Kwa hili madiwani wa Temeke mmechemsha

Giro

JF-Expert Member
Feb 9, 2009
359
22
Beda Msimbe
Daily News; Monday,March 16, 2009 @09:00

Barabara ya Kilwa ambayo imejengwa njia mbili inakaribia kumalizika huku kituo cha mabasi kikubwa katika barabara hiyo cha Mbagala Rangi tatu kikiwa hakina mwelekeo wowote ule wa msingi.

Tetesi ambazo zinazunguka katika maeneo hayo ya Mbagala Rangi Tatu na hii nadhani ni kweli, madiwani wa Temeke na wataalamu wao wameamua mahali lililopo soko katika eneo hilo ndiko kunakofaa kuwa na kituo cha mabasi.

Wakati fulani unashangaa uwezo na busara za watu katika kufanya mipango miji na maendeleo yake hasa kwa kuzingatia ukuaji wa mji na pia maeneo yanayozunguka mji wenyewe.

Lakini kwa mawazo yangu mimi busara, akili katika hili haikufuatwa, bali tamaa ndiyo ilitangulizwa mbele katika uamuzi huu ambao kimsingi mimi nauona kama umejaa ubabaishaji.

Kwa eneo kama la Rangi Tatu ambalo kwa sasa linapokea magari yote ambayo yanatoka mpaka Mkoa wa jirani wa Pwani ukiachia mbali mabasi yanayotoka maeneo mbalimbali ndani ya Mbagala yenyewe ambayo ni kubwa kama wilaya kubadili soko kuwa kituo cha mabasi ni dalili ya ufidhuli wa akili, na hili si tusi.

Nasema si tusi kwa sababu miaka mitano ijayo Mbagala Rangi Tatu itapokea magari mengi kutoka katika Wilaya inayokuja kwa kasi kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi ya Mkuranga.

Ukiangalia pia mipango ya Serikali Kuu kuhusiana na Mkuranga na wazo la kujenga moja ya viwanja vikubwa vya ndege nchini, mtu ataiangalia Mbagala Rangi Tatu kama sehemu inayohitaji Bus Terminal na wala si Bus Stop.

Nasema ni Bus Terminal wala si Bus Stop kwa sababu mazingira yanaonyesha wazi kuwa panahitajika eneo kubwa la mazingira ya Bus Terminal kama inavyostahili kuwa na katika hili eneo la soko ni eneo si tu dogo bali la kulazimisha.

Mbagala Rangi Tatu ina sehemu kubwa ya kuweza kujenga Bus Terminal ambayo inaweza kuchukua mabasi ya kawaida hata mia nane ikiwa na ukubwa sawa na Ubungo Bus Terminal na ipo sehemu nzuri tu ambapo kuingiza na kutoa mabasi hakuhitaji ufundi mkubwa.

Eneo hilo ambalo wajanja walishataka kuliuza kwa Sh milioni 800 awali tunaambiwa lilikuwa ni miliki ya UDA kama ilivyokuwa Ubungo. Sehemu hii wapo wajanja wengi wameikomalia kama yao na wanataka kuifanyia kazi ambayo ni ya kijanja zaidi.

Eneo hili ambalo lipo mkabala na Kanisa la Kristo, mbele ya Shule ya Kimataifa ya St Mary's ni ardhi ambayo bado haijaendelezwa sana na ingeliweza kufaa kuwa terminal na pia kitega uchumi bora kabisa kwa Wilaya ya Temeke ambayo inasuasua katika vitega uchumi vyake.

Lakini madiwani na mkurugenzi wake wameamua kuchukua mahali ambapo mimi napaona padogo na pia kuleta usumbufu kwa watu waliopo pale bila sababu na kisha unatazama watu wataingizaje mabasi yao na kuyatoa.

Mathalani watu wanaokwenda Kiburugwa njia ya awali ambayo imefikiriwa kutumiwa kuingiza mabasi stendi hiyo inayofikiriwa,(sokoni) inapita karibu kabisa na njia ya bomba la mafuta na ukweli huu unatisha. Nasema unatisha kwa sababu hakuna mtu anayetaka kuukubali ukweli kuwa barabara ile iko katika eneo lisiloruhusiwa na tumefumbia macho.

Pili kutahitaji ubunifu wenye gharama kubwa kuzungusha mabasi katika eneo hilo na kuingia katika barabara kuu wakati kwa kutengeneza terminal mbele ya St Marys eneo hilo linalodaiwa kuwa la UDA kuingia katika eneo hilo ni rahisi na kutoka kwani ni kama muondoko wa sambusa.

Nini kinawapeleka madiwani na wapanga miji kufikiria leo badala ya kufikiria kesho na kesho kutwa, mimi sijaelewa. Na kwa kuwa sheria ya ardhi inatoa mamlaka makubwa kwa serikali kubadili matumizi kwa kuzingatia hali halisi ya sasa na ijayo na ili tusije tena kubomoa eneo hili ambalo wajanja wanataka kuliuza kwa Sh milioni 800 linafaa kujengwa kituo na kumaliza uzia.

Mimi sielewi kama kweli tunahitaji fundi kutoka mbinguni kutuambia kwamba pale sokoni hapatufai kwani na mtu akinunua kiwanda cha Biasi itakuwaje hasa? Kiwanda hiki ingawa hakitumiki kwa sasa kilijengwa kwa ajili ya kutengeneza kioo.

Mimi naamini historia itakuja kutusuta kwa mara nyingine tena, baada ya makosa mengi katika mipango miji yetu na hili la Mbagala Rangi Tatu litakuwa lingine tena ndani ya vurumai za kuendekeza 'mkato' badala ya ukweli wa maslahi ya umma.

Je tunahitaji tena kupelekwa shule kujua kwamba tunatakiwa kutumia akili zetu kwa kuangalia mbele zaidi na wala si leo, au kila Rais akiingia madarakani aje na dizaini ya bomoa hapa kwani tumekosea pale? Nini hasa maana ya kuwa na madiwani na maofisa mipango wasioangalia ukweli kwa kutumia akili yao na kusikiliza ushauri kwa waliokuwapo.Tafakari............
 
Back
Top Bottom