KJ Leo: Msimamo Mkali Wa Vijana Wa UDSM | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

KJ Leo: Msimamo Mkali Wa Vijana Wa UDSM

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Sumaku, May 19, 2009.

 1. S

  Sumaku Member

  #1
  May 19, 2009
  Joined: Feb 17, 2009
  Messages: 53
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Ya Miaka Kumi ya Kuanzia 1960: Msimamo Mkali wa Vijana wa Mlimani (2)

  19 May 2009 3 views No Comment
  Na Born Again Pagan
  KATIKA makala yaliyopita, tulianza na hoja kwamba haiwezekani kabisa kuweza kusimulia maisha ya vijana wa Mlimani (1966 hadi 1970) na jinsi yalivyojenga mkitadha uliyozalisha msimamo mkali, bila kutoa, pengine, “background” ya matukio ya miaka kumi ya kuanzia 1960.
  Tuliona matukio kumi na tatu (matatu) yaliyochangia kidogo kidogo katika kujenga mkitadha wa msimamo mkali wa baadhi ya vijana waliokisoma hapo Mlimani mika hiyo. Hili ni kundi ninalolifahamu vizuri – wanafunzi wa mwaka wangu. Kwa kutamka hivyo, ningependa kumweka kando kidogo Samwel Sitta, ambaye alimaliza hapo Mlimani mwaka 1967.
  Wanafunzi wa mwaka wangu walikuwa ni wengi, karibu mara mbili. Ukubwa huo ulitokana na kufukuzwa na kurudishwa kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza (1966) na kujiunga upya na wanafunzi wengine wa mwaka kwanza (1967).
  Makala yaliwatambua baadhi tu ya hao vijana, kwa mfano, Souma (Guinea), Yoweri Kaguta Museveni (Uganda), Archibord Kapote Mwakasungura (Malawi), na John Garang (marehemu) wa Sudani. Vijana wa-Tanzania walikuwa, kwa mfano, Salim Msoma, Issa Shivji, Henry Mapolu, Andrew Shija, Ali Mchumo, Adamu Marwa, Pius Ngw’andu, Saida Yahya, Crispin Hauli, (marehemu), Abdallah Ngororo (marehemu), Patrick Qorro, Jenerali Ulimwengu, na wengine wengi sana, kama mimi.
  Hii haina maana ya kwamba vijana hao wenye msimamo mkali walikuwa ndio peke yao waliopata kuelemishwa hapo Mlimani. La, hasha! Wala haina maana ya kutamati kuwa matukio hayo yalitokea ili kuwafanya vijana hao wachache wawe na msimamo kama huo.
  Matukio hayo yalikuwa ni elimu mbadala (relevant information) ya wakati huo. Elimu hiyo ilikaribisha majadiliano (discussions) ya kina. Ilijikita katika tafukari makini (deliberations). Washiriki walifikia uamuzi (decision making). Walipanga mkakati wa amali (action) na mbinu za hatua (steps) za kuchukua kuyafanikisha waliyoyaona kuwa ni mazuri maishani.
  Kwa maneno mengine, vijana hao wachache walikuwa na dhamira au busara (prudence) ya kuona changamoto ya matukio hayo; walichukua fursa (opportune) kuyatafukari kwa undani na kuyatafsiri ili yawe na maana (internalise) maishani. Na waliamua cha kufanya: kusoma na kujitolea kusaidia wale ambao hawakuwa na nafasi nzuri kama wao, kulingana na msemo wa siku hizo, a luta continua (mapambano yanaendelea). Msimamo wao mkali ulilindwa na uongozi mzuri wa ki-siasa nchini na taaluma mahiri hapo Mlimani.
  Najua kati yenu kuna wenye swali, “Ikiwa nawapigia debe kiasi hicho, mbona waligoma kuunga mkono mswada wa Jeshi la Kujenga Taifa na hapo baadaye kufukuzwa kwa muhula wa mwaka mmoja wa masomo?” Fundisho walilopata lilisaidia sana kusukuma mbele akili ya kujitolea katika kusaidia masikini, kama nitakavyotamati katika makala ya mwisho: Mgomo wa Wanafunzi Jumamosi 22 Oktoba, 196l
  Makala haya yanaendelea kuelezea matukio mengineyo yasiyotiririka ki-miaka (chronology of events), sawa na yaliyopita, kama ifuatavyo:
  Kumi na nne, Tanzania Bara: Kushindwa kwa siasa na sera za ki-Bepari, chini ya Mpango wa Taifa ya Maendeleo wa Miaka Mitatu-Mitatu uliozingatia sana Tanganyika kukua ki-viwanda (ulioishia mwaka 1965). Mipango hii ilizalisha matabaka ya akina “ma-naiza” na “ma-kabwela” (mithili ya hali ilivyo sasa nchini kwetu). Ikumbukwe kwamba mfumo wa mipango hiyo ulitungwa na Mashirika ya Kimataifa ya Fedha (Benki Kuu ya Dunia na Mfuko wa Fedha) pamoja na wafadhili wengine, kwa mfano, Uingereza na Amerika.
  Kujengeka kwa matabaka hayo ya “ma-naiza” na “ma-kabwela” kulichangia sana kuchacha wimbi la Ujamaa wa ki-Afrika katika nchi zetu za kusini mwa Sahara. Wimbi hili lilitingisha sana, eti, maslahi ya wakubwa wengine kwa kuogopa kile Waziri Mkuu wa u-China Chou-en-Lai alichokiita “Afrika imeiva tayari kwa mapinduzi” (Africa is ripe for a revolution) – kufuatia ziara yake katika nchi kadhaa za ki-Afrika, zikiwemo Zambia na Tanzania.
  Kumi na tano, kupanuliwa kwa elimu ya sekondari ili kuharakisha kujitosheleza kuwapata wataalamu wetu: Kuongeza mitaala (streams) miwili kwa madarasa yote ya tisa; kuondoa kikwazo cha Mtihani wa Territorial Standard Ten ili kila mwanafunzi wa darasa la 9 aweze kumaliza darasa la 12; na kuondoa karo katika masomo ya sekondari na chuo kikuu.
  Ikumbukwe, kuwa miaka ya nyuma ya 1960 mtihani wa darasa la nane – Territorial Standard Eight – nao ulitolewa, ikiwa ni pamoja na kufupisha miaka ya elimu ya msingi kutoka 8 kuwa 7 na wanafunzi wa darsa la 7 kukubaliwa kujaribu mtihani wa Territorial Standard Eight.
  Zaidi, wanafunzi wa darasa la 11 kuruhusiwa kujaribu Mtihani wa darasa la 12 (Cambridge University Overseas School Certificate Examination – Ordinary Level) ili washindapo waingie darasa la 13; kuanza uratatibu wa pre-selection kwa wanafunzi wa darasa la 12 wenye uwezo kuweza kuingia na kuanza masomo ya darasa la 13 kabla ya matokeo ya (Cambridge University Overseas School Certificate Examination – Ordinary Level); na wanafunzi wa darasa la 14 kuweza kuingia chuo kikuu kwa kushinda somo moja (principal) na “subsidiary” moja.
  Zaidi, ili kujitosheleza kwa mahitaji ya walimu wenye digrii wanafunzi wote wa-Tanzania waliokuwa wakichukua masomo ya sayansi hapo Mlimani iliwabidi kuchukua pia somo la Elimu/Ualimu (Education Option). Ajabu ni kwamba watoto wa “vigogo” au waliokuwa karibu na “vigogo”, hawakuchukua Elimu/Ualimu (Education Option). Na hata wale wa mwaka wa kwanza 1966 waliporudishwa (baada ya mgomo, walidondosha kozi hiyo na kuchukua B.A. General – ili wasipelekwe ‘mikoani’ kufundisha!
  Hayo ya kudharau elimu yalianza zamani! Watoto wa “vigogo”, kwa kuelekezwa na wazazi wao, walitamani kubakia Dar es Salaam wakifanyakazi Wizara ya Nchi za Nje, Fedha na Mipango au Benki Kuu! Mwaka wetu kulikuwa na wanafunzi wawili tu, watoto wa ma-Waziri – walichukua Elimu/Ualimu (Education Option): Mvulana wa Muhaji (Waziri Mdogo – Elimu) na Blandina Mhando (Steven Mhando - Wizara ya Nchi za Nje).
  Tanzania ilikabiliwa na uhaba wa walimu katika mashule yake. Walimu wa-Uingereza walikuwa wananza kutoka mmoja mmoja. Nakumbuka mwalimu wangu wa Fizikia alikataa kutufundisha akidai, “I am going to teach in Kenya because you are now independent!” Ombwe la walimu lilizibwa na walimu wa-Amerika wa mpango wa Peace Corps – toka shule za msingi hadi sekondari. Wengine mliopita shule za msingi za wakati huo mnaweza kukumbuka uji wa ki-Amerika, “oatmeal”!
  Kumi na sita, kuzuka kwa vyama vingine vya siasa nchini, kwa mfano chama cha All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT), chini ya mnajimu mashuhuri Yahya Hussein. Lakini chama hiki kiliishiwa mafuta ya ki-siasa. Wengine walikiona kuwa ni chama cha ki-dini, eti kwa sababu wa-Islamu walikuwa wakisahauliwa. Lakini ukweli ni kwamba hata kabla ya uhuru Tanganyika chini ya TANU ilikuwa imeishatoa ubaguzi wa rangi na dini mashuleni!
  Kumi na saba, kutangaza kwa makusudi ya kuwafedhehesha wale serikali iliyowaona kuwa ni “majambazi ya uwongo”. Kulikuwepo na kundi la watu kama sita hivi walioshutumiwa kwa kueneza habari za uwongo nchini. Kwamba Makamu wa Pili wa Rais Rashid Mfaume Kawawa walipigana na Waziri wa Mambo ya Tawala za Mikoa Oscar Kambona wakati wa mkutano wa Kabineti.
  Kwa mara ya kwanza serikali ilitumia “propaganda ya kuaibisha” kupitia magazeti na Redio Tanzania Dar Es Salaam, kuyaanika majina ya “majambazi ya uwongo” wazi kila baada ya taarifa ya habari za jioni kwa muda wa juma moja! Sijui leo hii tunaweza, pia, kuwaadabisha mafisadi?
  Kumi na nane, kupinduliwa kwa Rais wa Ghana Kwame Nkrumah, ikiwa ni pamoja na nchi nyingi za Magharibi na Amerika kushirikiana katika kuunga mkono askari wa kukodiwa (mercenaries) walioranda-randa na kutamba-tamba katika nchi changa za Uwanda wa Joto wa Afrika na kutumika katika kupindua serikali zake, na kuweka viongozi vibaraka – wengi wakiwa ni wana-jeshi.
  Kumi na tisa, kuzaliwa kwa Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki: Makerere (Udaktari na Kilimo), Nairobi (Uhandisi na Biashara), na Dar es Salaam (Sheria na Elimu) na kuvunja uhusiano wa ki-taaluma na London University. Tukawa na digirii zetu za Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki badala ya za London University. Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki kiliwakutanisha vijana wengi.
  Ishirini, Tanzania ilikaribisha ma-Sosolisti waliokata tamaa (frustrated Socialists), ambao hawakuweza kupata ukumbi wa kufundisha au kutekeleza hayo ya Ujamaa huko kwao Ulaya, baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha. Azimio la Arusha liliwavuta, sio tu ma-Sosolisti waliokata tamaa bali pia wale wenye kutaka kutekeleza mfumo mpya wa maendeleo vijijini.
  Kiini cha Azimio la Arusha kilikuwa na mambo mawili makubwa:
  Azimio la Arusha ki-itikadi, lilikusudia kujenga akilini Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Ki-mkakati, liliashiria, kwa makusudi, kutekeleza mkakati uliojaa michakato ya kuleta mapinduzi ya uchumi na maslahi ya jamii vijijini (a total rural reform, transformation, transistion and change), ambayo yalikuwa hayajawahi kutekelezwa katika nchi changa, nje ya u-Uchina, Korea Kasikazini na Kuba!
  Ishirini na moja, Mlimani ikawa ndicho “kisima cha wanyama wenye kiu” ya itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea pamoja na nia ya kufanikisha mapinduzi ya uchumi na maslahi ya jamii vijijini (rural development strategy)!
  Serikali za nchi za kasikazini ya Ulaya Magharibi zilizokuwa na msimamo wa mkono wa kushoto, zilimwaga misaada mingi sana nchini Tanzania bila ya viongozi kutembeza mabakuli ya ombaomba! Mashirika yake pia yakafanya hivyo: DANIDA, SIDA na NORAD. Tanzania tukajikuta tunasaidiwa sana kinyume cha Siasa ya Kujitegemea!
  Baadaye, Nchi za Magharibi zilimshutumu Rais Nyerere kwa kuchomekeza wana-harakati wake wa ki-soshalisti katika nchi tulivu za Ukanda wa Joto wa Afrika (“unleashing his guerrilla socialist locusts in the otherwise tranquil savannah landscape”). Lakini Nyerere alipona kupinduliwa na ma-Bepari wenye kuchukia mwingilio wa Ujamaa!
  Ishirini na mbili, kufuatia kutangazwa kwa Azimio la Arusha, serikali ilitaifisha, kwa manufaa ya umma, nyenzo nyeti za uchumi. Azimio la Arusha lililoungwa mkono na vijana wengi kutembea kwa miguu, kwa mifano, kutoka Arusha hadi Dar es salaam na mmoja wa viongozi wake kufia njiani. Mwalimu Nyerere pia alitembea kwa miguu kutoka Butiama hadi Mwanza kuwatia nguvu vijana hao kwa kutembea. Vijana wengine walitembea kutoka Bukoba hadi Mwanza kama sio Dar es Salaam na wengine kutoa sehemu za huko kusini (Mbeya na Iringa).
  Ishirini na tatu, sambamba na utaifishaji huo, serikali ilibadilisha mkakati wa maendeleo vijijini kwa kuachana na sera za awali za “kunyesha misaada kutoka juu” kupitia “Makazi Mapya” (Rural Village Settlements): Upper Kitete (Arusha), Ikwiriri (Pwani), Luganga (Iringa), na makazi mengine huko Handeni (Tanga). Lakini mkakati huu, licha ya misaada kemukemu, ulishindikana. Wananchi hawakuwa tayari kuhamia vijijini! Tanzania ikaanza pole pole kuagiza watu wajiunge na Vijiji vya Ujamaa kwa kuanzia huko Mkoa wa Dodoma.
  Ishirini na nne, mgogoro wa Mashariki ya Kati ulijikita katika ukombozi wa wa-Palestina kutoka kuwafikiria kuwa ni wakimbizi tu kwenda katika suala la ukombozi wao. Msimamo huo uliingilia uhusiano wetu na serikali ya Israel, hususan, kufuatia vita ya mwaka 1967 ambapo Israel iliteka sehemu ya Afrika ya Sinai (Misri). Tanzania ilivunja uhusiano na Israel.
  Hadi kufikia wakati huo, Israel ilikuwa imewekeza katika kuanzisha Jeshi la Kujenga Taifa, misaada mingine ya ki-Jeshi la Ulinzi na usalama, utalii (ikiwa ni pamoja na kutujengea Hoteli za ki-talii, kwa mfano, Kilimanjaro kupitia Kampuni ya Uendelezaji wa ma-Hoteli ya Molonot), biashara ya Karadha, na miradi mingine ya kilimo cha kiangazi (kumwagilia mashamba).
  Uhusuiano huo ulihusu serikali. Lakini kuna watu walionufaika binafsi, pia. Kwa mfano, Mama Maria Nyerere alipata nafasi ya kwenda huko kusomea Mambo ya Nyumbani (Domestic Science) pamoja na utaalamu wa kufuga kuku hapo Kigamboni.
  Ishirini na tano, Tanzania ikawa ni kisima cha ma-Profesa wenye mlengo wa kushoto (ma-Soshalisti), kwa mfano, kufuatia mapinduzi ya Ghana, wakaja ma-Prof. David Kimble (Political Science) na mkewe (Uchumi); kutoka Denmark akaja Prof. Knud Svendsen kuwa Profesa wa Uchumi (mshauri wa mambo ya uchumi kwa serikali na chama), Prof. Chodak (Sosiolojia), Prof. Osborn (Fisikia), na Prof. Wellbourne (Elimu).
  Wengine walikuwa Prof. Goran Heyden (aliyeondoka na mke wa ki-Haya), na baadhi ya ma-Soshalisti ambao hawakuweza kuhubiri na kutekeleza imani yao makwao (Ulaya/Amerika), kwa mfano. Prof. R. H. Green. Mshauri wa mambo ya Fedha kutoka Chuo Kikuu cha Sussex, Uingereza, na Prof. White (Sheria) aliyeondoka na mke wa ki-Chagga!
  Kulikuwepo na ma-Profesa wengine kutoka Visiwa vya Karibe (Caribbeans), kama akina Walter Rodney (Historia) na Earl Carl James (Public Management/Sheria). Hata Jaji Mkuu Biron alikitokea huko huko Karibe. Wengine walitoka Kenya: Grant Kamenju (Fasihi), Kiara (Sheria) na Lionel Cliffe (Sayansi ya Siasa).
  Tukutane wiki ijayo kumalizia matukio hayo.
  Barua pepe: romuinja@yahoo.com

  Chanzo: http://www.kwanzajamii.com
   
 2. Waberoya

  Waberoya Platinum Member

  #2
  May 19, 2009
  Joined: Aug 3, 2008
  Messages: 11,598
  Likes Received: 3,888
  Trophy Points: 280
  sumaku wako wapi hao siku hizi? wamekufa? kama wako hai wanafanya nini??

  isije ikiwawameshavutwa na 'dunia' ukabaki kueleza historia walikuwa, walikuwa, walikuwa......
   
 3. Shaycas

  Shaycas JF-Expert Member

  #3
  May 19, 2009
  Joined: Feb 13, 2009
  Messages: 899
  Likes Received: 34
  Trophy Points: 45
  Lengo la makala hii ni nini?
   
 4. Mnyisunura

  Mnyisunura Member

  #4
  May 20, 2009
  Joined: Aug 3, 2008
  Messages: 69
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 15
  Mkuu makala yako inavutia kama vitabu vya sheria na mipango ya wabunge wetu! Hao watu uliowtaja wengi bado wazima! Hatuoni strength yao sijui ndo wamevutwa na dunia!
  Unajua tunataka kuona performance! Halafu wengi uliowaorodhesha inaonekana bado wapo chuo wanaendelea kuboronga kama siyo wao basi wamekaa kimya huku madudu yanaendelea kufanyika pale chuo! Nadhani ungekaa kumya tu iwe siri yako kuwa mliwahi kuwa jemedari! Mwenzenu Mandela aliendelea mpaka mwisho licha ya kudhoofishwa!
  Kwa taarifa yako historia itawahukumu wote uliowaorodhesha hapo ambao bado wazima halafu wanaona madudu yanaendelea ndani ya nchi tukufu tuliyopewa na mungu halafu wako kimya!
  Ninawachukia wote mnaojiita kuwa mlikuwa vinara na wapigania haki halafu mnaona haki zinapotezwa mko kimya! Otherwise naweza sema nanyi mlikuwa na njaa tu zinawasumbua ndo maana kelele zilikuwa nyingi!
  Hao akina shivji, quoro, saida na wengine bado wapo chuo lakini wamezama ndani ya dimbwi lilelile walilokuwa hawalitaki!
  Aisee unazidi kuniudhi na makala hii!
   
Loading...