SoC03 Kutokuwajibika kwa wanaume wakati wa uchumba ni chanzo cha migogoro ya ndoa

Stories of Change - 2023 Competition

mkulu senkondo

JF-Expert Member
Feb 19, 2017
1,834
3,530
UTANGULIZI.
Kwa miaka mingi, migogoro baina ya wanandoa imekuwepo, hata hivyo, kwa siku za karibuni, migogoro ya wanandoa imeongezeka maradufu. Migogoro ya ndoa huleta matokeo hasi katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla kama vile; kutengana kwa wanandoa, kupigana na kusababishiana ulemavu pamoja na mauaji. Athari hizo hasi za migogoro ya ndoa ni mbali na matatizo ya kisaikolojia, kukata tamaa na hata kuporomoka kiuchumi.


Sababu zinazochochea migogoro ya ndoa.
Changamoto za uaminifu, kutokujali, tofauti za kiitikadi, kujisahau na kutotimiza wajibu miongoni mwa wanandoa ni miongoni mwa sababu chache kati ya nyingi zinazochochea migogoro baina ya wanandoa.

Mbali na sababu tajwa hapo juu, mwandishi anaamini kwamba, kwa kiwango kikubwa, mbegu ya migogoro ya ndoa inasababishwa na wanaume (wakuu wa taasisi ya ndoa) katika kipindi cha uchumba ama kuchunguzana kabla ya ndoa.

Picha kwa msaada wa mtandao.

"Je, ni kwa namna gani wanaume hawawajibiki ipasavyo katika kipindi cha uchumba kuwasoma na kuwafahamu wapenzi wao ili kuepuka migogoro ya ndoa hapo baadae?"

hapa chini ni hoja 7 kuthibitisha namna wanaume wasivyowajibika wakati wa uchumba, kitendo kinachosababisha migogoro ya ndoa hapo baadae na suluhu zake;

1. Kufuatilia muundo na mtindo wa maisha ya familia ya muolewaji.
Hili ni eneo la kwanza ambalo wanaume wengi wanafeli. Ukweli ni kwamba, mtindo wa maisha ya mama wa muolewaji una athari ya moja kwa moja kwa mtoto wake wake wa kike. Katika familia ambayo muundo wake mama ndio msemaji wa mwisho, kuna uwezekano mkubwa mtoto wake akarithi ama kuichukua tabia hiyo. Kama mama anadanga na kuruka majoka, kuna uwezekano mkubwa wa mtoto kuichukua tabia hiyo. Hali kadhalika, mtazamo wa mama juu ya wanaume (akiwemo mumewe) unaweza ukamuathiri binti yake.

Hivyo, ni muhimu kwa mwanaume muoaji kuwajibika kwa kufuatilia mtindo na muundo wa familia ya muolewaji ili kujua ni tabia na vitabia vipi hatoweza kuvivumilia na mwisho kufikia hitimisho kama anaweza kuendelea na mchakato au la!


2. Kupima utiifu na uwezo wa kufuata maelekezo wa muolewaji.
Baadhi ya wanaume huwa legelege na kupewa jina la waelewa mwanzoni mwa mahusiano. Kitendo hicho huwafanya wanawake kutokuwatii ama kutozingatia maagizo yao ipasavyo tangu siku za mwanzo za mahusiano na uchumba. Kwa kuchelea huko, baadae kwenye ndoa wanataka waoneshe uwezo wa kuongoza na kutoa amri na maelekezo kwa wake zao, kitendo ambacho mwanzoni hawakukifanya. Matokeo yake, mwanamke anahisi kama anaonewa ama kupelekeshwa hali inayosababisha migogoro ndani ya ndoa.

Kuliepuka hili, ni wajibu wako mwanaume kuonesha rangi yako kwa kusimama kwenye misingi ya wewe kuitwa mwanaume tangu mwanzo wa mahusiano. Ni muhimu sana mwanaume kuupima utiifu wa mchumba wako kwako kabla ya kuchukua uamuzi wa kumuoa.

picha kwa msaada wa mtandao.

3. Kuendana na kurandana.
Waswahili wanasema ndege wafananao huruka pamoja. Kwa sababu ya upofu wa mapenzi na kupenda kupita kiasi, baadhi ya wanaume huwaoa watu wasioendana nao. Huwa inatokea mara nyingi, baba amenyooka hana mambo mengi, vijana wa kileo wanasema hana mbambamba! wakati huo huo mwanamke anapendelea kuendekeza uswahili wa kuhudhuria vigodoro na vijiwe vya umbea! pia, huwa inatokea mama ni mchamungu mzuri wakati baba ni mlevi na mtu wa kuruka viwanja. Matokeo yake, migogoro inakuwa sehemu ya ndoa ya mtindo huo kwa sababu watu hao hawaendani.

Kuliepuka suala hilo, mwanaume unapaswa kufuatilia ni kwa namna na kwa kiwango gani mkeo mtarajiwa mnaendana kitabia, kimtazamo, kifalsafa, vipaumbele na mengineyo yanayofanana na hayo.

picha kwa msaada wa mtandao.

4. Kufuatilia utofauti wa kiutamaduni na kimazingira.
Chanzo cha baadhi ya migogoro baina ya wanandoa ni tofauti za kiutamaduni na kimazingira. Hii hutokea sana kwa wanandoa ambao mazingira ya makuzi na mtindo wa maisha ya kila siku hutofautiana. Mfano, kuoa mke zaidi ya mmoja ni jambo lisilokubalika katika utamaduni wa jamii za Wamarekani lakini huwa wanaukubali ushoga. Hiyo ni tofauti katika jamii za Waswahili ambapo ushoga haukubaliki lakini ni kawaida kabisa mwanaume kuoa mke zaidi ya mmoja!
Mwanaume wa pwani kumuolea mke wa pili mwanamke wa bara inaweza kuzua sintofahamu. Hiyo, ni tofauti na mwanamke wa mwambao ambaye katika mazingira yake amezoea kuona matukio ya namna hiyo.


Inawezekana utamaduni na mazingira ya kabila au familia ya muolewaji visiendane na muoaji, kitendo kinachoweza kuja kusababisha migogoro ambayo ingeweza kuepukika. Hivyo, ni wajibu wa mwanaume Kufuatilia na kupima aina ya utamaduni na mazingira ya mkewe mtarajiwa ili kufahamu ni kwa kiwango gani utofauti baina yao unavyoweza kuleta shida na namna nzuri ya kukabiliana na suala hilo.

picha kwa hisani ya mtandao.

5. Kiwango cha urafiki na mawasiliano.
Kitaalamu, mwanaume anatakiwa amuoe mwanamke ambaye anaweza kuzungumza nae wakasikilizana. Mawasiliano ya kuridhisha na ya mara kwa mara kwa wapendanao ni ufunguo muhimu kwa ndoa yenye afya baadae. Baadhi ya wanaume hawajishughulishi sana na hili badala yake hukijikita zaidi kwenye kutoa mahitaji.


Bila ya kujali utofauti wa kipato, kiumri, kiitikadi, kiimani au vinginevyo, mawasiliano yenye tija ni muhimu sana. Inashauriwa sana mwanaume kufuatilia kwa umakini kama anayemuoa anaweza kuwa rafiki yake wa kwanza na wa kweli. Hii inasaidia sana kupunguza tofauti za kimakuzi na kimazingira ikizingatiwa wahusika wamekutana ukubwani. Kwa kulizingatia hilo, migogoro mingi ya ndoa inaweza kuepukwa.


6. Marafiki wa mke mtarajiwa.
Kampani ya mwanamke au marafiki zake wanao mchango mkubwa sana kuitengeneza tabia ya mke mtarajiwa. Na hii inatokana na ukweli kwamba, wanaoingiliana kijamii na muolewaji wanayo athari chanya juu ya mtazamo, tabia, matarajio na namna ya kufikiri kwa kuwa miongoni mwao hukubalika zaidi na muolewaji. Hivyo, kabla ya kumuoa ni muhimu sana kwa mwanaume kuwajibika kwa Kufuatilia na kutambua aina ya watu wanaomshikia akili na kumshauri mke wako mtarajiwa.



7. Kiwango cha kujali, kupenda na heshima.
Katika mifumo yetu ya kijamii, mwanamke ndie anayefuatwa hivyo anaweza kumkubali mwanaume kwa kuwa anakidhi viwango na matarajio mbali na kumpenda. Hata hivyo, hiyo haimaanishi kuwa asimheshimu mumewe. Mwanamke anaweza akampenda mumewe mbele ya safari na hilo linathibitishwa na UN Data za mwaka 2021 ambapo katika kila wanawake 100 waliofunga ndoa 52 kati yao wameolewa na wanaume ambao sio wa ndoto zao! hiyo haimaanishi kuwa hawaishi, wanaweza kuishi na waume zao kwa sababu ya uwezo wa kujali, kutunza familia na kumheshimu mwanaume. Kwa mantiki hiyo, mwanaume anawajibika kufuatilia na kumjua mwanamke anayeweza kujali familia yake na kumheshimu. Hii itasaidia sana kupunguza migongano na mizozo ndani ya ndoa hususan katika kipengele cha malezi.



Mwisho wa andiko letu, karibuni kwa maoni, mtazamo, hoja na hata kukosoa.
 
Back
Top Bottom