Maafisa Halmashauri Mbeya Wapopolewa Mawe-Kisa ni Ushuru

wikolo

JF-Expert Member
Oct 19, 2010
800
270
BAADHI ya maafisa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini, wamenusurika kufa baada ya kupopolewa mawe na wakulima wa kijiji cha Igoma wilayani humo.


Habari kutoka eneo la tukio zimesema kuwa maafisa hao walifika katika eneo hilo na kuwataka wakulima na wafanyabiashara wa zao la viazi kulipa ushuru wa sh 1,000 kwa kila gunia hali iliyoleta mtafaruku kati yao.
Baada ya kulumbana kwa muda mrefu, ndipo wakajitokeza vijana na kuanzisha vurumai kati yao na maafisa hao kwa madai kuwa serikali imekuwa ikijitokeza kutoza ushuru wa mazao lakini wakati wa kuhudumia mashamba yao inakuwa mafichoni.


Maafisa hao baada ya kuona wanazidiwa waliamua kuingia katika gari lao lenye namba za usajili STK 864 na kuanza kukimbia huku wakulima hao wakiendelea kuwavurumishia mawe. Baada ya hapo maafisa hao wakiwa wamejeruhiwa, walifika katika kituo cha polisi cha kati na kutoa maelezo huku gari yao ikiwa imevunjwa vioo vyote.


Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Andason Kabenga, alisema kuwa alipata taarifa hiyo akiwa katika shughuli za kukagua maendeleo na Diwani wa Kata ya Halungu aliyemtaja kwa jina la Hashim.
“Ni kweli nimepata taarifa hiyo ya kuumizwa watendaji wetu lakini ushuru waliokuwa wanadai ushuru halali maana ulipitishwa katika Baraza la Madiwani,” alisema Kabenga.


Tanzania Daima lilifika katika kituo kikuu cha polisi mkoani hapa na kulikuta gari hilo likiwa limeegeshwa nje ya kituo huku maafisa hao wakiwa ndani wakitoa maelezo.


Sakata hilo limetokea baada ya wiki moja wakulima wa eneo la Namba One Wilaya ya Rungwe kufunga barabara na kuchoma moto lami, wakipinga ushuru wa namna hiyo mpaka pale Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, alipoingilia kati na kusitisha ushuru huo.

Source: Tanzania Daima
 
Back
Top Bottom