BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,769
- 288,283
Maamuzi haya vyuo vikuu ni hatari kwa taifa
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
ITAKUMBUKWA kuwa Novemba 12, 2008 wanafunzi wa vyuo mbalimbali nchini walisimamishwa masomo kutokana na migomo iliyofanyika katika vyuo hivyo, ambayo wanafunzi walikuwa wakipinga sera ya uchangiaji wakitaka Bodi ya Mikopo iwalipie ada kwa asilimia 100.
Juzi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na cha Sokoine cha Kilimo (SUA) vimetoa orodha ya wanafunzi waliokubaliwa kurudi chuoni huku ikibainika kwamba wengi wameachwa kutokana na kutokidhi masharti waliyopewa.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Makamu Mkuu wa UDSM, anayeshughulikia taaluma, Makenya Maboko, ilisema kati ya wanafunzi 9,000 waliorudisha fomu zilizochambuliwa, ni wanafunzi 3,000 pekee ndio waliokidhi vigezo na kutangaziwa kurudi chuoni.
Ilisema chuo hicho kitafunguliwa Januari 19 mwaka huu na wanafunzi watakaotakiwa kuripoti, ni wale ambao majina yao yamo katika orodha iliyotolewa, kwamba wanafunzi ambao majina yao hayakutajwa katika orodha wajihesabu kuwa hawakufanikiwa na hivyo hawaruhusiwi kuingia katika mazingira ya chuo.
Taarifa hiyo ilisema kuwa wale waliowasilisha fomu za maombi lakini hawakulipa ada ya mwaka 2008/09 wanatakiwa kulipa kiwango wanachodaiwa kupitia benki kabla ya Alhamisi ijayo.
Kwamba kutokana na asilimia kubwa ya fomu kubainika kuwa na dosari, chuo hicho kimetoa muda hadi Alhamisi ijayo, wanafunzi hao wapatao 6,000 wawe wametatua dosari hizo, na orodha ya watakaorekebishwa itatolewa katika tovuti ya chuo Ijumaa ijayo.
Kwa upande wa SUA, taarifa iliyotolewa imewaelekeza wanafunzi wote ambao majina yao yamo katika orodha warejee chuoni hapo kuanzia juzi hadi jana, kwamba wanafunzi ambao majina yao hayataonekana katika orodha, wajue kwamba hawakukidhi masharti ya udahili na hawatatakiwa kuripoti kwa ajili ya masomo.
Kwetu sisi, uamuzi wa uongozi wa vyuo hivyo kuacha kuwarejesha masomoni idadi kubwa ya wanafunzi, kwa kuzingatia kigezo cha ujazaji wa fomu na sharti la ulipaji ada, haupaswi kuungwa mkono na Mtanzania yeyote mwenye kujali haki na mustakabali mwema wa taifa lake, tunasema hivyo tukizingatia yafuatayo: wanafunzi hawa waligoma wakitaka kupewa mikopo ya asilimia 100 ili walipe ada na kugharamia mahitaji yote ya kielimu, hatuoni uhalali wa serikali kukataa au kushindwa kutoa mikopo hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa ina uwezo huo na baada ya kuhitimu, itarejeshwa.
Wanafunzi wengi kushindwa kukidhi vigezo na masharti yaliyowekwa kwenye fomu za kuomba kurejereshwa chuoni ni kielelezo cha wazi wazi kuwa wazazi wao hawana uwezo huo na ndio maana waligoma wakiitaka serikali itoe mikopo ya asilimia 100 ili maskini hao ambao ndio wengi waweze kusoma.
Hatua ya vyuo hivyo kuamua tu kuwachukua wanafunzi wachache walioweza kukidhi vigezo na masharti yaliyowekwa kwenye fomu hizo, inatoa tafsiri ya kibaguzi kati ya watoto wa maskini walioshindwa kukidhi masharti hayo ikiwemo sharti la kulipia ada, na watoto wa familia zinazojiweza ambao wamemudu masharti hayo.
Kwanini tunazidi kutengeneza matabaka katika jamii? Serikali inapata faida gani kwa kuacha wanafunzi hao warudi nyumbani huku ikijua fika kuwa taifa linakabiliwa na upungufu mkubwa wa madaktari, walimu na wataalamu wengine?
Ni rai yetu kwa serikali na wadau wote wa elimu nchini, kuingilia kati kwa mazungumzo ili wanafunzi hao waweze kurejea chuoni, vinginevyo maamuzi haya ya vyuo vikuu ni hatari mno kwa amani na mustakabali wa maendeleo ya taifa letu.