The Bourne
JF-Expert Member
- Aug 24, 2017
- 1,077
- 1,322
MBWEMBWE ZA KEKI KUUTAMBIA MKATE
Popote pale ninapousikia wimbo "Tumeagizwa Upendo" wa mtaalamu wa Bongo Fleva, Nuruelly, akili yangu huwa inahama. Hupata hisia zenye kuchoma fikra na kukumbuka unyenyekevu umpasao kila binadamu.
Kiitikio: Hivi mimi ni kama nani, niseme naringa. Chuki uadui kwa wenzangu mi', na nimeumbwa. Tumeagizwa upendo. Tumeagizwa upendo.
Ndani ya wimbo Nuruelly ameyagusa maudhui inavyotakiwa. Wimbo mzuri sana. Hata hivyo mimi naomba nijihoji kupitia kiitikio: "Hivi mimi ni kama nani mpaka nianze kujitapa? Mimi ni nani mpaka niringe? Mwisho kabisa, nimeumbwa sawa na binadamu mwingine yeyote.
Nakuhoji na wewe; hivi wewe ni nani mpaka ujione wewe ndiye wewe na hakuna mwingine mfano wako? Mikogo ya nini ikiwa wewe ni kiumbe usiye na uhakika na kesho yako? Mwisho kabisa umeumbwa sawa na wengine.
Unyenyekevu wa kibinadamu unakumbusha pia kutolamba miguu ya binadamu wengine. Usijipandishe juu ya wengine, wala usijishushe mpaka kuwa chini ya wengine. Jinyenyekeze sawa na wengine. Katika kundi la wenye kujikweza, hakikisha unadhibiti unyenyekevu.
Karne ya 21 sasa, dunia ikiwa imeshahudia kuja na kuondoka kwa watu walioitikisa kwa ufahari wa hali ya juu, wewe nani leo mpaka uwe na jipya la tambo kwenye ulimwengu? Hao waliotamba mwisho wao ulikuwa upi?
Kuishi Karne ya 21, maana yake miaka zaidi ya 2,000 imepita, miezi zaidi ya 24,000 imekatika, wiki zaidi ya 104,000 zimeyoyoma, siku takriban 732,000 zimeondoka, saa zipatazo 17.6 milioni nimesomwa.
Je, kwa nyakati zote hizo ambazo zimepita, binadamu yupi mpya wa kutikisa na asemwe hajawahi kutokea mfano wake? Na hao waliopata kutikisa na kuacha historia ya kukumbukwa mpaka leo, wao waliishia wapi?
WAJIVUNIA UTAWALA?
Ni kichekesho tu ukijisema wewe ni mtawala mwenye nguvu; tutakuuliza umepata kufunuliwa habari za Alexander III wa Macedon? Huyo ambaye dunia inamfahamu kwa uzuri zaidi kupitia jina la Alexander The Great.
Okoba 336 Kabla ya Kalenda, Mfalme wa Macedon, Philip II, alikuwa mwenye furaha sana. Ilikuwa siku ya harusi kati ya binti yake, Cleopatra wa Macedon na Mfalme wa Epirus, Alexander I.
Phillip II na Alexander I walikuwa marafiki wakubwa. Sasa katika kunogesha urafiki wao, Phillip II aliamua ampe Alexander I bintiye amuoe.
Akiwa kwenye mji wa Aegae (sasa unaitwa Vergina), lilipokuwa kasri la Mfalme wa Macedon, Philip II akiwa hana ulinzi, mmoja wa walinzi wake, Pausanias wa Orestis, alimshambulia na kumuua. Ni hapohapo mtoto wa Philip II, Alexander III wa Macedon (Alexander The Great), alitawazwa kuwa Mfalme wa Macedon.
Baada ya Alexander The Great kusimikwa ufalme wa Macedon, alitikisa ulimwengu na kuacha historia ya kipekee. Alexander The Great akawa mwamba wa vita usioshindwa. Alishinda kila vita. Alitanua dola ya Macedon (Ugiriki ya Kale), akafika Afrika na Asia.
The Great alifika Afrika, akaitawala Misri, akaitwa Mfalme wa Misri (Pharaoh of Egypt), alishinda vita ya Gaugamela na kuiweka sehemu ya Bara la Asia chini ya himaya yake, akatambuliwa kuwa Mfalme wa Asia (Lord of Asia).
Endelea na ukuu wa The Great; aliitawala Persia ambayo sasa ndiyo Iran. Taifa la Kiislam ambalo tangu kupinduliwa kwa Mfalme (Shahanshah) Mohammad Reza Pahlavi, humtambua Ayatollah Ruhollah Khomeini kuwa Baba wa Taifa.
Unaweza kupata picha The Great alikuwa na nguvu kubwa kiasi gani. Kishindo chake kiliilazimisha sehemu kubwa ya dunia imtii na kuwa chini ya himaya yake. Aliyafikia maeneo mengi na kujitangaza Mfalme Kabla ya Ujio ya Yesu (BC). Je, Alexander The Great aliishia wapi? Alikatika ghafla akiwa na umri wa miaka 33 tu.
JEURI YA UTAJIRI?
Ukija na majigambo ya mali nitakupa simulizi ya Mfalme (Mansa) wa Mali, aliyeishi kati ya mwaka 1280-1337, mwenye kuitwa Musa Keita I, jina maarufu zaidi ni Mansa Musa I.
Mwaka 2012, gazeti la Independent la Uingereza, lilichapisha ripoti ya matajiri wa muda wote ulimwenguni kama utafiti ulivyofanywa na mtandao wa kufuatilia mali na utajiri wa watu mashuhuri ulimwenguni, Celebrity Net Worth na kubainisha kuwa Mansa Musa I, utajiri wake ulifikia dola 400 bilioni.
Ukizibadili fedha hizo kwa sarafu ya sasa, unapata Sh900 trilioni. Na hapo ndiyo walimpunguzia ili akaribiane na akina John Rockefeller. Swali; Mansa Musa I na utajiri wote huo ambao haujawahi kufikiwa na binadamu mwingine yeyote yule aliishia wapi?
Mansa Musa I na utajiri wake wote, aliishi miaka 57 tu. Muongo wa tisa na 10 Karne ya 13 kisha akafikwa na mauti akiwa mwaka wa saba, muongo wa nne, Karne ya 14. Ni hapo unakumbuka maneno ya Nuruelly; "Hivi mimi ni kama nani, niseme naringa."
Mansa Musa I alikuwa tajiri, vilevile mtawala. Aliishi maisha aliyotaka. Je, alifikia wapi? Ni hapo palipo na ukumbusho kuwa kila binadamu ameumbwa. Utajiri, utawala, vipaji, ubora wa muonekano, nguvu na tofauti ya misuli kwa binadamu ni nakshi za dunia lakini binadamu ni yuleyule. Binadamu ameumbwa kwa namna moja.
Mfalme wa mwisho wa Urusi, Nicholas II (Tsar Nicholas II), alikuwa tajiri mkubwa kati ya matajiri wa kihistoria ulimwenguni. Alinyongwa na familia yake yote mwaka 1918 akiwa na umri wa miaka 50. Fedha na mamlaka havikumfaa chochote.
Alikuwepo Mfalme Osman Ali Khan, Asaf Jah VII katika dola iliyoitwa Nizam ya Hyderabad, India. Hata aliponyang'anywa ufalme alibaki kuwa binadamu tajiri zaidi chini ya jua katika nusu ya kwanza ya Karne ya 20. Yupo wapi?
Walichanua sana mabilionea wa sekta ya viwanda ulimwenguni, John Rockefeller na Andrew Carnegie. Dunia nzima ikawatazama wao. Muda ulipofika walizimika mithili ya mshumaa.
Haujapata kutokea duniani ukoo wenye utajiri mkubwa kama Familia ya Rothschild. Kuanzia London, Uingereza, Frankfurt na Vienna, Ujerumani na Napoli, Italia, ukoo huo ulitikisa kwa uwekezaji mkubwa. Karne za 18 na 19, kulikuwa hakuna tajiri kama Familia ya Rothschild. Familia hiyo ipo wapi?
Ukiijua Familia ya Rothschild na jinsi ilivyopotea, utaelewa kwa nini Rutha Maximilian Bushoke aliimba "Dunia Njia", na akapaza sauti kwa hisia kali:
"Wanadhani Mungu anabagua tajiri na fukara, yeye hana kubagua wote wake. Kwa Mungu wote mwendawazimu na timamu, yeye hana kubagua wote wake."
UKWELI DHAHIRI
Haya maisha ni safari ndefu sana lakini binadamu ni kiumbe mwenye pumzi fupi mno. Hata hivyo, kwa hiyo pumzi fupi bado binadamu hutamba utadhani ataondoka na dunia, wakati ataondoka yeye na dunia itabaki.
Binadamu ni bidhaa isiyodumu. Maarifa ya binadamu si ya milele. Binadamu atapenda kuishi lakini miaka ikisogea na nguvu zikiisha anageuka kituko. Pamoja na ukweli huo dhahiri, bado binadamu hakubaliani nao.
Mfanye Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe kuwa mfano wa karibu. Mwaka 1980 (miaka 37 iliyopita), akiwa na umri wa miaka 56, alikuwa imara, mwenye nguvu zake. Akachaguliwa kuwa Waziri Mkuu, akiwa ndiye mtendaji mkuu wa Serikali ya Zimbabwe (key figure).
Miaka saba baadaye, yaani mwaka 1987, Mugabe akiwa na umri wa miaka 63, aliongoza mabadiliko ya Katiba, akamuweka benchi aliyekuwa Rais (figure head), Canaan Banana, hivyo akawa Rais mwenye kofia za ukuu wa Serikali, ukuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu.
Miaka imeenda, Mugabe ana umri wa miaka 93 sasa, na kila mtu ni shuhuda kwamba analazimisha uongozi wakati umri umeshamtupa mkono. Huu ni mfano dhahiri kuwa binadamu si bidhaa ya kudumu. Aweza kukawizwa duniani lakini kamwe haachwi na nguvu zake.
Unapopata ufunuo wa mambo hayo, ndipo unabaini ni kwa nini maisha ya binadamu hayajawahi kuwa na 'guarantee'. Hakuna binadamu ambaye alipozaliwa, wazazi wake walipewa karatasi ya 'warranty', kwamba ataishi zaidi ya miaka ambayo amehakikishiwa.
Shangaa binadamu alivyo wa ajabu; akiwa hajahakikishiwa umri wa uhai wake, analala bila kujua kama ataamka, atoka nyumbani asubuhi pasipo kuwa na uhakika wa kurejea salama, lakini vishindo vyake ni vingi utadhani maisha yake aliyakatia bima kwa malaika mtoa roho.
Hapa naomba nikuguse kwa hisia; nilimuona nyota wa Kwaito Afrika Kusini, Mduduzi Tshabalala 'Mandoza' akiwa kwenye kiwango chake bora kabisa. Nilimshuhudia akitamba jukwaani kutokana na nishati za kutosha alizokuwa nazo.
Ungependa kumuona Mandoza jukwaani. Aliiweza sanaa na alipenda kazi yake. Aliujua uwezo wake na alitumia nguvu zake kufanya kile kitu anachokipenda. Aliuza albamu zake na alijaza watu kwenye maonesho yake. Kila aliyehudhuria maonesho ya Mandoza, aliondoka ameridhika.
Kwaito ilivyo na mdundo mzito, basi ungefurahi kumuona Mandoza akiwajibika jukwaani. Akiimba moja kwa moja (live) na kucheza kwa kujitikisa akitumia nguvu nyingi. Kwa ile mitembeo yake jukwaani, unampatia picha kuwa alijiamini kwa afya nzuri aliyokuwa nayo. Afya ikiwa haina shida humfanya mwenye nayo ajidai mno.
MANDOZA ALIPONILIZA
Ilikuwa Septemba 10, 2016. Shirika la Utangazaji Afrika Kusini (SABC), lilifanya onesho ambalo liliitwa Tamasha la Shukurani (SABC Thank You Concert).
Msingi wa tamasha hilo ulikuwa SABC kusherehekea na wanamuziki, pamoja na wasanii wa nyumbani kwa jumla, ukuzaji wa muziki na sanaa ya Afrika Kusini kwa upana wake, kupitia mpango wao wa kutoa kipaumbele kwa maudhui ya ndani.
Wakati wa maandalizi ya tamasha hilo, ilikuwa ikifahamika kuwa Mandoza ni mgonjwa. Alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya Kansa ya Kichwa na Shingo, athari ikiwa kwenye sehemu ya koo (pharyngeal cancer). Zaidi ilitaarifiwa Mandoza alipoteza uwezo wa kuona.
Tamasha lilifanyika Uwanja wa Orlando, Soweto, Johannesburg. Mandoza hakutarajiwa kuwemo kwenye onesho achilia mbali kutumbuiza. Siku ilipowadia, Mandoza alihudhuria na kumfurahisha kila mtu, maana ilidhaniwa yupo kitandani.
Hata hivyo, wakati wa kutumbuiza mwishoni iligeuka simanzi. Mandoza hakuwa yule. Kwanza alimfurahisha kila mtu aliposema: "Leo nitatumbuiza hapa kwa shoo kali kuthibitisha Shetani ni muongo." Watu walishangilia lakini mwisho aliwaumiza.
Mandoza alipanda jukwaani na kundi kubwa, wawili wakiwa kuhakikisha usalama wake, maana hakuwa akiona. Alijitahidi kuimba wimbo mmoja akisaidiwa na watu aliopanda nao jukwaani, koo likawa linakataa. Wimbo uliofuata uliimbwa na watu wake, yeye akawa anaitikia kwa unyonge.
Ilikuwa siku ya maumivu makubwa kumuona shujaa wa muziki wa Kwaito aliyezoea kufanya makubwa jukwaani akishindwa kabisa kufanya kile anachokipenda. Hilo likawa onesho la mwisho kwa Mandoza na wiki moja baadaye, yaani Septemba 18, 2016, Mandoza alifariki dunia.
Huyo ndiye binadamu jinsi anavyoweza kuondoka akipukutika kama Mandoza au ghafla kama Papa Wemba, aliyekatikia jukwaani kwenye tamasha la muziki la Femue, Abidjan, Ivory Coast, Aprili 24, 2016.
Ndiye binadamu ambaye anaweza kufikwa na mauti kipindi anajiona ni kijana sana mwenye afya njema kama mchezaji wa kimataifa wa Cameroon, Marc-Vivien Foe aliyefariki dunia uwanjani, Juni 26, 2003, bila kuguswa na mtu yeyote, akiwa na umri wa miaka 28.
Foe alikuwa na timu yake ya Taifa, Cameroon katika michuano ya Kombe la Mabara. Alicheza dhidi ya Brazil na Uturuki na kushinda, alipumzishwa dhidi ya Marekani maana Cameroon ilikuwa imeshafuzu.
Katika mechi ya nusu fainali, Uwanja wa Gerland, Lyon, Cameroon ikicheza dhidi ya Colombia, mnamo dakika ya 72, katikati ya dimba, bila kuwa na mchezaji mwingine karibu, Foe alianguka na kufariki dunia. Ni sawa tu na Mcameroon Cheick Tiote aliyefariki ghafla mazoezini, Beijing, China, Juni 5, mwaka huu.
Ni binadamu na mwisho wake. Anaweza kufia kwenye daladala kama mwanamuziki wa Msondo, Joseph Maina, Februari 17, 2009, au vifo vyao vikawa utata kama Steven Kanumba na Albert Mangweha 'Ngwair'.
Anaweza akafia kufuani mapenzini au katikati ya ibada. Roho inaweza kumtoka akiwa shereheni au msibani. Anakufa anapokuwa kwenye mwendo, anapokaa au anapolala usingizini. Muhimu kukumbuka ni kuwa maisha ya binadamu hayana guarantee.
Ni kichekesho sasa kwa mtu ambaye hana warranty na maisha yake, anakuwa mjivuni, mwenye maringo, tambo nyingi na kuwaonea wengine, wakati inawezekana asubuhi ikifika akawa ameshaitika wito wa Mungu au akawa kitandani akiwa hajiwezi, akisubiri kugeuzwa.
KEKI KUUTAMBIA MKATE
Michael Schumacher ni bingwa mara saba wa mbio za magari, Formula 1. Aliingia mchezoni mwaka 1991 akiwa na umri wa miaka 22 na ilipopita miaka mitatu (1994), akawa bingwa. Kuanzia hapo aliendelea kuwa mtawala katika mbio za Langalanga.
Schumacher akawa mwenye kupanda kwa mafanikio. Alitisha kwenye mashindano Formula 1 na alinyoosha kwa kipato. Aliwafunika kwa ingizo la fedha si waendesha magari wenzake tu, bali wanamichezo wote, maana ulifika wakati alitambuliwa kuwa mwanamichezo anayelipwa zaidi.
Mwaka 2010, jarida la takwimu na machapisho ya kifedha na kiuchumi ulimwenguni, Forbes lilimtangaza Schumacher kuwa na utajiri unaofikia Pauni za Uingereza 515 milioni, sawa na Sh1.5 trilioni kwa fedha ya Tanzania katika sarafu ya sasa.
Kuanzia mwaka 2010 mpaka 2013, alikuwa anaingiza kwa mwaka pauni 30 milioni. Pauni 21 milioni ukiwa ni mshahara wake katika timu ya Mercedes na pauni 9 milioni ni fedha za mikataba ya matangazo. Pauni 30 milioni ni Sh89 bilioni (hiyo ni fedha ya mwaka).
Ukihesabu kiasi hicho cha fedha za mwaka ni kuwa Schumacher alikuwa anaingiza wastani wa Sh7.4 bilioni kila mwezi, Sh1.8 bilioni kila wiki, sawa Sh265 milioni kila siku. Tafakari mapato hayo na utajiri wa mtu huyo.
Unauliza ufahari wa kimaisha kwa Schumacher? Ni mtu wa magari, kwa hiyo anamiliki magari ya kifahari daraja la kwanza duniani. Tena hakuyanunua kwa pesa, isipokuwa yeye ndiye alilipwa kuendesha magari hayo, kwani Schumacher kuendesha aina yoyote ya gari ni tangazo tosha.
Schumacher kuwa na magari mengi na ya kifahari ni sawa na bishoo wa Sinza kuwa na nguo nyingi na viatu. Kutoka Mercedes Benz mpaka Bugatti EB110, Ferrari 575M, FXX mpaka Kenzo, Maserati Spyder hadi Alfa Romeo 159.
Majumba ya kifahari, anza kukitambua kisiwa binafsi cha Schumacher kilichopo Dubai, kisha elekea kwenye 'villa' yake ya maana pembezoni ya Ziwa Geneva, Uswis. Ukitaja orodha ya watu ambao wameonja nusu pepo wakiwa duniani, tafadhali sana, utapata dhambi usipomuweka Schumacher.
Pamoja na kuionja nusu ya pepo duniani, Desemba 29, 2013, siku mbili kabla ya kuuona mwaka 2014, kipindi ambacho Forbes walitoka kumtangaza kwa mara nyingine kuwa na utajiri wa dola 800 milioni (Sh1.7 trilioni), Schumacher alipata ajali mbaya iliyobadili maisha yake.
Schumacher akiwa na mtoto wake wa kiume, Mick mwenye umri wa miaka 17 sasa, wakijiburudisha kwa mchezo wa kuserereka kwenye theruji (Skiing), Meribel, Tarentaise, French Alps, Ufaransa, alipita eneo lisilo salama na kuanguka kisha kukita kichwa kwenye barafu.
Jinsi alivyoanguka, uhai wake leo ni kwa sababu alivaa kofia ngumu (helmet), vinginevyo wataalam wanasema angekufa palepale eneo la tukio. Hata hivyo, ukuu wake katika Formula 1 uliishia hapo, maana sasa hajiwezi.
Schumacher wa leo amepooza. Utajiri wake wote haujafanikisha kumrejeshea utimamu wake wa kiafya. Alitibiwa na madaktari bingwa wa dunia, hospitali yenye hadhi namba moja duniani, lakini imekuwa vigumu kupona. Schumacher amekuwa wa kufanyiwa kila kitu.
Mapito kama ya Schumacher husaidia kupanua ubongo na kukuza tafakuri, kwamba binadamu ni mmoja isipokuwa hudanganywa na vikolombwezo wa juu, mithili ya keki na mkate, wakati vyote ni ngano na huokwa kwa moto. Basi kwa nakshi za nyongeza husababisha keki kuutambia mkate.
Ajali ya Schumacher na hali yake ya sasa itoshe kukumbusha kuwa hakuna binadamu asiye binadamu wala hakuna binadamu zaidi ya binadamu. Tambo za mamlaka, vyeo, mali, umaarufu, elimu, vipaji ni nyongeza tu kama keki kwa mkate.
LAZIMA TUELEWANE
Malkia Elizabeth II alikuwa binti mrembo sana. Alikuwa mtoto na kijana mwenye matumaini makubwa. Maisha yake yote hajawahi kuijua shida. Alipokuwa na umri wa miaka 26 tu, akatawazwa kuwa binadamu mwenye nguvu kuliko yeyote yule ulimwenguni.
Ndiyo, mwaka 1952, Malkia Elizabeth II alitawazwa kuwa Malkia wa Uingereza, nafasi ambayo ilimpa hadhi ya Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa Uingereza. Kumbuka alikuwa na umri wa miaka 26 tu.
Mwaka 1947, Prince Philip, Duke wa Edinburgh, akiwa kijana mzuri, maridadi kweli, umri wake ukiwa miaka 26, alimuoa Malkia Elizabeth II aliyekuwa na umri wa miaka 21. Miaka mitano baadaye Elizabeth II akasimikwa Umalkia.
Kwa cheo chake, Malkia Elizabeth II mpaka sasa ni Malkia wa Canada, New Zealand, Australia, Jamaica, Barbados, The Bahamas, Grenada, Papua New Guinea, Visiwa vya Solomon, Tuvalu, St Lucia, St Vincent and Grenadines, Belize, Antigua and Barbuda, St Kitts and Nevis.
Alishakuwa Malkia wa Tanganyika (Tanzania Bara) kabla haijajitangaza kuwa jamhuri, vilevile Pakistan, Afrika Kusini, Ghana, Nigeria, Kenya, Malawi, Gambia, Trinidad and Tobago, Ceylon, Sierra Leone, Uganda, Mauritius, Malta, Guyana na Fiji.
Tafsiri hapo ni kuwa ingekuwa vyeo, mamlaka na fedha vinafanya binadamu asizeeke, Malkia Elizabeth II angedumu kijana. Alipo hana presha, maana Serikali ya Uingereza inaongozwa na Waziri Mkuu lakini yeye ana mamlaka yasiyohojiwa. Ndiye binadamu anayetamkwa kuwa juu ya Katiba ya nchi yake.
Hata hivyo, Malkia Elizabeth II mwenye umri wa miaka 91 sasa, amechoka mno. Mume wake, Duke wa Edinburgh, ambaye ndiye mshauri wake mkuu, ameshaomba kupumzika majukumu ya kumsaidia Malkia kwenye uso wa umma, maana kachoka. Duke wa Edinburgh ana umri wa miaka 96 sasa.
Malkia Elizabeth II na Duke wa Edinburgh wanapozeeka sasa na kufilisika nguvu pamoja na utimamu wa kiafya, pamoja na maisha ya raha, yasiyo na presha waliyoishi miaka yao yote, ikukumbushe kwamba hakuna binadamu asiye binadamu wala hakuna binadamu zaidi ya binadamu.
Duke wa Edinburgh siye yule mtema cheche hadharani kwa kiburi kuwa ni mume wa Malkia. Amechoka. Pengine hata Malkia Elizabeth II kama si kuzuiwa na mila za cheo chake, angejiuzulu Umalkia ili apumzike.
Watu wanapenda sana simu za iPhone, kompyuta za Apple, wanatumia iPads, iPods, wananunua na kupakua nyimbo iTunes. Nawakumbusha kuwa mwenye navyo vyote hivyo, Steve Jobs, alifariki dunia Oktoba 5, 2011 kwa maradhi ya kansa ya tumbo (pancreatic cancer).
Hayo ndiyo mambo ambayo humshangaa binadamu anapojiona bora kwa sababu ya vitu na ufahari wa dunia. Wanasahau kuwa dunia ni njia. Tambo za binadamu kwa binadamu mwenzake, huzifananisha na zile za keki kwa mkate. Hakuna binadamu asiye binadamu. Hakuna binadamu zaidi ya binadamu.
Mkate na keki vyote asili yao ni moja na mwisho wa vyote ni kuliwa na visipoliwa huoza.
Ndimi Luqman MALOTO