LUQMAN MALOTO: JPM ndio mwalimu sahihi wa Mbowe na Zitto

RUSTEM PASHA

JF-Expert Member
Jan 26, 2016
4,671
11,279
JPM NDIYE MWALIMU SAHIHI WA MBOWE, ZITTO

NA LUQMAN MALOTO

KATIKATI ya Karne ya 20, aliyekuwa Kamanda wa Vikosi vya Umoja wa Mataifa (UN), Jenerali Douglas MacArthur, alipendekeza kwa Serikali ya Marekani, kuendeleza uchochezi kwenye Vita ya Korea na China kama njia muhimu ya kuutokomeza Ukomunisti.

Hata hivyo, mbele ya jopo la wanadhimu wa majeshi ya Marekani, katika mkutano ambao ulihudhuriwa pia na aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo, Harry Truman, aliyekuwa kamanda Nyota-5 wa Jeshi la Marekani, hayati Omar Nelson Bradley, alipingana na wazo hilo la kuchochea Vita ya Korea na China.

Bradley alisema kuwa uchochezi huo wa vita ya China na Korea ni “wrong war, at the wrong place, at the wrong time, and with the wrong enemy.”

Kiswahili: Vita batili, katika eneo batili, katika muda batili, na dhidi ya adui batili.

Kwamba nyakati hizo, Marekani kama baba wa ubepari, ilipaswa kujielekeza kupambana na Umoja wa Dola ya Kisovieti (USSR). Kujiingiza kwa Wachina na Wakorea, ilikuwa ni kupoteza rasilimali fedha, muda na watu, tena zaidi mafanikio yasingeonekana.
Si kwamba China na Korea hawakuwa maadui kwa Marekani, hapana, ila ni maadui wadogo. Katika vita unapaswa kuangalia mshindani wako hasa ni nani na kujiondoa kwenye kupambana na maadui wadogowadogo.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kwa muda mrefu walipigana vita batili, katika eneo batili, katika muda batili na dhidi ya adui batili. Walinyukana wao kwa wao kwelikweli. Walishindwa kutambua kuwa upo umuhimu wa kushirikiana dhidi ya adui yao. Kwamba wao wote ni wapinzani, kwa hiyo wanatakiwa kulenga shabaha zao kwa mtawala.

Wakapigana vita wao kwa wao kutafuta ukuu wa upinzani. Wakasahau kuwa upinzani wenye nguvu ndiyo unaweza kuiteteresha serikali. Hujuma na kuhujumiana wao kwa wao, mashambulizi na kushambuliana wenyewe kwa wenyewe ni kuufanya upinzani upoteze nguvu ya kutosha.
Watu wenye kuchangia adui huwa hawapigani wenyewe, bali wanajielekeza kwa adui. Hata kama hakuna kushirikiana lakini ukiwa Mashariki na wewe Magharibi halafu adui akiwa katikati, hapo ni kurusha mishale tu mpaka adui anachanganyikiwa.

Mshale ukimgonga kutoka Mashariki, akitimua mbio kuelekea Mashariki, mshale mwingine unamchoma makalioni kutokea Magharibi. Anachanganyikiwa aende wapi? Mwisho adui anaishiwa nguvu.Hii ndiyo sababu mara nyingi vyama tawala hutumia mbinu nyingi, ikiwemo za kijasusi au kimabavu ili wapinzani wasiwe imara. Vyama tawala huwa vinapenda kuwepo na nafasi (gape) kubwa ya kiushindani kati yao na wapinzani. Mshikamano wa upinzani huwa na athari kubwa kwa nchi, na huwafanya watawala wapepesuke.

Kwa siasa za Afrika ni rahisi mno kusikia wapinzani wenye nguvu wakishutumiana kwa usaliti. NCCR-Mageuzi leo kingekuwa na nguvu ileile ya miaka ya 1990, sipati picha siasa za Tanzania zingekuwa na sura gani. Hata hivyo kiliuawa kwa wimbo wa kusalitiana. Ukifuatilia, mtunzi wa wimbo usaliti anatokea Chama Tawala.

Mtunzi wa wimbo “usaliti wa Zitto” hupati shida kumtambua. Mtunzi wa wimbo “CHADEMA ya Wachaga” au “CHADEMA Saccos ya Edwin Mtei na Mbowe” yupo. Ila waliokariri nyimbo ndiyo wakaziimba kwa bidii kubwa mithili ya msanii wa American Idol au Bongo Star Search. Wakasahau nyimbo zina watunzi wao na walitunga kwa sababu maalum. Wakaziimba kama zao.

Watu hawajui kuwa mtu akiwa anataka kununua nyumba yenu ya urithi kwa bei nafuu au kama hapendi kuona mnavyoelewana na kushirikiana, anaweza kuwachonganisha kisha moto ukiwaka, ndipo unasikia “tuuze nyumba tugawane kila mtu na chake”, bila kujua kuwa ugomvi wenu ni mafanikio ya mchonganishi. Mara nyumba inachorwa “epuka matapeli nyumba hii haiuzwi.”

Vita ya Mbowe na Zitto iliwanufaisha mno CCM, maana ilikuwa kujishambulia wenyewe. Wapinzani wanapogombana wao kwa wao, maana yake wanakuwa wanaushambulia upinzani, hivyo Chama Tawala kinajitanua kama siyo kujinafasi vizuri. Mbowe na Zitto walihitaji kukumbushwa kuwa wao ni wapinzani ambao hawatakiwi kugombana wao kwa wao, bali wanapaswa kuunganisha nguvu kumkabili adui yao.

Ametokea Rais John Magufuli. Mtikisiko ambao ameusababisha kwa wapinzani, sasa unawazindua Zitto na Mbowe. Wanaona umuhimu wa kushirikiana, maana wao wote ni wapinzani. Alichokifanya Dk Magufuli kuwaunganisha Zitto na Mbowe ni sawa tu na Japan ilivyowaunganisha Wachina ambao miaka nenda rudi walikuwa kwenye vita ya wao kwa wao. Wakakumbuka kuwa kumbe kuna umuhimu wa kushirikiana kama taifa.

Wenye uadui mdogo huungana pamoja pale anapokuwepo adui mkubwa zaidi dhidi yao. Mkiwa mnachukiana kidogo, anapotokea yule ambaye nyote mna chuki kubwa juu yake, mnaungana kumkabili. Zitto na Mbowe wanaungwanishwa na adui mkubwa zaidi.

China ni mfano hai, ilibidi waungane na waache kupigana kwa maslahi ya taifa lao. Wachina walisitisha vita ya wao kwa wao na kuungana pamoja kupigana na Wajapan katika Vita ya Sino-Japanese II. Kituko ni kuwa Wachina baada ya kumshinda Mjapan walirudi tena kupigana wenyewe kwa wenyewe.
Kulikuwa na mchuano mkali wa kugombea madaraka kati ya Chama cha Kuomintang (KMT) ambacho kilikuwa kinawakilisha daraja la watawala China dhidi ya Chinese Communist Party (CCP), kilichowakilisha watawaliwa.

Kuomintang na Communist, vilipigana vita ya wenyewe kwa wenyewe. Ilianza Agosti Mosi, 1927 lakini pande zote mbili zilikubaliana kusitisha mapigano kisha kuunganisha nguvu dhidi ya Japan katika Vita ya Sino-Japanese II kati ya mwaka 1937 mpaka 1945, ikikutana juu kwa juu na Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Baada ya Vita ya Sino-Japanese pamoja na Vita Kuu ya Pili ya Dunia kwisha, Kuomintang na Communist walitengana na kuchapana wao kwa wao mpaka Mei Mosi, 1950, Communist waliposhinda na kushika hatamu ya kuongoza Jamhuri ya Watu wa China.

Ni darasa kwa Mbowe na Zitto kuona kuwa wao wote ni walewale na walipaswa kutambua hivyo muda mrefu uliopita. Siyo sasa, wanakuwa wameshachelewa sana. Ni sawa sasa Zitto na Mbowe kushirikiana. Wakati huohuo tukumbuke kuwa leo kuna muungano wa vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi. Na isisahaulike kwamba huko nyuma vyama hivyo havikuwa vikiiva. Vilikuwa vikisuguana vyenyewe kwa vyenyewe badala ya kushughulika na adui yao mkuu. Matokeo yake adui yao akawa anapumua kwa kitendo cha maadui zake kulumbana kama siyo kupigana.

Tukumbuke kuwa mwaka 2010, vyama vya NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF), vilipiga kelele sana kutaka nao waunganishwe katika kambi rasmi ya upinzani lakini CHADEMA kilichokuwa na wabunge wanaojitosheleza kuunda kambi, wakadengua kisha wakafunga milango. Hawakutaka ushirikiano.

Ukatokea mvutano mkubwa, nakumbuka hata bungeni walitoleana lugha chafu. NCCR-Mageuzi na CUF waliwaita CHADEMA ni wabinafsi na kwamba ni hatari endapo watapewa nchi, kwamba kambi tu ya upinzani hawataki kushirikiana na wenzao, je wakishika dola?

CHADEMA wakasema hawawezi kushirikiana na CUF kwa sababu kinaunda serikali Zanzibar (wakati huo), wakawaita CCM B. Tundu Lissu akasema, CHADEMA hakiwezi kuunganisha nguvu na vyama dhaifu, akakitolea mfano UDP chenye mbunge mmoja (wakati huo) ambaye ndiye mwenyekiti, John Momose Cheyo.

Kipindi cha malumbano hayo, CCM kilikuwa kinakenua, kinaona kuwa wapinzani walikuwa wakipigana vita batili, katika muda batili dhidi ya adui batili. Ni utaratibu, maadui zako wakiwa wanatwangana, wewe unapumua, maana mashambulizi hayaelekezwi kwako tena.
Ni kama Japan ilivyoona Wachina wanapigana wao kwa wao, ikaona bora kuvamia. Bahati yao Wachina wakaamua kumaliza tofauti zao kwa muda na kushirikiana kuikabili Japan.

Baada ya wapinzani kuvurugana mno, mwaka 2014, walijikuta wanakumbushwa adui yao ni nani wakati wa Bunge Maalum la Katiba. CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, viliona vyote havina wema kwa CCM.

Kimsingi hakuna chama cha upinzani dhidi ya kingine cha upinzani. Kinaitwa chama cha upinzani kwa sababu kinakuwepo kingine kinachotawala. Vyama vya UKAWA, vilikumbushwa kutambua kuwa vyenyewe kama vilivyo, ikiwa kuna jambo halipo sawa katika utawala wa nchi, vyote vinaathirika.

Misimamo ya CCM juu ya uelekeo wa Katiba Mpya, ikawafanya wapinzani wakumbuke kuwa ushirikiano ni muhimu katika kuhakikisha wanakuwa imara. Ndipo wakaungana.

Mwaka jana kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, Zitto na chama chake (ACT-Wazalendo) waliomba kujiunga UKAWA wakakataliwa. Walipokutana bungeni, baada ya dhoruba za hapa na pale, wamekumbuka kuwa kumbe uadui wao siyo mkubwa kuzidi ule wa watawala. Wameamua kuungana.

Hapo juzi, Zitto alikuwa anasakwa na polisi akiwa hajulikani alipo, wakati huohuo Mbowe alikuwa ameshatiwa mbaroni. Kumbe wote ni walewale, wanachotakiwa kufahamu ni kuwa wao wote ni wapinzani mbele ya mamlaka za mtawala. Kwa muda mrefu Zitto na Mbowe walipigana vita batili. Walikuwa chama kimoja (CHADEMA), wakashindwa kuishi pamoja, kwa hiyo wakafukuzana. Nje ya chama wakawa hawaivi.

Uchaguzi Mkuu 2015 ulionesha picha kuwa wapo watu wa ACT-Wazalendo, waliona bora CCM washinde kuliko CHADEMA. Vivyo hivyo kwa CHADEMA, katika maeneo ambayo hawakuwa na nguvu, waliona bora CCM ishinde kuliko ACT-Wazalendo.

Yapo majimbo mengi CCM kilishinda kwa sababu ya mvutano wa CHADEMA (UKAWA) na ACT-Wazalendo. Uchaguzi umekwisha, shuluba wanayokutana nayo inajidhihirisha kuwa kumbe wao hawatakiwi kupigana, tena ikiwezekana ni afya mno endapo watashirikiana.

Kama hili huwa hawajawahi kulifikiria ni kwamba wapo watu walipoteza matumaini na upinzani, hivyo kujielekeza CCM au kususia kabisa siasa kutokana na mivutano ya wapinzani hususan Zitto na Mbowe. Ni muda wao kujifunza na kujisahihisha.

Ni hapa ndipo inabidi kukiri kuwa Dk Magufuli ni mwalimu mzuri kwa Zitto na Mbowe. Anawafundisha na kuwakumbusha kwa wakati mmoja kufahamu umuhimu wa wao kubaki kitu kimoja. Siyo kuendelea kupigana vita batili wakati wao wote shabaha yao ipo kwa aliyeshika nchi. Wao wote hawana mamlaka, ni wapinzani tu.

Ndimi Luqman Maloto
 
Mi naona Mbowe ndio dikteta amebadili katiba ya chadema kinyemela ili aendelee kuwa mwenyekiti milele...mbowe awaachie na wengine akae pembeni
 
Kuungana kwa Zitto na Mbowe ni pigo kubwa sana UKAWA...umesahau kuwa Zitto na familia ya JK ni maswahiba wakubwa?? Mengine utajaza mwenyewe
 
Kweli Magufuli ni mwalimu wao mzuri maana atawanyosha tu na watanyoka,atakayekaidi kunyoshwa atavunjika.
 
And ofcourse " we need a common enemy to unite us "-Condi Rice
Inawezekanaje kujiunga na msaliti dhidi ya common enemy. U'common unatokea wapi na msaliti.Hauoni adui atafaidi zaidi kama kati yenu kuna msaliti??? Ama mnataka kutuaminisha kuwa ule " usaliti" haukuwa kweli bali ni mpango wa kumpoteza tu ili Mbowe asipate upinzani kwenye uenyekiti wa chama?????
 
K
Inawezekanaje kujiunga na msaliti dhidi ya common enemy. U'common unatokea wapi na msaliti.Hauoni adui atafaidi zaidi kama kati yenu kuna msaliti??? Ama mnataka kutuaminisha kuwa ule " usaliti" haukuwa kweli bali ni mpango wa kumpoteza tu ili Mbowe asipate upinzani kwenye uenyekiti wa chama?????
huu wimbo wa usaliti ndio unaowapoteza, kwa mpinzani wa kweli, ushauri wa Luqman basi yatosha kusema ni wa mazingatio kwa mwenye akili
 
Inawezekanaje kujiunga na msaliti dhidi ya common enemy. U'common unatokea wapi na msaliti.Hauoni adui atafaidi zaidi kama kati yenu kuna msaliti??? Ama mnataka kutuaminisha kuwa ule " usaliti" haukuwa kweli bali ni mpango wa kumpoteza tu ili Mbowe asipate upinzani kwenye uenyekiti wa chama?????
haukuwahi kuwepo!!...ku fend off changamoto na mawazo mbadala ndio lilikua lengo na " usaliti" ilikua njia.watakapojaribu kutengeneza now kuna watu walioanza kuwaamini watawapoteza pia...ni risk!wahesabu tu gharama ya "kuifuta dhambi ya usaliti ya Zitto" (kama walivyofanya kwa Edo) wajiunge nae tena au wakomae tu huku moyoni wakijua wanakosea ilimradi waonekane wamesimamia maneno yao japo watarisk kupigana a wrong war against a wrong enemy...CDM kuna wachanga wengi sana mule
 
Back
Top Bottom