Kongamano la Nyerere latamka 'utajiri wa viongozi unatishia amani' | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kongamano la Nyerere latamka 'utajiri wa viongozi unatishia amani'

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Josh Michael, Dec 4, 2009.

 1. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #1
  Dec 4, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Kongamano la Nyerere latamka 'utajiri wa viongozi unatishia amani'[​IMG]*MITANDAO YA KISIASA YATAJWA PIA KAMA KITISHO NA CHANZO CHA KUCHAFUANA

  Na Ramadhan Semtawa

  VIONGOZI wa dini na taasisi nyingine wameonyesha wasiwasi dhidi ya utajiri wa viongozi wakiweka bayana kuwa ukwasi wao unaweka hatarini amani na utulivu wa nchi.

  Tamko hilo la viongozi hao wa dini na wadau wengine wakiwemo wanaharakati, wanasiasa na wananchi wa kawaida limezidi kuiweka mahali pagumu serikali ya Rais Jakaya Kikwete ambaye anatuhumiwa kusita kufanya maamuzi magumu dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi, kiasi cha kutakiwa apumzike iwapo atashindwa kufanya hivyo kabla ya mwaka 2010.

  Tamko hilo lililoyolewa katika siku ya mwisho ya kongamano lilioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, limeeleza kuwa katika kipindi cha miaka kumi ya kifo cha mwalimu, taifa limekuwa njia panda.

  Sehemu ya tamko hilo inasema: "Kongamano lilikiri kwamba, taifa limepungukiwa kwa kiasi kikubwa na maadili hasa upande wa uongozi na viongozi baada ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, jambo ambalo linatishia amani, utulivu, maendeleo na ustawi wa muda mrefu wa taifa letu.

  "Mmomonyoko huo unadhihirishwa na ongezeko kubwa la rushwa na ufisadi na uvunjaji wa haki za binadamu. Jambo jingine ni pamoja na tabia na hulka ya viongozi kushindana kwa kujilimbikizia mali na kutoheshimiana."

  Tamko hilo ambalo limetiwa saini na mwenyekiti wa mfuko huo, Dk Salim Ahmed Salim limeonya kwamba "mitandao mbalimbali isiyo rasmi yenye sura ya vyama vya siasa ni chanzo kimoja kinachotishia amani hiyo ya nchi".

  Katika kuzidi kuonya, sehemu ya tamko hilo inaongeza kusema: "Mambo haya yanaondoa uzalendo, uadilifu, ufanisi, matumaini na imani ya wananchi kwa mfumo wa uongozi."

  Tamko hilo limetoa mambo makuu saba yanayopaswa kufanywa haraka ili kuinusuru nchi ambayo ni pamoja na kufanyika maamuzi magumu na hatua za kijasiri kwa lengo la kurejesha maadili aliyoacha Mwalimu.

  "Maadili hayo ni pamoja na kuheshimu na kuzingatia katiba, utawala wa sheria kwa mujibu wa katiba, na viapo vyao vya uongozi/utumishi; pili, kutambua cheo ni dhamana na kamwe kisitumike kwa faida binafsi; tatu na viongozi kusimamia matumizi bora ya rasilimali za taifa.
  Â
  "Nne,wananchi kutambua kwamba wana jukumu la kwanza kuhakikisha wanapata viongozi wazuri; tano, viongozi nao kutambua na kuheshimu maamuzi ya wananchi waliowapa madaraka; sita, viongozi wakishirikiana na wananchi wachukie rushwa na ufisadi na wavipinge kwa kauli na vitendo."
  Â
  "Na saba, viongozi wajenge utamaduni wa kuwajibika pale wananchi wanapowahusisha na kashfa na makosa ya kimaadili katika uongozi."
  Â
  Kwa undani tamko hilo liliongeza kwamba kongamano lilitambua juhudi za serikali za kuboresha sekta ya madini kwa kuunda Kamati ya Jaji Bomani iliyochunguza mikataba ya madini na kutoa mapendekezo.
  Â
  Hata hivyo, tamko hilo linaeleza: "Wajumbe walitoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka kutekeleza mapendekezo hayo ya kamati ya Jaji Bomani... pia limetahadharisha serikali si busara kuchimba madini yote kwa wakati huu bila kuzingatia mahitaji ya vizazi vijavyo."
  Â
  Akichangia mada ya utandawazi, mmoja wa mawaziri wa kwanza wa Tanganyika, Balozi Job Lusinde alionya serikali kuhusu uchimbaji wa madini ya ureniamu na kwamba, angekuwa ni yeye asingeruhusu yachimbwe sasa hivi.

  Sehemu ya tamko hilo inasisitiza kwamba serikali inapaswa kufuatilia kwa makini malalamiko yanayojitokeza katika utekelezaji wa sheria mpya ya rushwa inayoipa nguvu Takukuru.

  Kuhusu uwanja wa demokrasia na hali ya kisiasa ndani ya vyama vya siasa, tamko lilisema ipo haja ya kuwepo siasa za uvumilivu na kutambua kwamba upinzani siyo uhaini au uadui bali ni njia ya kukomaza demokrasia inayozaa serikali bora kwa faida ya taifa.

  Kuhusu dai la muda mrefu la madabiliko ya katiba, tmko hilo limeweka bayana kwamba hadi sasa wananchi hawana ufahamu wa katiba hivyo ni vema kwanza ikatolewa elimu ya uraia na ile inayohusu katiba.
  Â
  Kuhusu hali ya kisiasa visiwani Zanzibar, tamko hilo liliridhishwa na hali ilivyo sasa baada ya kufanyika mazungumzo kati ya Rais Amani Abeid Karume na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad. Kongamano hilo ambalo lilibua hisia na mitazamo mizito na tofauti, lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wasataafu, akiwemo waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, Balozi Lusinde, Balozi Daud Mwakawago na wanazuoni kama Profesa Issa Shivji na viongozi wa ngazi za juu wa dini za Kiislam na Kikristo. 
   
Loading...