Kuna mambo Paul Makonda anapitia

Kuna mambo Paul Makonda anapitia

kalulukalunde

JF-Expert Member
Joined
May 27, 2016
Posts
1,056
Reaction score
1,086
DSCF0788-1024x682.jpg



Naungana na Watanzania wote kutoa pole kwa familia ya Komredi Kingunge
Ngombale-Mwiru, kutokana na kifo cha mwamba huo wa siasa katika Taifa
letu. Mzee Kingunge atakumbukwa kwa umahiri wake wa kujenga hoja na weledi
aliojaaliwa na Mwenyezi Mungu, hata akaweza kuwa lulu na moja ya injini
muhimu katika ustawi wa Taifa letu.

Bahati mbaya watu wa aina yake wanapofariki dunia mara moja jamii
huwasahau. Tumeona juhudi nyingi za kuwaenzi waasisi wa Taifa letu kwa
kuyapa majina majengo, madaraja, barabara na kadhalika. Naamini katika
hili mamlaka zinazohusika, kila moja kwa wakati wake, zitaona namna
nzuri ya kumuenzi mzee huyu. Kwa mfano, inaweza kutazamwa barabara
moja yenye hadhi ikapewa jina la shujaa huyu. Lakini lililo kubwa zaidi ni kwa vyama vya siasa na wanasiasa kuyarejea maandiko ya nguli huyu ili yawasaidie katika ujenzi wa vyama imara vyenye maono ya kuwaletea wananchi maendeleo. Kumweleza Mzee
Kingunge kunahitaji kurasa nyingi mno. Itoshe kumwombea pumziko jema
huko alikotangulia.

Wiki iliyopita, kulikuwa na matukio mawili mengine yaliyowagusa makabwela katika Jiji la Dar es Salaam, na bila shaka na sehemu nyingne nchini. Tukio la kwanza lilikuwa ni la Wiki ya Sheria, na la pili ni lile lililotangulia – la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda – aliyewakaribisha wananchi wenye malalamiko ya kudhulumiwa haki zao.
Hili la Wiki ya Sheria sina mjadala nalo sana kwa sababu limekuwa tukio la kila mwaka.

Wananchi hujitokeza kupata msaada wa kisheria kwa mashauri yanayowagusa. Kama ilivyo ada, Rais wa Jamhuri ya Muungano hupata wasaa wa kueleza aliyonayo. Hotuba zake mara kadhaa zimeibua mijadala. Wapo wanaodai amekuwa akivuka mpaka kwa kuingilia muhimili mwingine! Lakini wapo wanaoona yuko sahihi.

Rais ndiye kiongozi mkuu wa nchi (dola). Dola inaundwa na mihimili mitatu – Utawala (Rais), Bunge (Spika) na Mahakama (Jaji Mkuu). Pengine kwa kuwa Rais anachaguliwa na wananchi, hii inaweza kuwa sababu ya kumfanya aingilie baadhi ya mambo ambayo wakati mwingine yanatafsiriwa kuwa ni kuingilia mihimili mingine.

Kufaulu au kufeli kwa dola yoyote kunaweza kusababishwa na kasoro kwenye muhimili mmoja, miwili, au yote. Lakini lililo kubwa ni kuwa muhimili wa Utawala ndiyo wenye dhima ya kutekeleza yale ambayo wananchi wangependa kuona wakitendewa. Rais anachaguliwa na wananchi.

Jaji Mkuu anateuliwa, na Spika anachaguliwa na wabunge. Kwa wote hawa watatu Rais ndiye aliyeko kwenye kikaango zaidi hata kama udhaifu utakaoikabili dola unaweza kuwa umesababishwa na ama Bunge, au Mahakama.

Mathalani, wananchi wakikosa dawa au chakula Mahakama hawawezi kuilaumu Mahakama. Wanafunzi wakikosa huduma za kuwawezesha kusoma vizuri hawalishutumu Bunge (labda kama limekataa kuridhia bajeri).

Watumishi wa Bunge, Mahakama au Serikali wanapokosa mishahara wa kulaumiwa ni Utawala. Huu mzigo wote wa kuibeba dola nadhani ndiyo unamfanya wakati
mwingine, Rais, ama kwa kukusudia, au kwa kutokusudia, ajikute anatoa maelekezo yanayotafsiriwa tofauti. Kama alivyowahi kusema yeye mwenyewe, yote inaweza kuwa mihimili, lakini upo wenye mzizi mrefu zaidi.

Hatua hii inanipeleka moja kwa moja kujadili uamuzi wa Makonda wa kuwakaribisha makabwela wanaolia na kutaabika kwa kudhulumiwa haki zao. Yamekuwapo mambo kadhaa ambayo nimekuwa sikubaliani na Makonda, lakini imeniwia vigumu kumpinga katika hili alilolifanya kwa wanyonge wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Kwenye hili tunapaswa kuweka pembeni lawama za kuhoji kuwa yeye ni nani hata aweze kuwaita watu wamweleze kilio chao cha kudhulumiwa. Tunaweza kusema hana mamlaka ya kubadili uamuzi uliotolewa na Mahakama au mamlaka nyingine. Tunaweza kuhoji kama kweli ana nguvu au mamlaka ya kutengua adhabu zilizozipendelea benki, na kadhalika.

Vyovyote iwavyo, hatua ya Makonda kuwakaribisha maskini waliodhulumiwa ni ya kupigiwa mfano. Inatusaidia kwenda mbali zaidi kutambua ukubwa wa tatizo la upatikanaji haki katika nchi yetu. Kwenye shughuli hii ya Makonda, lawama nyingine zimeelekezwa kwa Mahakama, Polisi na wanasheria (mawakili). Wananchi wengi wameonesha vielelezo kuthibitisha namna walivyodhulumiwa kwa msaada wa Mahakama,
wanasheria au Polisi.

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba tunaweza kumpuuza Makonda kwa hatua yake ya kuwaita maskini hao waliodhulumiwa, lakini hatuna budi kukiri kuwa tukio hili limetusaidia kujua ukubwa wa tatizo la dhuluma katika Mkoa wa Dar es Salaam na kwa hakika kwa nchi nzima.

Sisi tunaofanya kazi katika vyumba vya habari tunaletewa malalamiko mengi mno na wananchi waliodhulumiwa nyumba, mashamba, magari au mali nyingine. Yapo matukio mengi mno. Nakumbuka tukio moja niliwahi kuwapeleka wananchi kwa Jaji Mkuu wa wakati huo, Augustino Ramadhani.

Huyu ni mmoja wa majaji wanyenyekevu. Wananchi walionifuata, walikuwa wamehangaika kwa miaka minne kumfikia Jaji Mkuu bila mafanikio. Walikuwa na fedha zao – milioni kadhaa – zilizokuwa zimekaliwa katika Ofisi ya Msajili. Nilipowasikiliza, nikaona ile si habari ya kuiandika, bali ya kuwawezesha wamwone Jaji Mkuu. Nikampigia simu. Akapokea. Nikamweleza kisa cha maskini hao.

Akaagiza wamwone ofisini kwake baada ya siku moja. Nikawaeleza. Hawakuamini. Mmoja akasema, “Tumehangaika miaka minne bila mafanikio wewe leo unasema tumwone
keshokutwa? Sidhani kama tutafanikiwa, tutaenda tu lakini siamini kama
kuna lolote la maana tutakalopata.”

Haya maneno yalionesha namna walivyokata tamaa, na kwao walichoamini ni habari hiyo iandikwe ili Rais aisome na kisha awasaidie. Kweli, siku ilipowadia walifika ofisini kwa Jaji Mkuu. Akawapokea na kuwasikiliza. Hapo hapo akawafurusha hao waliokalia haki ya
wananchi hao kwa miaka zaidi ya mitano! Akawahakikishia kuwa watapata haki yao. Wale watu wakarejea ofisini kwangu siku hiyo hiyo. Mmoja alipofika akanipa mkono, lakini hakujibu kitu. Akawa ameufunika uso wake. Alikuwa akilia (kwa furaha).

Hoja ikawa kwamba mimi ni nani hata nimewawezesha wamwone Jaji Mkuu ndani ya muda mfupi? Nikawajibu kuwa tunao viongozi wazuri wasiopenda kuona watu wakitaabika, lakini shida inaletwa na wachache walio kwenye nafasi nyeti!

Baadaye wananchi wale wakalipwa fedha zao. Hawakurudi kwangu, lakini nikawa nimefarijika kwa kuona kuwa nimetekeleza wajibu wangu. Maskini wamepata haki yao. Ofisini kwetu tuna mwandishi mmoja mahsusi kwa ajili ya kupokea na kufanyia kazi malalamiko ya wananchi waliodhulumiwa ardhi, nyumba,
mashamba na kadhalika. Malalamiko ni mengi sana. Tunawashukuru baadhi
ya viongozi na watendaji kwenye mamlaka za utoaji haki ambao mara kadhaa tumewapelekea vilio vya maskini hawa na wakawasaidia.

Moja ya vitu vinavyowaumiza sana maskini katika nchi yetu ni huu mfumo
wa kisheria wa kufuta kesi kwa njia za ‘ujanja ujanja’ (technicalities).

Kwa mfano, mwananchi aliyedhulumiwa shamba anamfuata wakili. Yule wakili anaandaa maelezo ya kesi ya mlalamikaji, lakini badala ya kutumia kwa mfano kifungu 12, anaweza kuandika 22. Wanapokwenda kwa hakimu au kwa jaji, wakili wa upande wa pili
anawasilisha hoja ya kutupwa kwa kesi kwa sababu kifungu kilichotumiwa na upande wa mlalamikaji si kilichopo kwenye sheria. Kesi nyingine zimetupwa kwa njia hii. Kuna madai kwamba baadhi ya mawakili huwa ‘wana-conspire’ na upande wa pili ili kuvuruga kesi.
Tufanye nini? Hili suala baadhi ya Mahakimu na Majaji wameliona.

Wamelilalamikia lakini wamefungwa mikono kwa sababu wao kazi yao ni kutafsiri sheria. Tunapofika hapo ndipo tunapowageukia wabunge wetu na kuwaomba watazame upya hii kitu ‘technicalities’ ili warekebishe sheria. Kwa kufanya hivyo, pale inapokuwa kifungu kimekosea, basi hakimu au jaji awe na mamlaka kisheria ya kuutaka upande husika
kufanya marekebisho na hivyo kuendelea na kesi. Huu ni wajibu wa wabunge. Kufuta kesi kwa njia hizi za ‘ujanja-ujanja’ kunawaumiza mno maskini wengi katika nchi yetu.
Itoshe tu kusema Makonda ametukumbusha namna mfumo wetu wa utoaji haki katika Taifa letu ulivyo na mushkeli.

Tunaweza kuilaumu Mahakama, lakini ukweli ni kuwa mnyororo wa chanzo cha shida hii ni mrefu. Upo kwa wanasheria, Polisi na mamlaka nyingine za usimamizi na utoaji wa
haki.

Tukilikiri hilo tutajua ni kwanini Rais Magufuli wakat mwingine anazungumza kwa hisia kali na kuonekana kama vile anaingilia mihimili mingine. Atakuwa kiongozi wa ajabu kuona watu wake wakitaabika kwa dhuluma, na yeye kama kiongozi mkuu wa dola akakaa kimya. Nchi inapojaa dhuluma lawama nyingi humwendea kiongozi mkuu maana wananchi wanamjua yeye kwa kuwa wamemchagua awaondolee kero.
 
Kesho Jumamosi asubuji atakiwa live tusikie majibu.

Kiongozi anayependwa kufatiliwa habari zake haswa na watu wa upinzani.. wakiongozwa na Mangenita.

Makonda oyeeeeeeeee
 
Hayanihusu....niko Gairo napiga mahela ya kumfurahisha my Nuru. Mimi ndo afisa miradi mzoefu bwana.
 
Back
Top Bottom