Lema, Chatanda wavutana bungeni

Lilombe

JF-Expert Member
Apr 11, 2011
242
39
MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) na Mbunge wa Viti Maalumu, Mary Chatanda (CCM) jana walilumbana bungeni kuhusu mauaji yaliyotokea mkoani Arusha, huku Lema akimtuhumu mwenzake kwamba ndiye chanzo cha mauaji hayo.

Malumbano hayo yalianza muda mfupi baada ya Chatanda kumaliza kuchangia hotuba ya Makadiro ya Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, ambapo Wizara hiyo imeomba Bunge liidhinishe matumizi ya Sh. bilioni 16.2.

Baada ya Chatanda kumaliza kuzungumza, Lema alisimama na kuomba kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kikao cha jana, Sylivester Mabumba, ambaye ni Mbunge wa Dole (CCM) na kueleza kuwa wakati Chatanda akizungumza, alipongeza mwafaka wa madiwani wa Chadema na CCM Arusha.

Pia alishukuru wanawake wa Tanga kwa kumchagua kuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia mkoa huo.

Lema alisema kauli ya Mbunge mwenzake kupongeza madiwani wa Chadema kwa mwafaka wa Arusha si sahihi, kwani hakuna kitu kama hicho na kwamba mwishoni mwa wiki, Kamati Kuu ya Chadema ilikuwa na kikao na jambo hilo halitambuliki.

Alieleza kuwa kama Mbunge huyo anatafuta mwafaka wa jambo hilo, aendelee kuutafuta, lakini aelewe Chadema haijui suala hilo na kusema kwamba Chatanda alikwenda kufanya fujo jimboni mwake Arusha huku akijua yeye anatoka Tanga na kumtuhumu kuwa chanzo cha mauaji ya Arusha.

Watu watatu waliuawa na polisi Arusha katika maandamano haramu yaliyoandaliwa na kufanywa na wana Chadema wakiongozwa na viongozi wao.

Baada ya taarifa hiyo, waliendelea kuchangia wabunge wengine wawili hotuba ya Waziri, kisha Chatanda akasimama na kuomba Mwongozo wa Mwenyekiti. Chatanda alisema: “Lema alipotoa taarifa, alisema chanzo cha mauaji ya Arusha ni Mary Chatanda, ningekuwa nimefanya hivyo, tayari ningekuwa nimeshitakiwa hivi sasa.

“Amenisingizia, amenidhalilisha, naomba Mwongozo wako Mwenyekiti,” alisema Mbunge huyo ambaye pia ni Katibu wa CCM wa Mkoa wa Arusha. Akitoa Mwongozo, Mwenyekiti Mabumba alisema suala la mauaji ya Arusha liko mahakamani, hivyo si sahihi kulizungumzia kwa kuwa Mahakama ndiyo itaamua kama kuna mtu ametuhumiwa au anatuhumiwa.

Wakati huo huo, Theopista Nsanzugwanko, anaripoti kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, amesema madiwani wa chama hicho Arusha waliotakiwa kujiuzulu, watachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa hawatafanya hivyo ifikapo leo mchana.

Madiwani hao walitakiwa na Kamati Kuu ya Chama hicho kujiuzulu nyadhifa zao katika halmashauri ya jiji hilo, kutokana na madai kwamba walizipata kinyume cha utaratibu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Dk. Slaa alisema hatua hizo zitachukuliwa baada ya leo mchana ikiwa atakuwa hajapokea vithibitisho vinavyoonesha kuwa watakuwa bado hawajajiuzulu.

Dk. Slaa alisema baadhi ya madai ya madiwani hao juzi yalipotosha baadhi ya mambo ikiwamo kudai kuwa walituhumiwa kupokea rushwa ili kufikia mwafaka kati yao na madiwani wa CCM.

Slaa alisema Kamati iliyokuwa ikiongozwa na Mabere Marando haikuwatuhumu madiwani hao kula rushwa, wala hakuna aliyetuhumiwa na kamati hiyo, ila yeye Katibu Mkuu alipata malalamiko hayo.

Alisema kama wao wametuhumiwa kwa rushwa, wanaweza kuchukua hatua zozote za kisheria wanazoona zinafaa, lakini suala la kujiuzulu nyadhifa zao liko pale pale.

Source: GAZETI LA HABARI LEO, Juni 22, 2011
 
Back
Top Bottom