SoC03 Kitanzi chakula lishe shuleni

Stories of Change - 2023 Competition

AUGUSTINO CHIWINGA

JF-Expert Member
Apr 23, 2017
220
689
Inaeleweka kwamba mwanafunzi anayepata chakula lishe shuleni humsaidia kuacha utoro, kuwa na afya njema ya akili na mwili, mimba za utotoni na ukatili mwingineo wa kijinsia, na usikivu mzuri darasani.

Takwimu zilizopo juu ya madhara ya kukosekana kwa chakula lishe zinatisha na zinatoa ishara mbaya juu ya mustakabali wa elimu Tanzania. Ubora wa elimu unapungua wanafunzi wapo kitanzini.

Mtoto kula chakula nyumbani kutamgharimu mambo mengi ikiwamo muda na kuchoka. Aghalabu kwa mazingira ya vijijini mtoto atatakiwa kupika chakula mwenyewe, kwa kuanzia kwenda kuchota maji kisimani kukusanya kuni/kuwasha jiko na kupika. Akimaliza hapo lazima awe amechoka hali itakayomuathiri darasani pindi akirejea.

Licha ya Serikali na wadau wengine mbalimbali kujitahidi kulisemea jambo hili lakini bado idadi ya wanafunzi wanaopata CHAKULA LISHE ipo chini sana. Hali hiyo inasababishwa na udhaifu wa mifumo ya utawala bora na uwajibikaji kwa Serikali, shule na jamii/wazazi.

Ninapozungumzia CHAKULA LISHE, napenda kitofautishwe na chakula cha kawaida walichozoea wanafunzi kupewa kama vile ugali/wali /maharage.

CHAKULA LISHE ni kile chakula ambacho kina virutubisho ya makundi muhimu matano ya chakula.

Kutokana na udhaifu wa utawala bora na uwajibikaji jambo hili limekuwa gumu kwenye kutekelezeka katika mitaa na vijiji vyetu.

Jamii/wazazi/walezi wamekosa kuwajibika katika kuhisi na kuona kwamba jukumu la kuhakikisha kwamba mtoto anapata chakula bora (Chakula Lishe) ni jukumu lao. Wengi wao wanadhania ni kazi ya Serikali kufanya hivyo.

Lakini pia Serikali, na viongozi wa ngazi zote hususani katika Serikali za Mitaa nao wamekosa utaratibu wa utawala bora ili usaidie katika kutatua changamoto za wanafunzi kupata chakula lishe shuleni.

Ukosefu wa uwazi kwenye michango ambayo wazazi wanachanga shuleni iwe ya fedha, au chakula ni eneo mojawapo ambalo linaathiri jambo hili kufanikiwa.

Unakuta wazazi wanachanga michango kwa ajili ya watoto kula shuleni lakini hawasomewi mapato na matumizi kwenye vikao vyao vya wazazi, kamati za shule na viongozi wa serikali za mitaa, hali inayopelekea wazazi kuvunjika moyo wa kuendelea kuchanga.

Kukosekana kwa uwazi kunapelekea wazazi na wanajamii kuhisi labda michango yao inatumiwa vibaya na viongozi wa Serikali za mtaa na walimu.

Eneo jingine ni kwenye usimamizi wa fedha na uhifadhi (storage) wa vyakula. Kama ilivyo kawaida fedha zinahitaji usimamizi mzuri ili ziendane na bajeti iliyopangwa.

Lakini kutokana na usimamizi mbovu fedha za michango huwa zinatumiwa hovyo hovyo hali inayopelekea kutokufikia lengo la kutoa chakula lishe kwa wanafunzi shuleni. Vile vitu vinavyotakiwa kununuliwa havinunuliwa hivyo wazazi/ jamii huona thamani ya michango ya fedha zao imepotea.

Lakini pia walimu, wazazi na kamati ya shule huwa hawazingatii kutayarisha eneo zuri safi na salama kwa ajili ya kuhifadhia chakula. Chakula kinahifadhiwa hovyo hali inayopelekea kuharibika hivyo kuathiri utolewaji wa chakula lishe shuleni.

Chakula kilichochangwa na wazazi kikiharibika inakua ni ngumu tena kumshawishi mzazi huyohuyo kuchangia tena, uwajibikaji katika kutayarisha eneo la kuhifadhia au kutunzia chakula ni muhimu sana.

Mara nyingi ushirikishwaji wa mipango endelevu ya utoaji wa chakula lishe unakosekana. Walimu na wazazi na Serikali za vijiji/mtaa /kata hua wanakosa kushirikishana kwenye mpango huu.

Kundi moja hususani wazazi huhisi wametengwa hali inayopelekea kutokufikia lengo. Endapo ushirikshwaji utakuwepo ni wazi kila kundi litajiona linahusika moja kwa moja na watawajibika katika kuhakikisha utolewaji wa chakula lishe unafanikiwa.

Uwajibikaji wazazi wanahisi au kudhani kwamba huduma ya utolewaji chakula ni jukumu la Serikali pekee. Hivyo wanashawishiana kutotoa michango ambayo ingeweza kuwapa watoto wao wenyewe lishe nzuri.

Nini kifanyike ili kukitoa kitanzi hicho?

1. Wazazi na jamii washirikishwe kila hatua juu ya mpango huu ili wawe sehemu au wamiliki wa mpango wa utolewaji chakula lishe. Lazima wazazi waeleweshwe kwa kina juu ya faida ya kuwapatia watoto chakula lishe shuleni na wao wakiwa wadau muhimu kabisa.

2. Uwazi uwepo katika usomaji wa taarifa muhimu kama vile mapato na matumizi.

3. Zitungwe sheria ndogo ndogo na Serikali za mtaa.
Hakuna jambo linalofanikiwa bila ya kuwepo kwa utaratibu wa utawala wa sheria.
Utawala wa sheria utawaongoza wazazi/wanajamii kutekeleza makubaliano ya utolewaji wa chakula lishe.

4. Kwa maeneo ya vijijni wazazi wanaweza kupewa hamasa ya kuanzisha na kulima shamba lishe la shule kwa ajili ya chakula cha watoto wao mwaka mzima, na kwa maeneo mjini hamasa kubwa ielekezwe kwenye utolewaji wa michango.

5. Lazima ufanisi uzingatiwe. Malengo ya pamoja yanawekwa yahakikishwe yanafikiwa ili kutatua changamoto kadha wa kadha zinazowakumba wanafunzi kutokana na ukosefu wa chakula lishe.

6. Kwenye shule ambazo zinazungukwa na rasrimali kama vile migodi basi utaratibu uwekwe ili wawekezaji hao wawe wanazihudumia shule hizo kwa chakula lishe.

7. Wazazi na wanajamii waelimishwe kwamba wao wanawajibika katika sehemu kubwa ya kuhakikisha upatikanaji wa chakula lishe shuleni unakua ni wa siku zote za mwaka na sio kipindi fulani hususani katika msimu wa mavuno ili kutoa hakikisho kwa mwanafunzi kupata huduma hii mihula yote ya masomo.

8. Kuundwa kwa kamati za pamoja usimamizi na ugawaji wa chakula baina ya viongozi wa mtaa, walimu na wazazi ili kuondoa sintofahamu ya dhana kwamba pesa na michango ya wazazi inaliwa au kutumika vibaya.
 
Back
Top Bottom