifu katika usimamizi ni ombwe katika usimamizi na uwajibishaji wa wasiotekeleza mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), jambo linalosababisha ufisadi na upotevu mkubwa wa fedha na rasilimali za nchi.

Kuhusu kupuuzia sharia: Imejengeka tabia ya viongozi kufanya mambo kinyume cha sheria zilizopo, hata katika mambo makubwa yanayotishia amani, umoja, na ustawi wa raia. Mfano ni uvamizi wa mifugo wa mashamba wa makusudi unaombatana na kujeruhi na mauaji ya wakulima kuchukuliwa kama migogoro baina ya wafugaji na wakulima na kusuluishwa kisiasa; ilhali ni uhalifu unaoadhibika na ni rahisi kuukomesha kisheria. Matokeo ni wafugaji kuendelea kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima makusudi kwa kile kinachoonekana kuwa kiburi na nguvu ya rushwa, na kuwakosesha wakulima kipato, chakula, usalama wa maisha yao, raha, na amani.

Pili, nizungumzie uwajibikaji. Matatizo katika uwajibikaji, kwa kiwango kikubwa, yanatokana na udhaifu katika utawala. Na huu ndio uhusiano nilioutaja kwenye aya ya tatu. Ni kawaida kwamba usimamizi ukilegalega au usipokuwepo, na uwajibikaji unalegalega, ama kutokuwepo kabisa. Kurejea mfano wa mapendekezo ya CAG, ni dhahiri kunapokuwa hakuna ufuatiliaji na uwajibishaji unaolingana na makosa, kwa vyovyote makosa hayo yatajirudia. Hali inakuwa mbaya zaidi ikiwa kama upotevu wa fedha, ama rasilimali, umehusisha wakubwa.

Mbali na kutowajibishwa, wakati mwingine kutowajibika kunatokana na kutozingatia kanuni, miongozo, na sheria husika. Watendaji wengi hapa nchini wanafanya kazi kimazoea; wengi wao hawana hata maandiko ya kanuni, miongozo, ama sheria kuhusu kazi zao.

Ukiangalia matatizo makuu yanayohusu utawala wa nchi na uwajibikaji hapa Tanzania, utaona kuwa Katiba tuliyo nayo ya 1977 na sheria husika anuai tulizo nazo zinatosha kuwezesha dola kuendesha nchi kwa utawala ulio bora na kusimamia masuala ya uwajibikaji uliotukuka. Hivyo kuwepo kwa matatizo hayo siyo suala la Katiba, na kwa hiyo kupatikana kwa Katiba mpya hakuwezi kukawa muarobaini wa matatizo hayo.

Aidha, tunayo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na taasisi kadhaa za kiserikali na zisizokuwa za kiserikali zinazohusika na utawala bora na uwajibikaji. Isitoshe zimeishafanyika semina na makongamano mengi yanayohusu kuboresha utawala na uwajibikaji. Hakika juhudi zilizokiwishafanywa zikilengalenga kuboresha utawala na uwajibikaji ni nyingi.

Hata hivyo, nionavyo mimi, juhudi zote hizo hazijazaa matunda lengwa. Badala yake kunaonekana kuongezeka kwa rushwa, ufisadi, uhujumu uchumi, mmomonyoko wa maadili na kukithiri kwa wizi; mambo ambayo yanaigharimu nchi fedha nyingi, yanashusha uchumi, yanapunguza ajira, na kuathiri ustawi wa jamii.

Kitakwimu, Tanzania siyo maskini tena. Mwaka 2021 Tanzania iliingizwa kwenye kundi la Kiwango cha Chini cha Uchumi wa Kati duniani; na katika Hotuba ya Bajeti ya 2023/24 serikali imetangaza kuwa uchumi wa Tanzania mwaka 2022 umekua kwa asilimia 5.2, ambayo ni kubwa ukilinganisha ya wastani wa dunia ambao ni 3.2 kwa kipindi hicho. Lakini ukija chini kwa wananchi, hali ni ngumu! Na umaskini unaonekana kuongezeka.

Hali hiyo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliiona wakati anaingia madarakani 2021, na kuelekeza juhudi kubwa na za makusudi kuinua maendeleo ya jamii kwa kuongeza bajeti za huduma za kijamii na shughuli za uchumi zinazowahusu wananchi wa kawaida, lakini hadi sasa mafanikio ni kidogo. Hali hii inatokana na udhaifu katika utawala na uwajibikaji, ama kukosekana kwa utawala bora kimatendo.

Kwa mujibu wa Mwongozo wa Utawala Bora uliochapishwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Policy Forum 2013, utawala bora ni matumizi ya mamlaka ambayo yanakuwa na uwazi, uwajibikaji, ushirikishaji wa watu, ufanisi, tija, uadilifu, usawa, na unaofuata sheria. Hivyo, haya ndiyo malengo ya Tume kama chombo mahsusi cha utawala bora. Na kwa hiyo tungetegemea katika miaka 22 ya kuwepo kwake, ukiongeza na nguvu ya Rais Samia, kungekuwa na mafanikio yanayodhihirika bayana. Kwa maoni yangu, kinachodhihirika ni kuendelea kudhohofu kwa utawala na uwajibikaji.

Ukizingatia juhudi zote zilizowahi kufanyika kuboresha utawala na uwajibikaji, inaonekana dhahiri kwamba kuna jambo la msingi linalokosekana; na hili ndilo nimeita jicho la tatu.

Jicho la tatu, kimsingi, ni mdau wa tatu baina ya masimamizi na mtekelezaji, ama mtoa huduma na mpokea huduma au mteja kwa lengo la kuhakikisha majukumu husika yanatekelezwa ipaswavyo. Hivyo, jicho la tatu linaweza kuwa ofisi, taasisi, utaratibu, ama mfumo wa kuwezesha dola/serikali kujua kama mipango, miradi, majukumu, sharia, ama maelekezo yanatekelezwa ipaswavyo. Mfano, TAMISEMI kuweza kujua kama jukumu la serikali za vijiji na mitaa kuitisha mikutano ya wananchi kila baada ya miezi mitatu linatekelezwa ipaswavyo. Na kunapotokea ukiukwaji, unagundulika kwa wakati, na hatua stahiki zinachukuliwa.

Ni muhimu kuelewa kuwa jicho la tatu ni tofauti na utratibu wa sasa wa ofisi za kero, ama mahusiano. Ofisi yenye dhima ya jicho la tatu ina mawanda mapana kiutendaji na hivyo kuhitaji ofisi kamili zenye wafanyakazi wenye sifa mahsusi na vitendeakazi vya kuweza kufanya ukaguzi wa kiada na dharura, na kupokea malalamiko ya wananchi au wateja, na kuyafanyia kazi kwa wakati. Jicho la tatu ni dhana itakayoleta mageuzi kidogo kwenye mfumo na muundo wa Serikali, lakini manufaa yake yatakuwa makubwa sana kwa Taifa.
 
Back
Top Bottom