Maandamano ni silaha ya wanyonge

Maandamano ni silaha ya wanyonge

Joined
Feb 13, 2011
Posts
37
Reaction score
14
MAANDAMANO ni utaratibu wa kidemokrasia watu kutembea umbali fulani wakiwa na ujumbe wa kuunga mkono au kupinga au kulaani jambo, mfumo, utawala fulani au kudai haki.

Mwaka 1967 watu waliandamana kuunga mkono Azimio la Arusha huku wakiwa na ujumbe wa kulaani unyonyaji, ukabaila na ubepari. Pia, watu walipokosa haki maeneo ya kazi walitumia maandamano kama silaha ya mwisho kudai haki yao.
Maandamano ni njia ya kidemokrasia ya kupinga mfumo dhalimu. Njia hii, haipendwi na watawala hivyo huweka vikwazo kukandamizi. Lakini kokote duniani ambako imetumika, yamesaidia anyone kupata haki na madai halali ya kikatiba na kidemokrasia.
Hii ndiyo sababu tawala nyingi za kidhalimu, kifisadi, kijeuri na kikatili hukataa maandamano. Hata watawala waliosalia madarakani baada ya maandamano, walitekeleza kwa vitendo madai ya waandamanaji.

Maandamano ni silaha ya wanyonge, yanapofanyika watawala huweka vikosi vya usalama ambavyo hutumia nguvu nyingi, kupiga, kutesa, na kuweka watu kizuizini.

Aidha, gharama ya maandamano katika nchi inayoongozwa na serikali dhalimu ni kubwa. Gharama hiyo ni pamoja na vitisho, kujeruhiwa, kushitakiwa, kufungwa na kuuawa.

Waandamanaji hudai haki yao ikiporwa, watawala hujibu kwa vikosi vya usalama kupambana na umma.
Hata hivyo, historia inaonesha katika nchi kadhaa, umma ulifanikiwa kukomesha udhalimu, ufisadi na ukandamizaji. Umma uliona bora kuingia gharama ya vitisho, kuuawa, kubaki vilema au kufungwa gerezani kuliko kuishi maisha chini ya mfumo udhalimu, unyanyasaji, ukatili, uporwaji, wizi na ufisadi milele.

Katika Biblia Takatifu, Nabii Musa aliongoza maandamano kwenda kwa Farao kudai uhuru wa Waisraeli waliokuwa watumwa nchini Misri kwa miaka mia nne. Farao alitumia kila aina ya vitisho na nguvu za majeshi ya wapanda farasi na magari, ilishindikana. Baadaye alikubali kuwapa uhuru Waisraeli wa kwenda kujitawala katika taifa lao.

Mwaka 1789 umma wa taifa la Ufaransa, baada ya kuchoshwa na dhuluma, ukatili, unyanyaswaji chini ya Mfalme Louis, uliingia mitaani na barabarani. Mfalme Louis alitumia vikosi vyake vya usalama kuua, kukamata, kutesa na kuwafunga waandamaji. Nguvu hii haikusadia kukomesha maandamano.

Tarehe 4 julai 1789, maandamano yalikoma baada ya Kasri la Mfalme Louis kuangukia mikononi mwa umma.
Mfalme Louis aliona Ufaransa kama miliki yake binafsi milele yote, kumbe wenye nchi walikuwepo. Baada ya mapinduzi, Ufaransa ilikuwa Jamhuri inayoongozwa na rais aliyechaguliwa na watu na anayewajibika kwa watu.
Mwaka 1947 India ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Waingereza yakiwa ni matokeo ya maandamano yaliyojengwa na kuongozwa na hamasa za fikra za mpigania uhuru Mahatma Gandhi.

Ingawa Gandhi na wenzake walikabiliwa na vifungo na mateso, maandamano ya kudai uhuru hayakukoma mpaka siku ile ukoloni wa Kiingereza ulipokoma.

African National Congress (ANC), chama cha siasa cha Afrika Kusini, ambacho kilianzishwa mwaka 1912, kilifanikiwa kung'oa utawala wa kibaguzi mwaka 1994.
ANC ilitumia njia ya migomo na maandamano. Serikali ya makaburu ilifanya juhudi kubwa ya kuua, kufunga na kuweka kizuizini wapigania uhuru, akiwemo Nelson Mandela aliyekuja kuwa rais wa kwanza mweusi.
Mwaka 1976, wanafunzi walioandamana kupinga ubaguzi katika utoaji elimu, walipigwa risasi, waliuawa lakini maandamano hayakukoma. Mwaka 1994, utawala wa makaburu ulikoma rasmi.

Mwaka 2010, wananchi wa Tunisia waliandamana kupinga rushwa, ukosefu wa ajira, mfumuko wa bei na ukandamizaji wa kisiasa. Maandamano ya takriban wiki nne, kuanzia tarehe 18 Desemba 2010 yalihitimishwa tarehe 14 Januari 2011 kwa Rais Ben Ali kung'olewa madarakani na kulazimika kukimbilia ukimbizini Saudi Arabia.
Julai 2011, maandamano mengine yalitokea nchini Misri ambako watu walimiminika kwenye Uwanja wa Tahrir kupinga ufisadi, rushwa, ukandamizaji, udikteta wa serikali ya Hosni Mubarak na vibaraka wake.

Mubarak aliamuru vikosi vya usalama kuingia mitaani na kuua mamia ya watu. Baada ya kuchoka kufyatua risasi, vikosi viliamua kujiunga na waandamanaji, Mubarak naye alisalimu amri akaondoka madarakani.
Vikosi vya usalama vilivyokuwa na kila aina ya silaha vilishindwa mbele ya umma.

Novemba 2012, umma wa Argentina uliingia mitaani kupinga sera za serikali ya Rais Cristina Fernandez de Kirchner. Watu zaidi ya 700,000 walikusanyika jijini Buenos Aires kupinga ongezeko la uhalifu, mfumuko wa bei na hatua ya serikali kuingilia mambo ya uchumi. Serikali ya Cristina ilikubali kufuata matakwa ya waandamanaji.

Nchini Tamzania, serikali iliyopo madarakani imeonja hasara ya kisiasa ya maandamano ndiyo maana wakubwa wanatumia kila njia kuzuia Chadema wasiandamane.

Kati ya mwaka 2008 na 2010 Chadema walifanya mikutano na maandamano nchi nzima kwa kauli mbiu ya Oparesheni Sangara. Kupitia oparesheni ile Chadema waliitisha maandamano ya kupinga ugumu wa maisha, mfumuko wa bei na ufisadi wa EPA.
Serikali ya CCM ilitumia Jeshi la Polisi kuweka vikwazo ili Chadema washindwe kutimiza malengo yao. CCM walitunga propaganda za ukabila na udini dhidi ya Chadema bila mafanikio.

Maandamano ya 2008-2010 yalionesha tija kwa Chadema na hasara kwa CCM katika uchaguzi wa mwaka 2010. Pamoja na kuchakachua matokeo kutokana na kutokuwepo Tume Huru ya Uchaguzi, kura za aliyekuwa mgombea wa CCM, Rais Jakaya Kikwete zilipungua kwa karibu asilimia 20. Majimbo mengi yaliyokuwa chini ya CCM kabla 2010 yalichukuliwa na Chadema.
Wakati wa uzinduzi wa Bunge la Kumi Novemba 2010, wabunge wa Chadema walisusia Hotuba ya Rais Kikwete, wakatoka nje ya ukumbi kupinga mfumo wa uchaguzi uliomrudisha Kikwete madarakani.

Hatua hiyo iliweka msingi wa kudai katiba mpya. Maandamano ya kudai katiba mpya yaliendelea kuratibiwa. Chadema walikuja na mkakati mpya wa Vuguvugu la Mabadiliko (Movement for Change –M4C) ili kuhamasisha umma kupigania mabadiliko ya kisiasa.
Japokuwa Fredrick Werema, mwanasheria mkuu wa serikali, na Celina Kombani aliyekuwa waziri wa katiba na sheria walidai Tanzania haina haja na katiba mpya, Rais Kikwete alikubaliana na madai ya umma uliokuwa nyuma ya Chadema.

Hivi sasa uongozi wa Rais Kikwete umeshindwa kusimamia mchakato wa katiba. Mchakato unakwenda mrama. Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samwel Sitta amesimamia mabadiliko ya kanuni, kwamba hata aliyesafarini, mitaani anaweza kupiga kurakwa nukushi au e-mail kupitisha Katiba.

Wapinzani kupitia umoja wao wa Ukawa wameitisha maandamano yasiyokuwa na kikomo kushinikiza kusitishwa kwa BMK kutokana na kupoteza mwelekeo na kubaki likifuja fedha za walipa kodi. Vikosi vya usalama vinaandamana nchi nzima kuzuia. Je, watawala wataushinda umma? Tusubiri.
 
Back
Top Bottom