Kunani nyuma ya diplomasia ya Mzee Mwinyi? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kunani nyuma ya diplomasia ya Mzee Mwinyi?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mbonea, Oct 2, 2009.

 1. Mbonea

  Mbonea JF-Expert Member

  #1
  Oct 2, 2009
  Joined: Jul 14, 2009
  Messages: 640
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33


  [​IMG]
  Godfrey Dilunga​
  [​IMG]
  UNAPOZUNGUMZIA uwezo wa kiuongozi wa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, yapo masuala muhimu ambayo ni lazima kuyataja, kuyatafakari na hata kuhoji. Masuala kama kifo cha Azimio la Arusha, na baadaye soko huria lililogeuka soko holela, likiongozwa na kanuni za kibepari, zilizoshamiri kutokana na serikali kwenda ‘likizo’ kwa wakati huo.
  Kwa mfano, utaweza kuhoji ni kwa nini Mzee Mwinyi akiwa mkuu wa nchi aliridhia kufutwa kinyemela (badala ya kurekebisha) Azimio la Arusha, bila kutambua kuwa ni azimio lililokuwa dira ya viongozi na taifa. Azimio lililobainisha miiko ya uongozi na wakati huo huo, kuwawezesha umma kutambua kwa haraka, kiongozi gani amekiuka miiko husika kwa kutazama matendo yake.
  Pia utaweza kukumbuka msukosuko dhidi ya aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani, Augustine Mrema, bila kusahau mirindimo ya kashfa ya Loliondo, iliyovaliwa njuga na mwanahabari, Stanley Katabalo.
  Hata hivyo, upande mwingine utamwona Mwinyi kama mkuu wa nchi, akivumilia na kufungua milango na madirisha ya uchumi.
  Katika pande zote hizo mbili za uongozi wa Mwinyi, yapo mambo yaliyomchukiza Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambayo pia, bila shaka, yaliwachukiza Watanzania wengi. Mfano, serikali kwenda ‘likizo’ mwishoni mwa muhula wa pili katika awamu hiyo, kiasi cha kushindwa kukusanya kodi kwa wafanyabiashara wakubwa, huku Mwalimu akibaki kutafsiri kuwa hiyo ni sifa ya “viji-serikali corrupt.”
  Lakini pia jambo jingine lililomchukiza Mwalimu Nyerere, mtangulizi wa Mwinyi Ikulu, ni serikali kukimbizwa mchakamchaka na Benki ya Dunia, pamoja na wafadhili wengine.
  Kwa muhtasari, Mwinyi hakuwa kiongozi mwenye mikakati madhubuti iliyofuta wasiwasi miongoni mwa Watanzania kuhusu uhakika wa mustakabali wa taifa lao, kiasi cha kumlazimu Mwalimu Nyerere (Rais wa kwanza wa Tanganyika na Tanzania), kuhimiza viongozi wazingatie sheria kuongoza nchi, na si mawazo au ushauri wa wenzi wao.
  Ni kweli, hakuna kiongozi asiye na kasoro kiutendaji, akiwamo Mwalimu Nyerere kama ambavyo binafsi alivyowahi kukiri. Hata hivyo, kiwango cha makosa hutofautiana. Kwa mfano, Baba wa Taifa, pamoja na kufeli katika uchumi, lakini hakuvumilia vigogo wala rushwa na hakuwahi kuhusishwa na kashfa za rushwa.Kwa viongozi wenzake, ushahidi wa mazingira ulitosha kuwawajibisha.
  [​IMG]

  Mzee Ali Hassan Mwinyi
  Nimeanza kumzungumzia Mzee Ali Hassan Mwinyi, kwa kuwa ndiye kinara wa mjadala wa leo.
  Akiwa katika kata ya Ndungu, jimbo la Same Mashariki, mkoani Kilimanjaro, Septemba 24, mwaka huu, alitoa kile ninachoweza kuita msimamo wake kuhusu ufisadi, kwa mara ya kwanza.
  Katika msimamo wake, Mwinyi anafikisha katika jamii ujumbe wa aina tatu. Mosi, ili kiongozi tumtambue kuwa ni fisadi, si lazima athibitishwe na Mahakama. Maana yake ni kwamba, hata ushahidi wa mazingira unatosha kwa jamii kumweka mhusika katika kundi la mafisadi.
  Pili, kiongozi anayebainika kuwa fisadi (kwa ushahidi wa mazingira au vinginevyo) hana wito au kipawa cha uongozi na hivyo basi, atakuwa amepata nafasi hiyo kwa kujipenyeza tu. Amekuwa kiongozi kwa bahati mbaya, asiye na sifa 10 za uongozi.
  Sifa ambazo kwa mujibu wa msimamo wa Mzee Mwinyi ni kipawa, asiwe mchoyo, mwenye huruma kwa anaowaongoza (si mafisadi au viongozi wenzake), mpenda watu, mkarimu, awatendee wengine kile anachopenda kutendewa, mpenda maendeleo, awe na uchungu na mateso ya wananchi, awe mkweli, ajali shida za wananchi.
  Sehemu ya tatu ya ujumbe ni kwamba; kama katika safu za viongozi waandamizi nchini kuna waliojipenyeza kwa bahati mbaya na kisha kuumbuliwa kwa ufisadi wao, kama taifa na hususan kama wapiga kura, Mzee Mwinyi anatuwajibisha kwa kututaka tuwang’oe.
  Tuwang’oe si kwa mapanga, bakora au kuchoma moto mali walizopata kwa njia ya ufisadi la hasha, tuwang’oe kupitia sanduku la kura na kama tukishindwa kufanya hivyo na kuwapa nafasi tena ya kubaki kwa bahati mbaya madarakani, itakuwa zamu yetu kushughulikiwa kwa kasi na hasira maradufu.
  Msimamo wa Mzee Mwinyi unatujengea upeo wa tunakopaswa kuelekea, ingawa pia upeo huo uko mbali nasi. Rais huyu mstaafu kwa msimamo wake huo, unatuwezesha kutambua rasmi kwamba; viongozi waliochaguliwa kwa bahati mbaya wawekewe ukomo.
  Kwa msimamo huu, Mzee Mwinyi anajitambulisha upya kwa Watanzania. Amekurupuka na kulikimbia genge la ufisadi. Genge linaloachiwa kumega keki ya taifa ovyo, kwa masharti kwamba; kipenga cha uchaguzi mkuu kinapopulizwa ni lazima wachangie fedha ili chama kishinde, kibaki madarakani ili kulinda usalama wao uliobatizwa jina la “usalama wa taifa.”
  Sina hakika, labda anasahihisha makosa yake alipokuwa Rais na hasa aliposhindwa kuwaeleza ‘rafiki’ zake na wakamuelewa kuwa; Ikulu ni mahali patakatifu, na si pango la walanguzi.
  Ali Hassan Mwinyi wa sasa kama ataendelea hivi atakuwa amejisogeza karibu zaidi na walalahoi. Mbele ya walalahoi, atakuwa amejitambulisha upya kwamba; pensheni anayopata kutokana na kodi zao inamtosha, hahitaji ufadhili wa kifisadi.
  Mara kwa mara tumesikia baadhi ya viongozi waandamizi CCM na serikalini, wakitaka wananchi kutaja kwa majina mafisadi, licha ya ukweli kuwa kwa kuzingatia madaraka yao, wanawajua hao mafisadi kwa majina na kwa ushahidi.
  Ali Hassan Mwinyi amekwenda kinyume nao. Amekwenda kinyume cha mawaziri na makada wa CCM, akiwamo Katibu Mkuu wa chama hicho, wanaotaka wananchi wataje majina na kuwapa ushahidi, bila kujali kuwa wao ndiyo viongozi wanaowajibika kutaja majina hayo kwa wananchi.
  Mwinyi amekwenda kinyume. Kwa tafsiri ya msimamo wake, anampinga Makamba, anayeamini fisadi ni aliyethibitishwa na Mahakama tu, bila kutambua kuwa hata ndani ya Mahakama kuna mtandao wa mafisadi, kama ilivyo katika CCM na taasisi nyingine nyeti.
  Mwinyi amepingana na Makamba, akizingatia ukweli kwamba; wakati mwingine ni vigumu kumthibitisha fisadi ndani ya wigo wa Mahakama, pengine kutokana na Mahakama kutokuwa na unadhifu wa kimaadili kiwango cha kuridhisha.
  Anajua kuwa mfumo wa Mahakama umezongwa na malalamiko, ingawa pia ndani ya Mahakama hizo wapo majaji, mahakimu na maofisa wengine waadilifu, wazalendo, watenda haki, wanaodondosha machozi ya uchungu dhidi ya fursa wanazopewa mafisadi kutenda uovu.
  Mwinyi anajua kwa mfano, ni dhahiri kuwa wapo mafisadi waliofaidika na mabilioni ya noti za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia kampuni ya Kagoda, lakini wamevuruga ushahidi, na wakati huo huo wamekubali kurejesha mabilioni hayo.
  Kwa kutambua hayo yote, Mwinyi kwa tafsiri ya msimamo wake, anatueleza; fisadi si lazima athibitishwe na Mahakama, bali hata ushahidi wa mazingira unaweza kumthibitisha. Hivyo, kama ni viongozi tunaweza kuwakataa kwa kuzingatia ushahidi wa mazingira, na si hukumu ya Jaji au Hakimu.
  Ili kuendelea vema na mjadala ninukuu msimamo wa Mwinyi akisema; “Uongozi ni fani na kipawa, mtu aliyekosa vitu hivyo hawezi kuwa kiongozi mzuri na hata kama atajipenyeza kwa bahati mbaya, ndo hao mnaosikia kuwa ni mafisadi na wanaoingiza nchi katika mikataba mibovu.”
  Kwa maelezo hayo, Rais huyo mstaafu ambaye ni mlezi wa mfumo wa vyama vingi nchini ametutajia majina ya viongozi mafisadi. Viongozi mafisadi ambao wamejipenyeza kwenye uongozi kwa bahati mbaya.
  Ndiyo, Mwinyi ametumia diplomasia tu, lakini ukweli ni kwamba ametutajia majina ya viongozi mafisadi na hasa anapotamka ni wale walioingiza nchi katika mikataba mibovu. Ili kuwajua kwa majina yao, tafakari viongozi wenye kashfa zilizotokana na mikataba mibovu.
  Fungua fikra na uwezo wako wa kutafakari utasikia sauti ya Mzee Mwinyi ikitaja jina moja baada ya jingine na utatambua nani ni mafisadi na ambao wameingia kwenye uongozi kwa bahati mbaya.
  Fungua fikra zako, tafakari viongozi gani wamewajibika kutokana na mkataba wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond na baadaye Dowans? Mkataba ambao, wanasheria wa kampuni ya kimataifa ya Rex-Attorneys waliishauri serikali iufute kwa kukosa nguvu za kisheria.
  Sumbua kidogo fikra zako, rejea ripoti ya Kamati Teule ya Bunge, iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe na utabaini, orodha ya viongozi walioshauriwa kuachia ngazi au kuwajibishwa.
  Katika mikataba ya madini, ambayo hadi Rais Jakaya Kikwete alilazimika kuunda kamati ya Jaji Bomani, kutazama upya maslahi ya nchi ndani ya mikataba husika, nako utabaini orodha ya viongozi mafisadi, waliokwaa uongozi kwa bahati mbaya.
  Lakini ukiacha mikataba ya Richmond na madini, ipo mikataba mingine kama TICTS, TRL bila kusahau mikataba ya ununuzi wa rada na hata ndege ya rais. Tafakari, majina ya vinara wa mikataba hiyo.
  Naheshimu diplomasia aliyotumia Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ingawa pia namshauri katika masuala ya ufisadi, aache diplomasia. Yeye ni Mtanzania aliyewahi kushika madaraka ya juu nchini, aige mfano wa Mwalimu Nyerere aliyetumia fursa yake kukosoa bila kusita.
  Rais Jakaya Kikwete anapaswa kutafakari kwa kina msimamo huu wa Mzee Mwinyi, kwamba wapo viongozi waliojipenyeza kwa bahati mbaya. Viongozi wa namna hii, hawastahili kurudi madarakani.
  Atambue kuwa, viongozi wa namna hii wapo kwa sasa serikalini, kwenye vikao vikuu vya CCM ikiwamo Halmashauri Kuu ya chama hicho. Wamemzunguka, ndiyo hao baadhi wanatoa maagizo kwa niaba yake.
  Kama Rais Kikwete atapuuza mtazamo huu wa Mzee Mwinyi, ni dhahiri kuwa jamii itamtambua kuwa naye ni kati ya viongozi waliojipenyeza kwa bahati mbaya kwenye uongozi, na wananchi watafikiria hatua za kumchukulia katika Uchaguzi Mkuu 2010.
  Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
  [​IMG]
   
 2. Ngida1

  Ngida1 JF-Expert Member

  #2
  Oct 2, 2009
  Joined: Aug 25, 2009
  Messages: 554
  Likes Received: 33
  Trophy Points: 45
  "Katika msimamo wake, Mwinyi anafikisha katika jamii ujumbe wa aina tatu. Mosi, ili kiongozi tumtambue kuwa ni fisadi, si lazima athibitishwe na Mahakama. Maana yake ni kwamba, hata ushahidi wa mazingira unatosha kwa jamii kumweka mhusika katika kundi la mafisadi".

  Kutokana na hayo ya hapo juu inaonesha wale wanaotueleza kuwa Warioba nae ni fisadi kupitia hio kampuni ya Mwananchi Gold basi hawajakosea!
  Hii nchi kweli imejaa mafisadi na yule aliesema kuwa inaliwa nyuma na mbele 24 hours hakukosea pia!
   
Loading...