Kitila Mkumbo: Mafanikio na utata wa Membe kidiplomasia

Jabirimakame

Member
Jan 15, 2014
71
37
"MAFANIKIO NA UTATA WA MEMBE KIDIPLOMASIA

Kitila Mkumbo
KATIKA makala iliyopita nilianza kumjadili Benard Membe anayetajwa kuwa kati ya wagombea urais wenye nafasi kubwa ya kupitishwa kupeperusha bendera ya chama chake cha CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Katika makala haya ninajadili wasifu wa Membe katika maeneo ya kazi, uadilifu na diplomasia.

Kikazi, tunaweza kusema Membe ni mtu aliyekulia katika ushoroba wa madaraka (power corridors). Mara baada ya kumaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa, Membe aliajiriwa kufanya kazi katika ofisi ‘nyeti’ ya Rais. Na hata baada ya kuhitimu masomo yake ya shahada ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alirudi kuendelea na kazi yake ya ukachero na hivyo kushindwa kuchukua kazi aliyokuwa amepewa ya uhadhiri msaidizi katika Chuo hicho.

Membe alipanda ngazi kadhaa na hata kuwa msaidizi wa waliopata kuwa wakurugenzi wakuu wa Idara nyeti ya Usalama wa Taifa, Dk. Hans Kitine na Apson Mwang’onda.

Baada ya kumaliza masomo ya Shahada ya Uzamiri katika Chuo Kikuu cha John Hopkins nchini Marekani, Membe hakurudi tena kufanya kazi Ikulu bali alipelekwa ubalozi wa Tanzania nchini Canada kama Mwambata wa Ubalozi (Minister Plenipotentiary), akichukua nafasi ya Dk. Augustine Mahiga akiyekuwa amehamishiwa Umoja wa Mataifa.

Alidumu katika nafasi hiyo hadi mwaka 2000 alipoamua kugombea ubunge, akashinda na kuwa Mbunge wa pili wa Jimbo jipya la Mtama, akimrithi Masoud Ally Chitende.

Katika kampeni za urais za mwaka 2005 ndani na nje ya CCM Membe alifanya kazi kwa karibu na akina Edward Lowassa na Apson katika kuhakikisha kwamba Jakaya Kikwete anapitishwa kuwa mgombea na hatimaye kushinda katika uchaguzi wa urais.

Inafurahisha na hata kushangaza kwamba hawa leo ni mahasimu wakubwa kisiasa wote wakiwania nafasi ya kumrithi Rais Kikwete.

Tutarajie ushindani mkali hasa ndani ya CCM kati yao, ambao wanaonekana kuwa na nguvu, fursa, vikwazo na udhaifu katika maeneo tofautitofauti.
Baada ya Rais Kikwete kushinda uchaguzi wa mwaka 2005 alimteua Membe kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini nafasi aliyoshikilia kati ya Oktoba 2006 na Januari 2007, na baadaye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani kati ya Januari 2006 na Oktoba 2006. Baada ya kuteuliwa kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rais Kikwete alimteua Membe kuchukua nafasi yake.

Katika mawaziri 14 wa Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Kimataifa, Membe ndiye waziri wa pili kwa kushikilia nafasi hiyo kwa muda mrefu zaidi, akizidiwa tu na Rais Kikwete aliyedumu katika nafasi hiyo katika kipindi chote cha urais wa Mkapa.

Taswira ya Membe katika uadilifu

Bernard Membe ni kati ya viongozi wachache katika serikali ya CCM wanaojitutumua kwamba ni waadilifu.

Msingi wa uadifu wa Membe unajengwa katika maeneo mawili makubwa. Eneo la kwanza ni kazi aliyoifanya kuokoa fedha za umma kwa kutumia nafasi aliyoishika katika ubalozi wa Canada.

Mapema katika Bunge la mwaka 2001/2002, paliibuka kashfa kubwa ikimhusisha aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora Dk. Hans Kitine. Katika kashfa hiyo ilidaiwa kwamba Dk. Kitine alikuwa ametumia fedha za serikali kwa kumtibu mke wake, Saada Mkwawa Kitine, nje ya nchi kwa kiwango cha dola za kimarekani 63,000.

Hata hivyo, uchunguzi wa Serikali haukuonyesha ushahidi wowote kwamba mke wa Dk. Kitine alitibiwa nje ya nchi wala kuumwa. Kashfa hii ikasababisha Dk. Kitine kujiuzulu nafasi yake na mke wake kuamriwa kulipa fedha zote alizokuwa amechukua kwa matibabu hewa.

Hata hivyo, mwezi Julai 2002, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya Mbunge Richard Ndasa aliyekuwa anakaimu nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, iliandika barua Wizara ya Afya ikiiagiza wizara hiyo kumrudishia mke wa Kitine pesa ambazo alikuwa ameshalipa kiasi cha dola 15,000. Kamati hiyo ilidai kugundua kwamba Mama Kitine alikuwa kweli anaumwa na alitibiwa nje ya nchi kwa kufuata utaratibu.

Haraka haraka Dk. Kitine akaitisha mkutano na waandishi wa habari na kujigamba kwamba yeye ni mwadilifu na kilichotokea ilikuwa ni majungu tu na hivyo Bunge limemsafisha.

Ni katika hatua hii ambapo Bernard Membe alisimama Bungeni kueleza kwamba alikuwa na ushahidi bayana kuhusu ufisadi uliofanywa na Dk. Kitine kwa jina la matibabu ya mke wake.
Alipopewa nafasi, Membe akamwaga nyaraka muhimu zilikuwa zinaonyesha jinsi fedha zilivyotumwa kwenye akaunti binafsi ya mama Kitine badala ya kutumwa
katika akaunti ya ubalozi. Membe akiwa ubalozini Canada ndiye aliyepewa jukumu la kuchunguza uhalali wa matibu na malipo kwa ajili ya mama Kitine.

Katika hospitali zote zilizodaiwa kumtibu mama Kitine hawakupata ushahidi wowote kwamba aliwahi hata kufika huko, achilia mbali kutibiwa.

Kufuatia kuthibitika kwa kashfa ya Dk. Kitine, ilionekana wazi kwamba Kamati ya Bunge ilikuwa imetumika kujaribu kumsafisha Dk. Kitine na familia yake kwa njia za giza. Kwa sababu hii wajumbe watatu wa Kamati hii walifungiwa miezi miwili kihudhuria vikao vya Bunge. Wajumbe hawa walikuwa ni Richard Ndasa, Dk. Amani Kaborou na Dk. Hans Kitine mwenyewe.

Eneo la pili ni maelezo kwamba Membe ni mjumbe pekee wa Halmashauri Kuu aliyeshinda uchaguzi ndani ya chama chake mwaka 2012 kupitia kundi linaloitwa la kifo bila kuhonga wajumbe wa Mkutano Mkuu.

Katika uchaguzi huu Membe alichaguliwa kwa kura 1451, nyuma ya Wasira, Mwigulu Nchemba na Makamba, huku akipigwa vita kali na mahasimu wake waliopo katika kundi la Lowassa.

Mahasimu wake Membe wanakataa kwamba hakutumia pesa katika kushinda nafasi ya NEC. Hata hivyo, wanakiri kwamba walifanya kampeni dhidi yake ili ashindwe!

Mafanikio na Utata wa Membe kidiplomasia

Mafanikio na utata wa Membe kidiplomasia unaonekana katika maeneo mengi. Kwanza ni katika misimamo mbalimbali ambayo amekuwa akiitoa kwa niaba ya Tanzania.

Kwa mfano, amekuwa na msimamo wa wazi wa kumtetea Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe wakati ambapo mataifa ya Magharibi yakiwa yamemtenga na kutomtambua.

Hii inaweza kumtambulisha kama mzalendo wa Afrika (Pan Africanist). Aidha, Membe alisita kwa kipindi kirefu kuutambua utawala mpya wa Libya baada ya kupinduliwa kwa Rais Gadafi. Hata hivyo, baadhi ya watu walidhani kwamba Tanzania ingekuwa nchi ya kwanza kuutenga utawala wa Gadafi ukizingatia kwamba huyu ni mtu aliyetusaliti katika vita yetu na Idd Amin kwa kusaidia majeshi ya Uganda.

Pengine alama kubwa zaidi za mafanikio ambazo Membe anaweza kutembea nazo katika anga za kidiplomasia ni mbili. Mosi, ni kuchaguliwa kwake hivi karibuni kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Nchi za Jumuiya ya Madola (CMAG) mwezi Novemba 2013 huko Sri Lanka. Hii ni Kamati yenye nguvu sana katika Jumuiya ya Madola yenye majukumu mengi, ikiwamo kufukuza nchi uanachama wa Jumuiya hiyo. Kabla ya Membe, mara nyingi wenyeviti wa Kamati hii walitoka katika nchi zilizoendelea.

Alama ya pili ni jinsi alivyofanikisha ujio wa Marais wawili wakubwa duniani: Xi Jinping wa China na Barack Obama wa Marekani. Aidha, aina ya mapokezi waliyoandaliwa viongozi hawa yanaelezwa kuwa ya kiwango cha juu kiasi cha kusababisha kiwewe kwa nchi majirani.

Hata hivyo, kuna maeneo kadhaa yanayoonyesha utata kuhusu weledi wa Membe katika diplomasia. Kwa mfano, Membe aliitangazia dunia kupitia Bunge letu Mei 27, 2014 kwamba waasi wa kikundi cha M23 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuwa walikuwa ni raia wa Rwanda na walikuwa wakifadhiliwa na Serikali ya Rwanda.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Serikali ya Tanzania kuituhumu waziwazi Serikali ya Rwanda katika kufadhili kikundi hicho cha waasi katika kipindi ambacho uhusiano wa nchi mbili hizi ulikuwa unalegalega.

Kabla moto haujapoa, Mkumbwa Ally akikaimu nafasi ya Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, aliwaambia waandishi wa habari Julai 12 2013 kwamba “….Rwanda iachane na ndoto zake za kuivamia Tanzania; vinginevyo ...Kagame tutamtandika kama mtoto mdogo”.

Katika hali ya kawaida, na kwa kuzingatia nafasi ya Tanzania katika Afrika, haikutarajiwa kwamba Membe na Wizara yake wangemkabili Rais Paul Kagame kwa diplomasia ya kibabe.

Eneo jingine ambalo ni tata kuhusu diplomasia ya Membe ni sera ya diplomasia ya uchumi inayotekelezwa na Serikali ya Tanzania katika miaka ya hivi karibuni.

Kupitia demokrasia hii, balozi zetu zimekuwa na kazi kubwa ya kuvutia wawekazaji na kwa kweli zimefanikiwa sana kufanya kazi hii.

Hata hivyo, ni kipindi hiki pia ambacho nchi yetu imepokea wawekezaji wa ajabu ambao wamegeuka kuwa waporaji wa raslimali zetu na wengine kuingiza nchi yetu katika giza nene la ufisadi.

Ni katika kipindi hiki pia ambacho nchi yetu imegeuka kuwa ombaomba, na hatimaye, kupoteza kabisa msamiati wa ‘Kujitegemea’ katika falsafa za maendeleo Tanzania.

Aidha, kwa kiasi kikubwa, Tanzania imepoteza nafasi iliyokuwa nayo katika Bara la Afrika. Kwa mfano, wakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kwanza Tanzania ndiyo ilikuwa kiongozi lakini sasa tumekuwa ndio kikwazo cha Jumuiya hii na tumekuwa tukibembelezwa na kuburuzwa.

Tumewekeza zaidi kukubalika katika mataifa ya Wazungu na kusahau kabisa Afrika. Haishangazi basi kuona kwamba leo hii Rais wetu amefanya ziara nyingi zaidi Marekani na Ulaya kuliko alizofanya Afrika.

Inashangaza, kwa mfano, hadi niandikapo makala hii Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya hajawahi kufanya ziara ya kikazi rasmi Dar es Salaam zaidi ya mwaka mmoja tangu achaguliwe.

Eneo la tatu ni msimamo wa Membe kuhusu uraia pacha. Waziri Membe na Rais Kikwete wamekuwa na msimamo wa waziwazi wa kuunga mkono uraia pacha kinyume cha msimamo wa Julius Nyerere wa mwaka 1962 aliyepinga uraia huo.

Kwa baadhi ya watu uraia pacha ni jambo la maana na wanamuona Membe kama mtu anayekwenda na wakati na msimamo huu unakwenda sambasamba na diplomasia ya uchumi. Kwa watu wengine, hata hivyo, kuunga mkono uraia pacha ni kukosa uzalendo.

Hitimisho

Bila shaka kuna mambo mengi yanayombeba Membe kama mgombea urais kihaiba na kikazi. Kwanza ana msimamo. Bila kujali uhasi na uchanya wa misimamo yake, kuwa na msimamo ni jambo la msingi kwa kiongozi.

Msimamo wake mkali dhidi ya mambo kadhaa kimataifa na kukulia kwake katika kazi ya ukachero yamewafanya baadhi ya watu kufananisha haiba ya Membe na ile ya Rais Vladimir Putin wa Russia aliyekulia Kremlin.

Hata hivyo, ili avae haiba ya Putin sawasawa, itamlazimu kuuvaa ukali kidogo kwa kuwa baadhi ya watu waliopo naye karibu wanamueleza kuwa ni mtu mpole na mwepesi wa huruma. Hii inaweza ikawa kasoro kwa baadhi ya watu wanaoamini kwamba Tanzania ilipofika haihitaji Rais mpole wala mwenye huruma.

Pili, Membe anajitambulisha kwa taswira ya uadilifu na kwa kweli ni vigumu kumhusisha na kashfa yeyote iliyotokea hapa nchini.

Kwa mfano, Membe hatajwi popote katika Ripoti ya Dk. Harrison Mwakyembe iliyochunguza kashfa ya Richmond licha ya ukweli kwamba yeye alikuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini. Hata hivyo, Membe ana kazi ya ziada katika kujenga imani kwamba ana taswira tofauti na chama chake katika eneo la uadilifu.

Tatu, Membe anajivunia rekodi ya kuipaisha Tanzania katika anga za kimataifa,kidiplomasia. Hata hivyo, ana maswali ya kujibu kutokana na taswira ya Tanzania kufifia katika diplomasia ya Afrika na hasa kusuasua kwa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ni wazi kuwa Membe ana alama kadhaa chanya za kiuongozi zinazojionyesha katika utendaji wake sehemu mbalimbali alizofanya kazi. Hata hivyo, anayo kazi katika kuzinadi alama hizi katika jamii ili zimjengee taswira ya uchapa kazi, ambayo ni moja ya sifa muhimu za rais wa awamu ya tano.

Ninamtakia kila la heri Bernard Kamillius Membe katika mbio zake za kuwania uongozi wa juu katika nchi yetu"

(Prof. Kitila Mkumbo, Raia Mwema, Toleo la 375, Octoba 15, 2014)
Raia Mwema - Mafanikio na utata wa Membe kidiplomasia ImageUploadedByJamiiForums1413739402.355029.jpg ImageUploadedByJamiiForums1413739419.488757.jpg
 
Chini ya Uongozi Makini wa Bernad Membe hapo Wizara ya mambo ya nje, Tanzania ilikuwa Nyota ya Kidiplomasia hapa Afrika, aliwezesha Kuleta Maraisi wa nchi kubwa nchini kama vile George Bush, Obama na Xijinping, na Makubaliano yenye thamani ya Matrilion ya shilingi yalisainiwa. Hapa chini ni baadhi ya Ziara za maraisi wa Marekani na China nchini. kwa sasa najiuliza mbona nchini wanakuja akina Kagame
El-Sisi, Mfalme wa Morocco, Museveni etc mbona Trump au Putin haji kulikoni?

?
obama 1.jpg


xijinping 2.jpg


obama 1.jpg

Obama 3.jpg


bush 5.jpg



George bush.jpg
 
Labda kama lengo ni kumnanga jiwe, ila kwangu mwanasiasa yoyote aliyechezea mchakato wa katiba mpya ni mshenzi kama washenzi wengine. Huyo Membe alipokuwa kwenye madaraka alikuwa na nyodo, saa hii analambishwa mchanga na mkuu wa mashetani ndio anajifanya malaika.
 
Labda kama lengo ni kumnanga jiwe, ila kwangu mwanasiasa yoyote aliyechezea mchakato wa katiba mpya ni mshenzi kama washenzi wengine. Huyo Membe alipokuwa kwenye madaraka alikuwa na nyodo, saa hii analambishwa mchanga na mkuu wa mashetani ndio anajifanya malaika.

Nyodo ni subjective siyo hoja ya kisiasa, hoja ya kisiasa ni kuheshimu katiba, sheria na miongozo ya kazi, kama alikuwa hatabasamu kwa baadhi ya watu ila anatabasamu kwa wengine hilo ni personal, siyo suala la kitaifa!. Hatutafuti "Chakaramu" kwenye mamlaka ya raisi sisi
 
Ziara za kisiasa, wala hazikuwa na musukumo wowote katika Maendeleo ya taifa letu, zaidi yalikuwa manufaa ya watawala tu...!!

Unajua mchango wa Ziara ya George Bush kwenye kampeni ya Kuzuia Vifo vya akina mama wanaojifungua na vichanga vyao?, kupiga vita malaria? na ARV kwa waathirika wa HIV?
Ziara ilikuwa muhimu sana ile kwa afya za wananchi
 
Chini ya Uongozi Makini wa Bernad Membe hapo Wizara ya mambo ya nje, Tanzania ilikuwa Nyota ya Kidiplomasia hapa Afrika, aliwezesha Kuleta Maraisi wa nchi kubwa nchini kama vile George Bush, Obama na Xijinping, na Makubaliano yenye thamani ya Matrilion ya shilingi yalisainiwa. Hapa chini ni baadhi ya Ziara za maraisi wa Marekani na China nchini. kwa sasa najiuliza mbona nchini wanakuja akina Kagame
El-Sisi, mbona Trump au Putin haji kulikoni?

?View attachment 1174033

View attachment 1174022

View attachment 1174033
View attachment 1174024

View attachment 1174028


View attachment 1174030
Let's be true... Tulihitaji mtu aina ya Mzee baba...lakini kuna vitu vidogo sana akivirekebisha atakumbukwa vizazi na vizazi
 
Let's be true... Tulihitaji mtu aina ya Mzee baba...lakini kuna vitu vidogo sana akivirekebisha atakumbukwa vizazi na vizazi

Vitu vidogo vitu gani Mshana Jr?, huenda sisi hivyo unavyoviona vidogo sisi tunaona ni vikubwa sana, kimojawapo kwa mfano kutoheshimu katiba na kiapo cha Rais
"NITALINDA NA KUITETEA KATIBA, NITATIMIZA MAJUKUMU YANGU BILA UPENDELEO WALA HUBA, WALA KUMUONEA YEYOTE......". Hicho siyo kitu kidogo, Hicho ni kikubwa kabisa, ukikivunja hicho basi ni Msaliti!
 
Nyodo ni subjective siyo hoja ya kisiasa, hoja ya kisiasa ni kuheshimu katiba, sheria na miongozo ya kazi, kama alikuwa hatabasamu kwa baadhi ya watu ila anatabasamu kwa wengine hilo ni personal, siyo suala la kitaifa!. Hatutafuti "Chakaramu" kwenye mamlaka ya raisi

Uko sahihi sana, lakini kama Membe angekuwa anaheshimu maoni ya wananchi asingechezea mchakato wa katiba mpya mpaka leo tumejikuta hapa tulipo. Hivyo yeye ni muhuni kama wahuni wengine.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom