Kwa makala hizi za Kubenea waliokwenda Chadema na Lowassa hawakuwa wasafi wanatakiwa kutumbuliwa

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
Wadau nimekuwa nasoma sana makala za Kubenea za miaka ya nyuma wakati ule amabapo alijulikana kama mwandishi nguli na mwiba kwa mafisadi na wahujumu wa nchi yetu, leo nimekutana na andika lake moja linalomuhusu Masha na Mzee Kingunge ambao pia wapo kambi moja ya kisiasa na Kubenea Chadema.

Ukiisoma Makala hii utagungua kuwa waliokimbilia Chadema wengi wao wana madhambi ambayo yakiwekwa hadharani nao basi muda si mrefu watatumbuliwa jipu. Na sijui ikifikia hatua hiyo ya kuwatumbua majipu Kubenea atatuandikia nini kwa kuwa alikuwa akiwaponda sana na kuwaona kama mafisadi na wahujumu?

Mdau soma mwenyewe unipe coment yako kama hawa majipu au la?


Vigogo wahaha kumwokoa Masha


Na Saed Kubenea - Imechapwa 11 February 2009


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, ambaye katika misingi ya utawala bora angekuwa ameshajiuzulu au amefukuzwa kazi, sasa ameanza kukingiwa kifua, MwanaHALISI limeelezwa.

Masha anakabiliwa na tuhuma nzito za kuingilia mchakato wa kutafuta mzabuni wa kutengeneza vitambulisho vya taifa katika mradi utakaogharimu zaidi ya Sh. 200 bilioni ulioko chini ya wizara yake.

Waziri anadaiwa kubeba malalamiko ya kampuni ya nje iitwayo Sagem Securite na kuyatumia kujenga hoja ya kurejewa hatua za mchakato ili naye awemo.

Katika wiki moja tangu kufumuka kwa taarifa za waziri huyo kuingilia mchakato, Masha ameripotiwa kuwa katika wakati mgumu kwa kuwa suala lake ndilo limekuwa “gumzo la Dodoma.”

Hakuna taarifa zozote juu ya alichokisema Rais Jakaya Kikwete alipokutana na Baraza la Mawaziri mjini Dodoma, lakini taarifa zisizorasmi zinasema alidokeza juu ya “mwenendo wa baadhi ya viongozi na misingi ya maadili ya uongozi.”

Aidha, kuna taarifa kuwa waziri Masha amekwenda nyumbani kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kukutana naye. Haijafahamika ilikuwa matembezi ya kawaida, kikazi au safari mahsusi ya “kutafuta kinga” kutoka kwa kiongozi wa shughuli za serikali bungeni.

Bila ya kutaja majina, mbunge wa kuteuliwa, Kingunge Ngombale-Mwiru, alikiambia kikao cha wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma kuwa “waweke mbele maslahi ya chama.”

Ngombale-Mwiru amenukuliwa akisema kuna wanaosema “maslahi ya taifa kwanza.” Alisema sharti waweke maslahi ya chama mbele na kwanza.

Hoja yake ilionekana kama majibu ya hoja nyingine kuwa kashfa inayomkabili Masha, inaweza kuwa mtaji mkubwa kwa vyama vya upinzani; na kwamba wabunge wa CCM wasiposimama pamoja, basi chama kitabomoka.

Wachunguzi wa siasa za CCM wanasema kauli ya Ngombale-Mwiru ni sehemu ya vitisho kwa wabunge na hata karipio kwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kwa kitabu alichozindua (ambamo kuna sura aliyoandika) kiitwacho Bunge lenye meno ambacho kinasisitiza utaifa kwanza.

Hadi tunakwenda mitamboni, Kamati ya bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambayo ilipewa jukumu la kushughulikia hoja ya Masha kuingilia Bodi ya Zabuni ilikuwa haijatoa taarifa zozote kwa spika.

Kamati hiyo inayoongozwa na mbunge wa Muleba Kusini, Wilson Masilingi ilitakiwa kusikiliza hoja binafsi ya mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa juu ya tuhuma dhidi ya Masha na hatimaye kuwasilisha matokeo kwa spika.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya kamati zinasema wajumbe wake wamegawanyika kuwili. Upande mmoja unataka suala hilo lipelekwe bungeni na wengine wanataka liishie kwenye kamati.

Kinachofanya baadhi waogope hoja hiyo kwenda bungeni ni hofu ya kuundwa kwa Kamati Maalum ya kuchunguza tuhuma na hatimaye kuja na hitimisho kama lililomkumba aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa.

Naye baba yake Masha ambaye ni mbunge wa Baraza la kutunga Sheria la Afrika Mashariki, Dk. Fortunatus Masha, ameripotiwa kuwapo mjini Dodoma akikutana na baadhi ya wabunge na viongozi mbalimbali.

Taarifa zimeenea mjini Dodoma kuwa Dk. Masha amekuwa akiwaomba wabunge na viongozi wengine kumnusuru mwanae.

Waziri Masha anataka kukwepa, pamoja na mambo mengine, tuhuma za:

  • Kujipatia taarifa za maandishi juu ya mchakato wa zabuni wakati yeye siyo mjumbe wa Bodi ya Zabuni.
  • Kulalamikia hatua za Bodi ya Zabuni wakati yeye hayumo katika mlolongo wa wahusika.
  • Kutumika kama mlalamikaji wa mmoja wa wazabuni kutoka nchi ya nje kiasi cha kufikisha kilio kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
  • Kushinikiza Katibu Mkuu wa wizara yake kutafuta ushauri wa Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi serikalini (PPRA) wakati suala hilo halihitaji kufikishwa huko katika hatua ya sasa.
  • Kutawanya taarifa za Bodi, ambazo haziko mikononi mwake kihalali, kwa waziri mkuu, katibu mkuu wa wizara yake, katibu mkuu kiongozi na PPRA.
  • Kujadili mambo yaliyomo katika Bodi ya Zabuni ambayo bado hayajatangazwa na hivyo kuingilia uhuru wa Bodi.
  • Kushindwa kufuata sheria ya ununuzi kwa kupokea taarifa za malalamiko, kama anavyodai katika barua kwa waziri mkuu, na kukaa na taarifa hizo bila kuziwasilisha kwa Bodi ya Zabuni.
  • Kushindwa kufuata misingi ya utawala bora ya kutofanya au hata kuonyesha upendeleo.
Taarifa zilizopatikana Jumapili jijini Dar es Salaam zinaendelea kumshindilia Masha kwenye tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Inadaiwa kuwa Oktoba mwaka jana, alikwenda Geneva, Uswisi kuhudhuria mkutano wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Wakimbizi ambako baada ya mkutano, alipata wasaa wa kukutana na wenye kampuni ya Sagem Securite.

Imefahamika kuwa Masha aliondoka Dar es Salaam kwa ndege ya kampuni ya Swissair. Mjini Geneva alikutana na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hiyo, Jean Lin Fournereaux hapo 5 Oktoba 2008 kwa muda wa saa mbili kuanzia saa 12 jioni.

Taarifa zimeeleza kuwa Masha alifikia chumba Na. 0306 katika hoteli ya Mandarin Oriental na kutembelea ofisi za Sagem siku iliyofuata, katika eneo la Max Schmidheiny, Mtaa 202 CH 9435 Heerbrugg, mjini Geneva.

Naye Dk. Slaa, mwenye hoja binafsi juu ya waziri Masha kuingilia mchakato wa zabuni, aliiambia MwanaHALISI juzi Jumatatu kuwa kwa kuwasilisha hoja hiyo kwa spika, ametimiza wajibu wake na kwamba anasubiri jibu.

Kanuni za Bunge Na. 47 na 48 zinasema spika akiridhika, hoja binafsi yaweza kuwasilishwa bungeni. “Mpaka sasa hajanijibu,” amesema Dk. Slaa.

Mfumuko wa pilikapilika za kumtetea Masha ulianza pale Dk. Slaa alipoweka wazi kwamba ataomba maelezo bungeni kuhusu waziri kuingilia mchakato wa zabuni ya vitambulisho.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila aliiambia MwanaHALISI juzi kuwa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ilitarajiwa kuendelea na kikao chake jana na kupeleka ripoti yake kwa spika.

Alikataa kusema hatua gani imefikiwa hadi juzi na kuongeza kuwa shughuli za kamati hiyo ni za siri. Mkutano wa 14 wa Bunge unamalizika leo.

Wakati tuhuma dhidi ya Masha kuhusu kuingilia mchakato wa zabuni zingali mbichi, kampuni binafsi nchini imetishia “kumlazimisha kufuata sheria.”

Kampuni ya Power Roads (T) Limited inamtuhumu Waziri Masha kufuta amri ya Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji ya kumwondolea uhalali wa kuishi nchini Mwingereza aitwaye Douglas Hume Claxton.

Mkurugenzi wa Uhamiaji alifuta kibali cha Claxton, Daraja A Na. 018076 cha 30 Oktoba 2007, kwa barua Kumb. Na. 272673/31 ya tarehe 15 Septemba 2008, ambayo MwanaHALISI imeona.

Mkurugenzi amechukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa Claxton alipata kibali cha kuishi nchini kwa kutumia hati batili na iligundulika kuwa baada ya kupatiwa kibali, alikuwa akifanya kazi zisizolingana na kibali chake.

Lakini katika hali inayotia shaka, Waziri Masha alifuta amri hiyo ya Mkurugenzi wa Uhamiaji na badala yake akaruhusu Mwingereza huyo abaki nchini hadi sasa.

Katika barua yake Kumb. Na. DN 272673/32 ya tarehe 15 Oktoba 2008, Mkurugenzi wa Uhamiaji anamweleza Claxton juu ya uamuzi wa waziri.

Anasema, “…waziri ameelekeza kwamba uendelee kuishi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia hati hiyohiyo na kwamba mahakama ndizo zilizomo katika nafasi nzuri ya kushughulikia matatizo na migogoro inayokabili Power Roads (T) Limited.”

Barua ya mkurugenzi imesainiwa na M.P. J. Ulungi kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uhamiaji.

Hoja ya Power Roads kwa waziri, kupitia barua Kumb. Na. proads/08/16 ya 21 Oktoba 2008, ya kupinga hatua yake na kusema watahakikisha wanamlazimisha kufuata sheria, haikujibiwa hadi jana.

Baada ya kuona hawapati majibu, kampuni imemwandikia Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani na kumwomba afikishe nakala ya barua yao ya awali kwa waziri.

Katika barua hiyo, Kumb. Na. roads/09/01 ya 22 Januari 2009, kampuni inamwomba Katibu Mkuu kuwasilisha nakala ya barua yao kwa waziri kwa kuwa yeye, katibu mkuu, “ni mtekelezaji wa utawala bora, mu-wazi na muwajibikaji.”

Barua hiyo imesainiwa na Abba P. Mwakitwange, mkurugenzi na mwenye hisa 51 katika kampuni hiyo.

Mwanahalisi
 
Ungejiajiiri hata kazi ya kuzibua vyoo majumbani, mahotelini na Ofisi za umma ungeongeza kipato zaidi ya hii kazi unayotumia nguvu nyingi kwa ujira mchache kisha inaishia kudharauliwa.
 
Back
Top Bottom