Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
TAARIFA zimevuja. Wanasiasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanatajwa kushinikiza Jeshi la Polisi kumkamata Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF),
Si Maalim Seif pekee, viongozi wengine wa chama hicho wanaoundiwa mkakati wa kukamatwa ni pamoja na Mansoor Yussuf Himid na Nohamed Ahmed Sultan kwa sababu za kisiasa.
Taarifa hizi zinathibitishwa na Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Zanzibar ambaye amesema;
“Tunazo taarifa kwamba, kuna wanasiasa wameliagiza Jeshi la Polisi kuandaa mashtaka kwa ajili ya kumshitaki Maalim Seif Sharif Hamad kwamba alipokuwa Pemba alifanya maandamano bila ya kibali wakati hakukuwa na maandamano yoyote.”
Mazrui amesema hayo leo wakati wa Uzinduzi wa Taarifa ya Uvunjwaji wa Haki za Binadamu Zanzibar kwa mwaka 2015/2016 uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
“Viongozi hao wamepangiwa kukamatwa na kuletwa katika magereza ya Tanzania Bara kwa lengo la kuwanyamazisha Wazanzibar ili wasipaze sauti zao kupinga utawala wa kidkteta uliowekwa madarakani kwa nguvu za dola kinyume na matakwa ya kidemokrasia ya wananchi wa Zanzibar,” amesema.
Akizungumzia uzinduzi wa Taarifa ya Uvunjwaji wa Haki za Binadamu Zanzibar 2015/2016 amesema, CUF inajiandaa kuchukua hatua kutokana na uharibifu uliofanywa na Serikali ya CCM visiwani humo.
Mazrui akimwakilisha Maalim Seif kwenye uzinduzi wa ripoti hiyo amesema, nakala ya ripoti hiyo pia watamkabidhi Rais John Magufuli kwa lengo la kujua kilichofanyika na kinachofanyika Zanzibar.
“Baada ya hatua ya leo ya uzinduzi wa taarifa hii, CUF kimejiandaa kuchukua hatua ikiwemo ya kumuandikia rasmi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh, Dk. John Magufuli na kumkabidhi nakala ya taarifa hii ili ajue kinachofanyika nchini na hasa akiwa Amiri Jeshi Mkuu,” amesema Mazrui.
Hatua nyingine zitakazochukuliwa na CUF ni pamoja na kuiwasilisha taarifa hiyo pamoja na vielelezo vyote katika Jumuiya, Taasisi za Mashirika ya Kimataifa yanayotetea haki za binadamu ulimwenguni ili kuchukua hatua zao.
“Pia tutaiwasilisha taarifa pamoja na vielelezo vyote katika Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora hapa nchini ambayo hata katika mkutano wa Geneva ilitambuliwa uwepo wake,” amesema na kuongeza.
“Na katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) pamoja na taasisi nyingine zinazoshughulikia masuala ya haki za binadamu hapa nchini.”
Mazrui amesema “ Hatua nyingine itakayofuatwa ni kufungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania dhidi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kuhusiana na matendo yanayohusisha Jeshi la Polisi visiwani Zanzibar.
Hatua nyingine itakayochukuliwa ni CUF kukamilisha taratibu zitakazoiwezesha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu(ICC) kuanzisha uchunguzi dhidi ya watu wenye dhama mbalimbali ambao wamehusika kuchochea, kutoa au kusimamia maagizo yaliyoepelekea makosa dhidi ya ubinadamu na makosa yaliyoilenga jamii ya watu fulani.
Source: Mwanahalisi