Wild Flower
JF-Expert Member
- Jul 20, 2023
- 844
- 1,604
Jamii hasa vijana, wamekumbushwa kutambua kwamba tunu ya pekee katika taifa ni amani, upendo na mshikamano hasa katika kipindi hiki kuelekea zoezi la kupiga kura na kwamba ni jukumu la kila mmoja kulinda na kuhakikisha uwepo wa amani hiyo. Hayo yamebainishwa leo Oktoba 20, 2025, na aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii hapa nchini, Lazaro Nyalandu, alipokuwa akizungumza katika kongamano la amani la viongozi wa dini mbalimbali linalofanyika mkoani Mwanza.
“Tuwakumbushe vijana wetu, waumini wetu, kwamba hakuna tunu muhimu katika Taifa zaidi ya amani, upendo na mshikamano. Tunapofanya zoezi hilo la kupiga kura, tunapowasisitiza watoke, basi tuhakikishe kila mtu anailinda hiyo amani, anashiriki katika upendo wa watanzania na anafanya zoezi la haki yake ya kupiga kura” amesema Nyalandu.
Amesema ipo haja ya Tanzania kuendelea kulea imani zote za dini, ambapo nchi pamoja na mamlaka husika zinajipambanua kukosa udini, badala yake kuruhusu amani na uhuru kwa watu wote pamoja na kuendelea kuishi kwa amani. Kongamano hilo limeandaliwa na Kamati ya amani ya viongozi wa dini mbalimbali mkoa wa Mwanza, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Said Mtanda, likiwa na mada isemayo “Uchaguzi ni Muda wa Maamuzi, Tushiriki Sote. Tudumishe Amani na Mshikamano kwa Maendeleo ya Taifa”