* Shughuli zote kuendeshwa kwa Kiswahili
Serikali imeagiza matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika shughuli zake rasmi na pia majina ya mitaa na mabango kuandikwa kwa lugha hiyo ili kukienzi Kiswahili kama lugha ya taifa.
Pia, zimetakiwa jitihada za makusudi zifanyike ili shughuli za mahakama katika ngazi zote ziendeshwe kwa lugha ya Kiswahili.
Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika, alipokuwa akisoma kauli ya serikali kuhusu matumizi ya Kiswahili katika shughuli rasmi za serikali, bungeni mjini hapa jana.
Katika agizo hilo, Mkuchika alisema dhifa mbalimbali za kitaifa, hotuba, warsha, semina na mikutano ya kitaifa, ziendeshwe kwa lugha ya Kiswahili na kuwataka maofisa wa serikali na mashirika ya umma kutumia lugha hiyo katika shughuli zao zote, kama vile vikao vya bodi, mawasiliano ya kiofisi, matangazo ya nafasi za kazi na mahojiano.
Mkuchika pia alitaka mbao za matangazo na nyaraka zinazobandikwa za taifa na sheria zote ziandikwe kwa lugha ya Kiswahili, ikiwa ni pamoja na kutafsiri zile zilizoandikwa kwa lugha ya kigeni.
Vilevile alitaka mijadala inayohusu shughuli za umma iendeshwe kwa Kiswahili, pia kumbukumbu zote zihifadhiwe kwa lugha ya Kiswahili, ikiwa ni pamoja na nyaraka zilizotumika katika mijadala kuandikwa kwa lugha hiyo.
Katika agizo hilo, serikali imevitaka vyombo vya habari vinavyotumia lugha ya Kiswahili kuhakikisha vinatumia Kiswahili sanifu na mwanana na kuzingatia kwa dhati sarufi ya Kiswahili.
Mkuchika alisema agizo hilo la serikali linazingatia matamko mbalimbali ya viongozi wa serikali wa awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu na umuhimu wa lugha ya Kiswahili, ikiwa sasa pia ni lugha ya kimataifa inayotumiwa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na yaliyotolewa na viongozi wa serikali kuhusu matumizi ya lugha hiyo.
Alisema Kiswahili ndiyo lugha pekee, ambayo huzungumza na kueleweka na idadi kubwa zaidi ya Watanzania nchini kote, pia ni chombo muhimu ambacho kimewaunganisha Watanzania wakati wa kupigania uhuru na ni kielelezo thabiti cha utamaduni wa Mtanzania na kitambulisho kikuu cha taifa.
Hivyo, hatuna budi kukikuza na kukiimarisha. Haikuwa kwa bahati nasibu kwamba Kiswahili kilitangazwa kuwa lugha ya taifa la Tanzania mwaka 1962, alisema Mkuchika na kuongeza:
Kwa kuzingatia matamko haya na umuhimu wa lugha ya Kiswahili, ikiwa sasa pia ni lugha ya Kimataifa inayotumiwa mathalan kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika, serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, inasisitiza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika shughuli za serikali na kutoa kauli kuzingatia vipengele vilivyosisitizwa awali.
Alisema matamko hayo ya viongozi wa serikali, yalianza kutolewa baada ya Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kulihutubia Bunge kwa mara ya kwanza kwa lugha hiyo Desemba 12, 1962.
Alisema baada ya hapo, mwaka 1967, aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais, Hayati Rashid Kawawa, alitoa waraka wa matumizi ya lugha hiyo kwa mawaziri, naibu mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya, walimu wote na watumishi wa serikali wote.
Mkuchika alisema pia mwaka 1974 aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi katika Rais, Utumishi, alitoa waraka wa utumishi namba moja wa mwaka 1974 ulioeleza kuhusu matumizi ya lugha ya Kiswahili katika ofisi za serikali.
Alisema vilevile, Mei 2005, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), William Lukuvi, aliagiza taarifa za mikutano, semina na warsha nchini zitolewe kwa Kiswahili kwa manufaa ya wananchi, pia taarifa za miradi inayohusu wananchi ni lazima zitolewe kwa lugha hiyo ikiwa ni pamoja na vipeperushi na nyaraka zinazohusu miradi hiyo.
Mkuchika alisema katika kikao cha Baraza la Mawaziri cha Februari 18, mwaka huu, Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, alisisitiza suala la matumizi ya lugha ya Kiswahili katika shughuli za serikali na kuwakumbusha watendaji serikalini kuzingatia waraka wa Hayati Mzee Kawawa alioutoa alipokuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais.
---Tangu Tanzania ilipopata uhuru mwaka 1961 kutoka Uingereza, serikali imekuwa ikiendesha shughuli nyingi kwa lugha ya Kiingereza.
Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, zimekuwa zikitolewa kauli na viongozi mbalimbali wa serikali kutaka Kiswahili iwe lugha rasmi, ikiwemo kufundishia kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu.
CHANZO: Nipashe