Mkuu , 'Salary', huu ndio ungepaswa kuwa mjadala wa nguvu, wa maana sana katika jukwaa hili la JF, pamoja na kwamba umeliweka kwenye siasa, kwa hiyo kama kutakuwepo na uchangiaji juu yake utakuwa ni ule ule wa aki"JohnBabtist' na watani wako wengine.
Nami nitaongeza machache katika mwonekano huo huo, hadi hapo itakapoonekana kwamba mjadala unakwenda kivingine.
Haya, nami nianzie hapa:
1. Kuhusu usalama wa chanjo hiyo - kwanza sisi haituhusu, kwa sababu tulishatangaza tayari kuwa Mungu wetu katuwekea kinga. Ni chanjo ipi itakayozidi hiyo ya muumba wetu aliyotuwekea baada ya kusikia maombi yetu? Tumeacha kabisa kupima na kuchukua tahadhari nyingine zozote zinazotakiwa kuchukuliwa ili maambukizi yasienee zaidi; kwa nini sasa tuhangaike na kinga. Jambo muhimu kwetu hapa sasa ni kuhimiza tu hilo, la Kinga kutokuwa salama, pengine uamini wetu huo unatokana na sala tulizompelekea Mungu wetu na yeye kutujibu tusithubutu kabisa kujihusisha na kinga hizo.
2. Ukweli wa tuhuma: njia pekee ya kujua ni kufanya utafiti juu ya kinga hiyo na kuona matokeo yake. Kama hujafanya hivyo, soma tafiti za waliofanya ugunduzi na uendelezi wa chanjo hizo na mamlaka za nchi mbalimbali kuhusiana na hizo chanjo. Wasomi wa kusoma na kuelewa maandiko ya namna hiyo sasa tunao Tanzania, pamoja na kwamba hatuwapi nafasi na fursa nzuri za kuendeleza utaalamu wao.
Katika hili, hapa ndipo tutakapoachwa kwenye mataa hasa na wenzetu, majirani zetu. Wao angalau wanashiriki na kushirikiana na taasisi nyingi toka nje na kupata uzoefu mkubwa, sio katika nyanja kama hizi pekee, lakini sasa ni kama tumejitoa kabisa katika nyanja zote, hasa hizi zinazoinukia kama technology, na maeneo mengine.
Tutajutia sana kupoteza muda huu tunaopooteza kwa kujiweka pembeni.
Kwa hiyo; juu ya tuhuma - sisi badala ya kujishughulisha na kutafuta ukweli, tutakazana kueleza "ukweli" wetu (feki) ili tuendelee kuonekana kuwa taifa lililobarikiwa na Mungu. Ni mtaalam yupi atafanya kinyume cha matamko ya mtawala?
3. Ma-dokta na ma-profesa? Wewe huoni wanavyopigana vikumbo kutafuta teuzi? Ni dokta/profesa gani asiyependa kuteuliwa, ili abaki kwenye maabara akicheza na mapanya?
Miaka hii zaidi ya 60, tumekuwa na taasisi nzuri tu za kutufundishia wataalam wa aina hii, na wengi wamepelekwa nje kusomea mambo haya haya, halafu useme hatuna wataalam. Tafuta wanakoishia hao wataalam, hapo ndipo utakapopata jibu sahihi.
Vyuo na taasisi mbalimbali vimefanya nini, sio kutafuta tu majibu juu ya corona, uliza maeneo yetu yote tulikoweka juhudi ya kufumbua matatizo ya wananchi, si kilimo, si Afya, si elimu, n.k., matatizo kote huko ni yale yale unayotafuta majibu yako juu ya hili janga la corona.
Kwani hatuna matatizo ya "kutu' kuharibu au kufifisha ufanisi wa mitambo yetu? Kuna mTanzania mwenzetu alifanya utafiti wake, ukampa hadi Ph.D. yake katika eneo la kuzuia kutu kwa kutumia mafuta ya maganda ya korosho. Ulishasikia habari nyingine yoyote kuhusu kunufaika kwetu kutokana na juhudi zake hizo?
Sitaendelea kujibu hayo maswali yake mengine yaliyobaki huko chini, kwa sababu majibu yake yanafanana na hayo niliyokuandikia hapo juu.
Kinachokosekana: ni utashi wa kisiasa.
Hawa wenye madaraka, wakiamua kwamba wanataka kusimamia na kuona mafanikio katika eneo lolote tunaloweza kulipa kipaumbele, tutapiga hatua mbele. Miaka mitano inatosha kabisa, kwa mfano, tukiamua kwamba tunataka kuwa na "Chemical industry" yetu hapa itakayozalisha kemikali mbalimbali zinazohitajika maeneo mengi tu duniani na hasa kwenye nchi zetu hizi za kiafrika. Hiki kitakuwa ndio kitovu cha viwanda vingine muhimu kama viwanda vya madawa, mbolea n.k. Mali ghafi za kufanya hivyo tunazo, ambazo hatuna tutaagiza.
Wataalam ambao taifa hili lilikwishawasomesha na wengi wao hata kufikia kustaafu bila ya kuitumia elimu yao hiyo, wengi wapo, ni swala tu la kuwa-'organize' na kuwapa nyenzo za kufanyia kazi. Miaka mitano utaona mabadiliko makubwa. Huu ni mfano tu mmoja.
Corona sisi tuliishinda, na vile vipimo tuliwaeleza dunia nzima kwamba sisi havitufai, baada ya kupima mapapai na mbuzi. Halafu kuna watu kama akina 'Salary' wanaleta maswali yasiyoeleweka na yeyote hapa!
Najua utachoka sana kusoma haya mkuu wangu, lakini uchokozi unaoufanya na kuumiza utulivu wa mawazo hapa sio kitu kizuri.
Nakutakia Heri ya Mwaka Mpya 2021.