KAULI za kibabe na vitisho vya matumizi mabaya ya madaraka zilizotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi dhidi ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Godbless Lema na kuwatetea mafisadi wa Richmond na EPA, zimemtokea puani akidaiwa kuwa gamba linalopaswa kung'oka.
Lukuvi alitumia madaraka yake vibaya juzi wakati akihojiwa na kituo cha runinga cha Star tv, katika kipindi cha Tuongee Asubuhi, kwa kumtisha mtazamaji aliyepiga simu kuchangia mjadala na kupinga maelezo yake kwamba Serikali ya Awamu ya Nne imefanya mengi ya kujivunia.
Katika kujibu hoja, Lukuvi alidai mtazamaji huyo hakuwa mkazi wa Dodoma; na kwamba kwa jinsi alivyosikia sauti ile na hoja zake, simu ile ilikuwa imepigwa na Lema.
Katika hali ya kulewa madaraka, Lukuvi alitumia vitisho akisema kuwa anaagiza watumishi wa ofisini mwake wachunguze kama simu hiyo haikutoka kwa Lema.
Mbali na kauli hiyo, Lukuvi bila aibu alipohojiwa kuhusu ufisadi wa Richmond, EPA na mengine yaliyofanywa na viongozi, alijibu kuwa hizo ni santuri za zamani, hazipaswi kujadiliwa sasa badala yake watu wajadili mafuta na gesi.
Wakizungumza na Tanzania Daima, wasomi mbalimbali walisema kuwa kauli za Lukuvi ni za kuvunja katiba na uthibitisho kwamba naye ni gamba ambalo linapaswa kung'oka ndani ya serikali.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azavery Lwaitama, alisema kuwa Richmond haiwezi kutenganishwa na mafuta na gesi kwa kuwa wale wale waliohusika nayo leo wanautafuta urais, hivyo lazima watumie watu wa kuwatetea.
"Mimi nawashangaa sana waandishi, kwani mlitaka ama kutegemea Lukuvi aseme nini? Tatizo ni nyie ambao baadhi yenu wanatumika kuwapigia debe mafisadi waliotufikisha hapa kwa kunadi agenda zao za uzushi wanazoziibua sasa," alisema.
Alisema kama Lukuvi na serikali anayoitumikia hawataki wananchi wajadili ufisadi wa Richmond, EPA na madudu mengine, hiyo ni dadili kuwa wanajiandaa kufanya ufisadi wa kutisha huko kwenye mafuta na gesi wanakotaka kukimbilia.
Dk. Lwaitama alisisitiza kuwa, kuacha kuhoji ufisadi huo leo ni sawa na kuandaa kashfa nyingine, na kwamba yeye hana shida na Lukuvi isipokuwa wale wanaokubaliana na hoja anazozieneza.
"Haya anayotueleza Lukuvi ndiyo mtindo wa viongozi kurukaruka wakati wakitafuta madaraka na kusahau kuwa waliwahi kuwa na dhamana wakashindwa kufanya. Mfano Edward Lowassa alijiuzulu kwa kashfa ya Richmond, lakini hadi leo anasema hausiki ila hataji nani anahusika," alisema.
Dk. Lwaitama alisema kuwa badala yake Lowassa amegeuka na kuibua hoja mpya za ajira, tume ya elimu halafu watu wanamshangilia bila kumhoji ni kwanini ushauri huo autolee jukwaani badala ya kwenye vikao vya chama chake.
Kwamba hata Lukuvi anatumia mtindo huo wa kupoteza hoja na kurukia kuwatetea mafisadi waliosababisha matatizo ya umeme nchini hadi leo.
"Chama hiki kama kimeshindwa kujivua gamba ina maana kinapaswa kuondolewa kwa hiyo hata kauli za Lukuvi za kuwatisha wanaoikosoa serikali au kuhoji ufisadi ni dalili za yeye kushindwa kujivua gamba na kuhamia kutetea mafisadi," alisisitiza Dk. Lwaitama.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba, alisema kuwa kauli hiyo ya Lukuvi ni sawa na kuvunja katiba Ibara ya 18, inayotoa uhuru kwa kila Mtanzania kutoa maoni yake.
Kibamba alisema hiyo ni hali ya ulevi wa madaraka inayojengwa na baadhi ya viongozi kufikiri kuwa wao ndio wanajua zaidi na hivyo wengine wasihoji mambo yanayohusu nchi.
"Lukuvi ana uhakika gani kuwa katika miradi hiyo ya gesi asilia hakutakuwepo na mikataba mibovu itakayosababisha viongozi waibe fedha na kuweka kwenye mifuko yao badala ya kuelekeza kwenye mifuko ya maendeleo ya jamii?" alihoji.
Aliongeza kuwa, kiongozi mwenye kuheshimika kama Lukuvi asingepiga propaganda hizo, lakini akadai kuwa hana jinsi kwani wanaopiga propaganda ndio wanaoonekana wa kuheshimiwa na chama chake cha CCM.
"Tumejifunza kilichotokea jana na leo ndiyo kinaamua nini kinatokea kesho. Kwa hiyo walioiba jana na leo wanasema tusahau ya jana ili tuingie mkataba leo, wanajenga dhana kuwa wakiiba kesho watatuambia ni santuri ya wimbo wa gesi asilia umepitwa na wakati, watakuja na wazo jingine ili waendelee kuiba, hivyo kauli ya Lukuvi ni ya kupuuzwa," alisema.
Wakili wa kujitegemea, Mabere Marando alisema makampuni ya simu hayaruhusiwi kutoa siri za wateja wao, lakini Lukuvi amezungumza kwa kujiamini, pengine huwa anatumia ubabe wa kichama kuvunja sheria za nchi.
Alisema kuwa kama kiongozi hakupaswa kutamka vile kwa kumtisha mtazamaji aliyechangia hoja kwenye mjadala uliokuwa ukiendelea hata kama angekuwa ni Lema mwenyewe.
Kuhusu hoja ya kuwataka Watanzania waache kuzungumzia ufisadi wa EPA na Richmond, alisema kauli hiyo ni kuwalazimisha wananchi wasahau maovu yao, na kuwaelekeza kusiko.
"Wiki hii nitakuwa na mikutano Ruaha na Kilombero na sitaachana na hoja hiyo hadi tarehe 29/10/2015. CCM wameibia wananchi sana, tunapoacha kuzungumzia wizi huu tutakuwa tunabariki tabia hii," alisema.
Lukuvi akanusha
Alipotafutwa na gazeti hili jana, kufafanua maagizo yake ya vitisho kwa Lema, Lukuvi alikana akidai kuwa hakusema kwamba aliyepiga simu ni Lema, bali sauti hiyo ilifanana na sauti ya Lema.
Alipoulizwa kama amefanikiwa kuhakikisha kuwa aliyepiga alikuwa Lema au la, Lukuvi alijibu: "Unaniuliza nini wakati tayari leo mmeshanihukumu?
"Mimi nitaongea na Lema mwenyewe sitaki kuongea na gazeti, kwanza habari yenyewe imeandikwa na gazeti moja tu, hivyo sioni kama ina madhara."
Alipobanwa zaidi kuhusu kuingilia mawasiliano ya mtu, kazi ambayo inapaswa kufanywa na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) tena kwa kibali maalumu kama mtu ametuhumiwa kwa makosa ya jinai, Lukuvi aliendelea kung'aka akisema, "nimekwambia siongei na mtu wa gazeti."
|
|