Mwakaboko King
JF-Expert Member
- Apr 22, 2015
- 1,099
- 207
Picha - Wananchi wakiangalia majina yao kwenye Daftari la Wapiga Kura lililowekwa wazi.
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lilianzishwa chini ya Ibara ya 5 (3) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Kufuatia kuanzishwa kwa Daftari hilo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi hutekeleza uandikishaji wa Wapiga Kura chini ya Ibara ya 74(6)(a) na (e) ya Katiba.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inawajibika :- Kusimamia na kuratibu Uandikishaji wa Wapiga kura wapya waliotimiza umri wa kuandikishwa nchi nzima na Kusimamia na kuratibu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume inatakiwa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya Uchaguzi Mkuu mmoja na unaofuata.
Zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni linawahusu wananchi wote: -
- Waliotimiza Umri wa Miaka 18 na kuendelea ambao hawakuwahi kuandikishwa hapo awali;
- Waliojiandikisha awali kwenye Daftari hilo lakini wamehama kata au jimbo moja kwenda jingine;
- Linafanyika kuondoa wale waliofariki,
- Kufanya marekebisho ya majina yaliyokosewa wakati wa Uandikishaji,
- Pamoja na Kutoa kadi mpya kwa wale waliopoteza au wale ambao Kadi zao za Kupigia Kura zimeharibika.
(i) Awe Raia wa Tanzania;
(ii) Awe ametimiza umri wa miaka 18; na
(iii) Awe hajapoteza sifa kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi au Sheria nyingine yoyote iliyotungwa na Bunge.
Kuweka wazi Daftari la Awali la Wapiga Kura
Kwa mujibu wa Vifungu vya 11A na 22 vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, na Kifungu cha 15A cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, Tume hutakiwa kuweka Wazi Daftari la Awali la Wapiga Kura ili kutoa fursa kwa wananchi:
i. Kulikagua Daftari;
ii. Kufanya marekebisho ya jina au mahala wanapoishi;
iii. Kuingiza au kufutwa jina la Mpiga Kura;
iv. Kuweka pingamizi kwa Mpiga Kura aliyeandikishwa.
Kumwekea Pingamizi aliyeandikishwa kwenye Daftari la Awali.
Vifungu vya 24 na 25 vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 vinaruhusu Mkurugenzi wa Uchaguzi au Afisa Mwandikishaji au mtu yeyote aliyeandikishwa kuwa Mpiga Kura kuweka pingamizi dhidi ya jina lililopo katika Daftari la Awali la Wapiga Kura.
Kila pingamizi litatakiwa kuwekewa dhamana ya fedha ambayo Tume itakuwa imeweka kupitia Tangazo la Serikali. Aliyewekewa pingamizi hutakiwa kupelekewa taarifa ili aweze kutoa ufafanuzi ndani ya siku zitakazoelekezwa na Tume.
Kifungu cha 27 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, kinatoa fursa iwapo aliyewekewa pingamizi hakukubaliana na maamuzi ya Afisa Mwandikishaji ya kuendelea kukataliwa kuwemo katika Daftari kukata rufaa ya kupinga maamuzi hayo katika Mahakama ya Wilaya.