Getrude Mollel
JF-Expert Member
- Apr 26, 2022
- 308
- 424
Historia Fupi ya vyama vingi Tanzania
Tanzania ilirudia mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 baada ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 1977 kuruhusu ushindani wa kisiasa. Kabla ya hapo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho kilichokuwa chama pekee, kikiwa na mizizi kutoka TANU ya Tanganyika na ASP ya Zanzibar.Kuanzia uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, vyama vya upinzani vimekuwa vikijitokeza, vikishindana na CCM, ingawa mara zote CCM kimeendelea kushinda kwa kishindo kutokana na sera thabiti za maendeleo.
CCM imekutana na vyama vingi vya vikubwa vya upinzani kama NCCR-Mageuzi na CUF ambavyo vyama hivi vilikuwa vyama vya upinzani kwelikweli. CHADEMA, ambacho kinaitwa kama chama cha upinzania hivi sasa, kutokana na changamoto za kimfumo, itikadi, rasilimali watu wa fedha, CHADEMA inakosa hadhi kabisa ya kuitwa chama kikuu cha upinzani. Kabla sijatoa sababu kwanini CHADEMA haina hadhi ya kuwa chama kikuu cha upinzani, kwanza kwa uchache sana nitaeleza historia fupi ya CHADEMA.
Historia fupi ya CHADEMA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilianzishwa mwaka 1992 kama sehemu ya vyama vipya vilivyosajiliwa kufuatia kurejeshwa kwa vyama vingi.Kimepata umaarufu zaidi katika miji mikubwa kama Arusha, Mwanza na Dar es Salaam, lakini kimeendelea kudorora vijijini. Viongozi wake kama Freeman Mbowe na Tundu Lissu wamekuwa sura zinazojulikana, lakini chama kimekosa taasisi imara na sera mbadala zinazoweza kushindana na zile za CCM.
Kwa nini CHADEMA haina hadhi ya kuwa chama kikuu cha upinzani?
1. Ukosefu wa sera mbadalaCHADEMA kimekuwa chama cha malalamiko zaidi kuliko chama cha sera. Wakati serikali ya Rais Samia ilipoanzisha ruzuku ya mbolea mwaka 2022 na kushusha bei kwa zaidi ya 50%, CHADEMA walipinga bila kutoa suluhisho jingine kwa wakulima. Huu ni udhaifu mkubwa kwa chama kinachojiita kikuu cha upinzani. Chama cha siasa kinatakiwa kufanya constructive criticism", yani kukosoa kwa kujenga lakini Chadema, kimekuwa chama kinachokosoa tu bila kutoa hoja mbadala.
2. Uongozi wa kutegemea watu wachache
Chama kimeegemea kwa majina machache pekee, mwanzo alikuwa Mbowe na sasa Lissu. Uchaguzi wa 2020 ulipoisha na Mbowe akakamatwa kwa makosa ya uchochezi, chama kilibaki dhaifu bila uongozi mbadala. Hii inaonyesha si taasisi, bali klabu ya kisiasa ya watu wachache, tofauti na CCM iliyo na mfumo wa kitaifa kuanzia ngazi ya shina. Hivi sasa Mh. Tundu Lissu yuko ndani kwa makosa ya uhaini, chama kimekosa dira, kimepoteana na kina hali mbaya kuanzia taifa hadi katika ngazi ya mtaa.
3. Kushiriki harakati badala ya siasa za hoja
Badala ya kushindana kwa hoja bungeni au kwenye majukwaa ya sera, CHADEMA mara nyingi hujikita kwenye maandamano ambayo kimsingi hayana matokeo yeyote. Mfano ni kampeni ya “Ukuta” mwaka 2016 ambayo ilihamasisha maandamano ya nchi nzima lakini mwisho wake hayakuletea wananchi maendeleo bali vurugu na taharuki.
4. Kupoteza imani vijijini
Tanzania ni taifa la wakulima na wafugaji. CCM imewekeza kwenye skimu za umwagiliaji Ifakara, ruzuku ya mbolea, barabara na vituo vya afya vijijini. Uchaguzi wa 2020 ulionyesha wazi CCM ikipata zaidi ya 80% ya kura vijijini, huku CHADEMA ikibaki na ushawishi mdogo mijini pekee. Hivi sasa, CCM ina mashina zaidi ya 200,000 nchi nzima, na imefanya makubwa kwa watu wa vijijini kama kusambaza umeme kwenye vijiji vyote kwa 100%. Wakati wa CUF na NCCR, vyama hivi vilikuwa na wanachama wengi vijijini lakini kwa CHADEMA, kimebakia kuwa chama cha mijini tu.
5. Kususia uchaguzi
Mara kadhaa CHADEMA kimeamua kususia uchaguzi. Mfano ni uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 ambapo walijiondoa wakidai kasoro. Hatua hii iliwanyima nafasi ya kushiriki katika maamuzi ya wananchi ngazi ya msingi. Chama kikuu cha upinzani hakiwezi kila mara kujitenga badala ya kushindana. Hivi sasa, wakati tunakwenda kushiriki uchaguzi wa mwaka huu Oktoba 2025, CHADEMA imejitoa kwenye mchakato huu, Je, hii ni hadhi ya chama kikuu cha upinzani?
6. Siasa za mgawanyiko
CHADEMA mara nyingi huchochea siasa za kikanda na mara nyingine kidini. Wakati wa kampeni za 2010 na 2015, viongozi wake walilalamikiwa kwa kusisitiza hoja za “kanda ya kaskazini.” Hii ni hatari kwa mshikamano wa taifa, tofauti na CCM ambayo kila mara imehubiri umoja wa kitaifa bila ubaguzi. Lowassa mwaka 2015 akiwa mgombea wa Urais wa CHADEMA, alisikika akifanya siasa za udini Kanisani. Hii sio hadhi ya chama kikuu cha upinzani. Chama cha upinzani kinapaswa kuwa chama kinachounganisha watu sio kuwagawa kwa dini na kabila zao.
Tanzania inahitaji upinzani makini wenye hoja na sera mbadala. CHADEMA kimekosa dira hiyo. Ni chama cha malalamiko, cha watu wachache chini ya 400,000 nchi nzima, na cha siasa za mgawanyiko. CCM imebaki kuwa chama pekee chenye taasisi thabiti, sera za ukweli na matokeo yanayoshikika kwa wananchi. Hivyo basi, CHADEMA haina hadhi ya kuitwa chama kikuu cha upinzani.